Wednesday, November 29

Ocean Road yazungumzia ongezeko la upatikanaji dawa


Dar es Salaam. Taasisi ya Saratani ya Ocean Road imesema upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kwa sasa ni asilimia 80 kutoka asilimia nne mwaka 2015.
Akizungumza leo Jumatano Novemba 29,2017 katika mazungumzo na Bohari ya Dawa (MSD), Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Dk Julius Mwaiselage amesema upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi awali ulikuwa ni tatizo katika utendaji na changamoto kwa wagonjwa ambao walilazimika kununua dawa kwa bei ghali.
"Mwaka 2015 taasisi ilikuwa ikipata dawa, vifaa tiba na vitendanishi kwa asilimia nne, sasa ni asilimia 80. Haya ni matokeo ya ongezeko la bajeti ya dawa na utendaji wa MSD," amesema.
Dk Mwaiselage amesema bajeti ya taasisi hiyo mwaka 2015 ilikuwa Sh790 milioni kwa mwaka na sasa ni Sh7 bilioni.
David Lyimo anayeuguza ndugu yake katika taasisi hiyo ameiambia MCL Digital kuwa, “Taarifa ambazo awali tulikuwa tukizisikia kuhusu kero ya dawa hapa Ocean Road kwa sasa hatujaikuta. Mgonjwa anapatiwa dawa isipokuwa aina moja pekee ndiyo  tunatakiwa kwenda kununua.”
Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu amesema taasisi hiyo inatambua kuwa dawa za saratani ni gharama lakini atahakikisha zinaendelea kupatikana kwa wakati.
Amesema suala la vifaa vya maabara ni tatizo linalohitaji mpango wa kitaifa.
Bwanakunu ambaye pia ametembelea hospitali za Amana, Mwananyamala na Sinza Palestina amehimiza watoa huduma katika hospitali hizo kutambua jukumu walilonalo katika usimamizi wa matumizi ya dawa na vifaa tiba.
Akiwa Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala, Bwanakunu amesema anazitambua changamoto zilizopo za usambazaji wa dawa na vifaa tiba.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Palestina Sinza, Chrispin Kayola amesema hali ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika hospitali hiyo kwa sasa ni asilimia  80 
"Changamoto iliyopo ni uhaba wa vitendanishi vya maabara na vifaa vya macho na meno ambavyo tunapata chini ya kiwango, hivyo havikidhi mahitaji," amesema.

No comments:

Post a Comment