Tuesday, November 14

Mufti Menk asema magaidi hawawakilishi Uislam

Mufti Menk (katikati)akipokelewa na viongozi wa serikali alipowasili uwanja wa ndege mjini Mombasa. Kushoto Waziri wa Utalii Najib Balala na kulia ni Ali Hassan Joho ambaye ni Gavana wa kaunti ya Mombasa.
Msomi na mhubiri maarufu wa Kiislam Ismail Menk amesema wanaoendesha ugaidi siyo Waislam halisi.
Akizungumza katika hafla maalum mjini Mombasa nchini Kenya siku ya Jumapili, Menk mwenye shahada ya digrii katika somo la sharia za kiislamu alisema wanaoendesha ugaidi sio waislamu halisi.
“Hauwezi kuwa na nia ya kumdhuru mwenzako halafu ukajiita muislamu. Mtu yeyote anayefanya hivyo sio muislamu halisi, na dini haitambui tabia hiyo kabisa” Alisema.
Mufti Menk mwenye umri wa miaka 42 na mzaliwa wa mjini Harare nchini Zimbabwe amejizolea sifa kote duniani kutokana na mahubiri yake yanayolenga zaidi masuala ya kijamii.
Ugaidi ni changamoto kubwa inayolikumba bara la Afrika na ulimwengu mzima. Wakati mjadala kuhusu ugaidi ukiendelea, baadhi ya viongozi wa dini ya kiislamu wamepata shutuma mbalimbali kwa madai ya kuchochea tabia hiyo.
Hatua hii imepingwa vikali na msomi na pia muhubiri maarufu wa kiislamu Ismail Mufti Menk aliyezuru Afrika Mashariki wikendi hii.
Hatua yake ya kuzuru Kenya hasa mji wa Mombasa imetajwa kuwa ya manufaa makubwa kwani eneo hilo limeathirika pakubwa kutokana na changamoto ya uhasama baina ya waislamu na wasio waislamu.
“Kitabu kitakatifu kinatuhimiza kuishi vyema na majirani zetu hata kama sio waislamu.” Alisisitiza.
Katika ziara hiyo aliandamana na gavana wa jimbo la Mombasa Hassan Ali Joho pamoja na waziri wa utalii nchini Kenya Najib Balala.
Wakaazi wa mjini humo waliambia VOA kwamba ziara ya kiongozi huyo mwenye ushawishi mkubwa duniani ni faraja kwao na imesaidia kubadili dhana za wengi.
Licha ya kuwa maarufu Mufti Menk hata hivyo ameshutumiwa sana na baadhi ya mataifa ya barani ulaya kutokana na misimamao mikali katika mahubiri yake.
Mnamo mwaka wa 2013 alizuiwa kuingia nchini Uingereza alikotarajiwa kuzungumza na wanafunzi katika vyuo vikuu 6 nchini humo.
Mwezi October mwaka huu wa 2017 Singapore pia ilimnyima kibali cha kuingia nchini humo.
Katika mahubiri yake ameonekana kuwa na msimamo mkali dhidi ya mapenzi ya jinsia moja, ugaidi ndani ya uislamu pamoja na ukosoaji dhidi ya tabia zinazokiuka maadili katika jamii.

No comments:

Post a Comment