Harun Ahmed ni mmoja tu kati ya maelfu ya vijana kutoka Ethiopia ambao wamejaribu kufunga safari ndefu kupitia jangwa la Sahara hadi Libya, lengo lao kuu likiwa kufika Ulaya.
Sasa ana miaka 27 na huishi Ujerumani.
Amesimulia BBC jinsi alivyonunuliwa na kuuzwa mara tatu na wafanyabiashara ya kuuza watumwa.
Baadhi ya nyakati, alizuiliwa miezi kadha na waliokuwa wamemteka, akateswa na hata kunyimwa chakula.
Hii ndiyo hadithi ya maisha yake.
Nilizaliwa wilaya ya Agarfa katika eneo la Bale jimbo la Oromia nchini Ethiopia.
Niliondoka Ethiopia kwenda Sudan mwaka 2013.
Baada ya kuishi mwaka mmoja na miezi kadha Sudan, nilianza safari kwenda Libya nikiwa na wahamiaji wengine - tulilipa dola 600 kila mmoja kwa waliokuwa wanatusafirisha.
Tulikuwa watu 98 kwenye lori.
Tulisafiri kwa siku sita katika jangwa la Sahara na tukafika eneo moja katika mpaka wa Misri, Libya na Chad ambapo wanaowasafirisha wahamiaji kubadilishana wahamiaji.
Tulikuwa tumekumbana na matatizo mengi safarini.
Kuna watu wenye silaha ambao wangetusimamisha huko jangwani ghafla na kutuibia kila kitu.
Watu walilazimika kuketi mmoja juu ya mwingine na joto lilikuwa kali ajabu.
'Hawakuwa kama binadamu'
Katika eneo hilo la mpakani, kundi la majambazi lilituteka nyara sote na kutupeleka Chad. Walitusafirisha kwa siku mbili jangwani na kutupeleka hadi kwenye kambi yao.
Walikuwa na silaha kali. Na walizungumza Kiarabu na lugha nyingine.
Walileta gari na kusema kwamba wale miongoni mwetu ambao wangelipa dola 4,000 kila mmoja wangeweza kupata fursa ya kuingia kwenye gari hilo.
Lakini wale ambao hawangeweza wangesalia humo kambini.
Hatukuwa na pesa hizo lakini tulizungumza wenyewe na kuamua kwamba tujifanye kwamba tulikuwa na pesa hizo tupate fursa ya kuingia kwenye gari hilo.
Tulisafiri kwa siku nyingine tatu na kufika eneo ambapo huwa wanawauza wahamiaji.
Wale waliotuchukua walitwambia kwamba walikuwa wametununua dola 4,000 kila mmoja na kwamba tusipowalipa pesa hizo basi hawangetwachilia.
Kulikuwa na wahamiaji wengine kutoka Somalia na Eritrea ambao walikuwa wamekaa huko kwa zaidi ya miezi mitano.
Walikuwa wameteswa na kuteseka sana. Hawakuonekana kama binadamu.
Tuliteseka sana pia.
Walitulazimisha kunywa maji moto yaliyokuwa yamechanganywa na mafuta ya petroli ili tuwalipe pesa haraka.
Walitupatia chakula kidogo sana, mara moja kwa siku.
Walitutesa kila siku.
Baadhi ya wahamiaji kutoka Somalia na Eritrea ambao walitumiwa pesa na jamaa zao walifanikiwa kuondoka.
Lakini Waethiopia 32, mimi nikiwepo, tulikaa huko kwa siku 80 kwa sababu hatungeweza kuwalipa.
"Hamtatulipa pesa zetu, hivyo tutawauza," wafanyabiashara hao walitwambia.
"Hatukuwa tunapata chakula kwa zaidi ya miezi miwili na tulikuwa tumedhoofika sana, kwa sababu ya hilo mwanamume ambaye walitupeleka kwake akatununue alikataa kutununua akisema, 'hata hawana figo'."
Mtu mwingine kutoka mji mmoja wa Libya unaofahamika kama Saba alifika na kutununua dola 3,000 kila mmoja.
Lakini huko Saba, baada ya kusafiri kwa siku nne, tulifanyiwa mateso ya kikatili.
Walitutesa na kutufunga vifungashio vya plastiki vichwani, kutufunga mikono yetu nyuma mgongoni, na kuturusha kichwa kwanza ndani ya mitungi mikubwa iliyokuwa imejaa maji.
Walitupia kwa kutumia nyaya.
Baada ya mwezi mmoja wa mateso na kupigwa, baadhi yetu tulifanikiwa kuwasiliana na jamaa na marafiki kwa simu na kupata dola 3,000 ambazo tulitakiwa kulipa.
Walituruhusu kuondoka lakini kabla hatujafika mbali, watu wengine walitushambulia na kutufungia katika jumba moja kubwa, lililofanana na ghala la kuhifadhia mizigo.
Walitwambia kwamba tusipowalipa dola 1,000 kila mmoja, hawangetuachilia.
Tuliendelea kuteswa na kupigwa. Tuliwapigia jamaa zetu nyumbani tena na kuwaomba watupe pesa tena. Waliuza mifugo, mashamba na mali yao nyingine waliyokuwa nayo na kututumia pesa hizo.
Hadhi ya wakimbizi
Baadaye, tulikwenda mji wa Trablois ambapo wahamiaji wengi huishi.
Hali huko ilikuwa heri kidogo.
Tulifanya kazi kwa miezi kadha, kazi zozote ambazo tungepata na kisha tukavuka bahari ya Mediterranean kwenda Ulaya.
Mwanzo nilifika Italia na kisha nikavuka na kuingia Ujerumani.
Namshukuru Mungu kwamba nilifanikiwa kupata stakabadhi zangu kama mkimbizi na maisha yamekuwa mazuri hapa, lakini siwezi kusahau niliyoyapitia.
Kusema kweli, nilichokosa nilipokuwa naondoka nchini mwangu ni ujuzi na maarisa.
Ningekwenda shuleni au hata nifanye kazi huko.
Niliwaona watu wengine wakiondoka na hilo, pamoja na hali ya siasa, ilinishawishi nami kuondoka na kuikimbia nchi yangu.
Tulimzika mmoja wa marafiki zetu katika mpaka wa Misri na Libya.
Wengine wawili waliachana nasi tukiwa Saba; sijui kama wako hai au la.
Msichana mwingine alitumbukia kwenye bahari ya Mediterranean lakini wengine walifanikiwa kufika Ulaya.
No comments:
Post a Comment