Wednesday, November 29

MAONI YA MHARIRI: Tusikubali nguvu kazi hii ikapotea kizembe


Taarifa kwamba kundi linaloathirika zaidi na maambukizi mapya ya VVU ni vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 24, ambao ni sawa na asilimia 40 ya watu wanaopata maambukizi kwa mwaka zinashtua. Zinashtua zaidi inapoelezwa kwamba kati yao, asilimia 80 ni wasichana na asilimia 20 ni wavulana, hivyo kufanya katika kila vijana 10 wenye maambukizi mapya ya VVU, wanane kuwa wasichana na wawili wavulana.
Si hivyo tu, lakini hali ya maambukizi mapya kwa sasa ya takriban watu 55,000 kwa mwaka, huku asilimia 40 wakiwa ni vijana inasikitisha na kutufanya kama Taifa kufikiria mara mbilimbili juu ya ugonjwa huo. Lakini hali hiyo inatishia kundi ambalo ‘grafu’ yake inazidi kupanda la vijana ambao huchukua asilimia 40 kwa kila idadi ya watu wanaoambukizwa kwa mwaka, lakini kinachosikitisha ni kwamba ukichukua kundi la vijana asilimia 80 ni watoto wa kike.
Takwimu hizo ambazo zilitolewa juzi na mkurugenzi mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Leonard Maboko, zinaashiria kwamba kuna tishio kubwa la afya za vijana ambao ndio wachapazi na walengwa wakubwa wa kusaidia kunyanyua uchumi wa Taifa hili.
Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba wanaoathirika kwa kiasi kikubwa ni wasichana ambao licha ya kuwa na jukumu la kusaidia nchi katika mambo mbalimbali, pia ndio wazazi wa siku za usoni na walezi wa karibu wa kizazi kijacho.
Maboko, ambaye alikuwa akizungumza wakati wa kuzindua mkakati wa Taifa wa kondomu na wiki ya maonyesho na huduma kuelekea maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani Desemba Mosi, ni kama alitonesha kidonda ambacho mara nyingi wananchi hujisahau kukitibu mpaka kipone. Tunasema hivyo kwa sababu maambukizi mapya ya Ukimwi yalipaswa kupungua zaidi na hata kutokuwa tishio tena kwa kizazi kijacho, lakini kwa idadi hii ya vijana wanane kati ya 10 wenye maambukizi kuwa ni wasichana inaumiza zaidi. Bado jukumu la wazazi liko palepale katika suala la malezi ili kukiepusha kizazi hiki na balaa hili, kwa kuwa wao ndio walio karibu zaidi na watoto wanaowazaa na wanaowalea.
Haiwezekani tunaposema Ukimwi upo, na maambukizi ndiyo kama haya, kisha wazazi wakajitenga katika kutoa miongozo sahihi kwa watoto wao juu ya afya zao na hasa kupitia mazungumzo ya kifamilia.
Ni vyema jamii ikarejea enzi za mababu zetu ambao jukumu la malezi ya watoto walilipa kipaumbele cha aina yake. Mathalan, kulikuwa na mihadhara ya kijamii, vikao vya kifamilia na hata mazungumzo ya ana kwa ana baina ya wazazi na watoto wao juu ya masuala yanayogusa maisha yao.
Kupitia mazungumzo hayo, watoto na hasa vijana wenye rika la balehe walipata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali watakayokabiliana nayo maishani mwao na namna ya kuyaepuka. Huo ndio uliokuwa msingi sahihi zaidi wa malezi.
Hata hivyo, jamii ya sasa ambayo imetawaliwa na utandawazi imejitenga na utamaduni huo kiasi kwamba imefika mahali ni nadra kwa mama au baba kukaa na watoto kuzungumzia suala la afya ya uzazi, magonjwa ya zinaa na mambo mengine ya ‘kikubwa’ na hasa katika kukabiliana na changamoto zinazoambatana nayo. Ni kutokana na hali hiyo, wapo wazazi wachache wenye uthubutu hata wa kutaja neno “kondomu” mbele ya watoto wao na namna ya kuzitumia ili kujikinga na magonjwa ya zinaa.
Ni vyema wazazi wakasimamia wajibu wao ipasavyo wa kukilea kizazi hiki ipasavyo huku wakiwaeleza kwa uwazi watoto juu ya afya ya uzazi na namna ya kuepuka magonjwa ya zinaa.

No comments:

Post a Comment