Wednesday, November 15

Ripoti inayoeleza unyanyasaji wa Watanzania Uarabuni ilivyozuiwa Dar

Ofisa Mawasiliano wa Shirika la Human Rights
Ofisa Mawasiliano wa Shirika la Human Rights Watch, Audrey Wabwire akiwaonyesha wandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kitabu kilicho na Ripoti inayoangazia watumishi wa ndani kutoka Tanzania wanaopelekwa nchini Oman . Picha na Omar Fungo 

Dar es Salaam. Maofisa wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) wamezuia kuzinduliwa kwa ripoti ya unyanyasaji wa watumishi wa ndani wa Kitanzania nchini Oman na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Ripoti hiyo inatokana na utafiti uliofanywa na Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu (Human Rights Watch) ilitakiwa kuzinduliwa saa nne asubuhi jana katika ukumbi wa Holiday Inn.
Hata hivyo kabla ya kuzuiwa ripoti hiyo ilikuwa imeshasambazwa kwa waandishi wa habari.
Ofisa mtafiti wa Costech, Dk William Kindeketa alisema walilazimika kuzuia ripoti hiyo kwa sababu watafiti hawakufuata taratibu zinazotakiwa.
“Kwetu sisi utafiti wowote ule unaofanyika uwe wa kijamii au kisayansi, Costech ndio wenye mamlaka ya kupitisha,” alisema.
Dk Kindeketa alisema taratibu hizo ni kuandika dokezo, kujaza fomu na wasifu wa taasisi au shirika linalotaka kufanya utafiti.
Maofisa hao ambao baadaye waliwafukuza waandishi wa habari waliokuwa wamefika kwa ajili ya uzinduzi wa ripoti hiyo, walisema hadi watafiti hao watakapotimiza masharti yote ndipo wataruhusiwa kutoa ripoti.
Akiahirisha uzinduzi huo, ofisa mawasiliano wa Human Rights Watch, Audrey Wabwire alisema maofisa hao walifika tangu saa tatu asubuhi kwenye eneo la mkutano wa waandishi wa habari, wakafanya nao kikao lakini baadaye wakazuia kuzinduliwa kwa ripoti hiyo.
Kulikuwa na mvutano ambapo awali maofisa hao walizuia waandishi kuingia ukumbini lakini baadaye wanahabari waliruhusiwa kuingia huku wao wakitoka kabla ya kuzuia na kuwaondoa.
Katika ripoti hiyo ambayo tayari ilikuwa imeshasambazwa ilieleza kuwa watumishi wa Kitanzania wanaofanya kazi katika nchi hizo wanatimiza majukumu yao kwa saa nyingi za kazi, kutolipwa mishahara, ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa kimwili kinyume na haki za binadamu.
Katika ripoti hiyo yenye kurasa 99 iliyoandikwa ‘Kufanya kazi mithili ya roboti’, pia imeweka kumbukumbu ya namna watumishi hao wanavyonyanyasika na kutolipwa.
Mtafiti wa haki za wanawake Mashariki ya Kati wa Human Rights Watch katika ripoti hiyo, Rothna Begum amesema kwenye ripoti yake kuwa maelfu ya watumishi wa ndani wa Kitanzania wako Mashariki ya Kati. “Human Rights Watch ilifanya mahojiano na watu 87 ikiwa ni pamoja na maofisa wa Tanzania, vyama vya wafanyakazi, mawakala wa uajiri, watumishi wa ndani wanawake 50 wa Kitanzania ambao walifanya kazi Oman na UAE,” amesema. Ripoti hiyo imesema baadhi ya wahanga walidai kufanyishwa kazi kwa saa 21 kwa siku bila mapumziko, kula chakula kilichoharibika na wengine kunyanyaswa kimwili ikiwamo kulazimishwa kufanya ngono na kubakwa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo wote waliohojiwa walisema waajiri wao walitaifisha hati zao za kusafiria na kujikuta wakiwa na njia finyu za kujinasua na ukatili huo.
“Baadhi ya matukio haya ni sawa na kazi za shuruti au biashara haramu ya kusafirisha binadamu,” imeeleza sehemu ya ripoti hiyo.
Ripoti hiyo imeishauri Tanzania kuwa na mikakati maalumu ya kuzuia na kukabiliana na unyanyasaji wa watumishi hao ikiwa ni pamoja na kuandaliwa kwa kanuni kali zitakazoongoza ajira zao.
Pia, watafiti katika ripoti hiyo wanashauri kuwapo kwa programu za mafunzo ya haki na msaada wa kujitosheleza kutoka katika balozi za Tanzania ikiwa ni pamoja na kuwalipia gharama za tiketi za kurudi nyumbani wafanyakazi hao inapotokea unyanyasaji.
“Tanzania inapaswa kuhakikisha kwamba wanawake wanaweza kuhama kwa usalama kwa ajili ya kazi za ndani. Oman na UAE lazima zifanye kazi pamoja kuzuia unyonyaji wa watumishi wa ndani wahamiaji, kuchunguza unyanyasaji na kuwashtaki wale wanaohusika,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.

No comments:

Post a Comment