Wednesday, November 15

Sweden yaipa Tanzania msaada ya Sh 400 bilioni

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James 
Dar es Salaam.Sweden imeipatia Tanzania msaada wa Sh435 bilioni ili kuchangia katika bajeti ya Serikali na kuiwezesha sekta ya elimu.
Makubaliano ya msaada huo yametiwa saini leo Jumanne kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James na Mkuu wa Idara ya Ushirikiano wa Maendeleo Ubalozi wa Sweden nchini, Ulf Kallstig.
“Naomba ieleweke kwamba huu sio mkopo ni msaada, hatutakiwi kuurudisha,” amesema katibu mkuu baada ya kusaini mikataba mitatu.
Akifafanua, amesema kati ya kiasi hicho Sh159.4 bilioni zimetolewa na nchi hiyo ili kuisadia Serikali kuchangia kwenye bajeti yake ya 2017/18 hadi 2018/20.
Amesema fedha hizo zitasaidia kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani yanayohusu kodi na yasiyo ya kikodi.
Katika mkataba wa pili, Dotto amesema Sweden ameipatia Serikali Sh235.39 bilioni ili kusaidia elimu kwa kufuata vipaumbele vilivyopo.
“Unajua tangu Serikali imeanza kutoa elimu bure imekuwa ikitenga bajeti kubwa katika elimu kushinda sekta nyingine ndiyo maana marafiki zetu wameamua kutusaidia,”amesema.
Amesema sekta ya elimu imekuwa ikitengewa asilimia 18 ya bajeti yote ya Serikali na kuifanya sekta hiyo kuongoza kwa kuwa na kiasi kikubwa cha fedha.
Jamese amesema katika mkataba wa tatu, Sweden imetoa Sh40.72 bilioni ili kuongeza katika mradi wa kuwaelimisha watoto waliokosa elimu ya msingi kwa sababu ya matatizo mbalimbali.
Amesema Sweden imekuwa ikisaidia fedha kwa ajili ya kuwapa elimu watu wa aina hiyo tangu mwaka 2015 hivyo imeamua kuongeza fedha.
“Msaada huu unaonyesha namna nchi hizi mbili zilivyo na ushirikiano,” amesema.
Amesema mbali na msaada huo, Sweden imekuwa ikiisaidia Tanzania katika sekta mbalimbali zikiwemo za nishati na uwezeshaji katika tafiti.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Ushirikiano wa Maendeleo Ubalozi wa Sweden nchini, Kallstig amesema elimu ndiyo msingi wa maendeleo katika nchi zote.
Amesema ndiyo maana nchi hiyo imekuwa ikisaidia sekta ya elimu na inafurahishwa na mageuzi ya elimu yanayofanyika hapa nchini.

No comments:

Post a Comment