Tuesday, November 14

Watu milioni 1.25 wakumbwa na baa la njaa Sudan Kusini

Ripoti ya Umoja wa Mataifa inasema watu milioni 1.25 katika nchi inayozongwa na vita ya Sudan Kusini wanakabiliwa na baa la njaa.

Südsudan Hunger Symbolbild (picture alliance/ZUMA Press/M. Juarez Lugo)
Watu milioni 1.25 katika nchi inayozongwa na vita ya  Sudan Kusini wanakabiliwa na baa la njaa. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa ambayo imetolewa Jumatatu (06.11.2017). Ripoti hiyo imeeleza kuwa idadi hiyo ni mara mbili zaidi ya hali ilivyokuwa katika kipindi sawa na hiki mwaka uliopita. Serikali pamoja na maafisa wa kutoa misaada wameonya taifa hilo linaweza kutumbukia tena kwenye baa la njaa mwaka 2018.
Katie Rickard ambaye ni mratibu wa shirika la REACH nchini Sudan Kusini, shirika ambalo ni la utafiti wa misaada, na ambalo lilitoa data zilizotumiwa kuiandaa ripoti hiyo amesema kukithiri kwa upungufu wa chakula kunapaswa kuwafanya watu kuwa na wasiwasi kuhusu hali mbaya zaidi ya njaa katika sehemu nyingi nchini Sudan Kusini ifikapo mwaka 2018.
Maafisa wa mashirika yanayotoa misaada wanalaumu machafuko yanayoendelea Sudan Kusini ambayo yanakaribia kuingia katika mwaka wake wa tano, na ambayo yamesababisha vifo vya watu 50,000 kuchangia hali ya njaa nchini Sudan Kusini.
Mama akimpima uzito mtoto wake ambaye anakabiliwa na utapia mlo eneo la Panthau Sudan Kusini
Mama akimpima uzito mtoto wake ambaye anakabiliwa na utapia mlo eneo la Panthau Sudan Kusini
Shirika la Chakula Duniani WFP limesema mnamo Februari, nchi hiyo changa kabisa duniani ilitangaza hali ya kiangazi katika kaunti mbili zilizoko jimbo la Unity. Watu 100,000 katika kaunti hizo mbili walikuwa katika hatari kubwa ya njaa, lakini kupitia utabiri wa mapema, na mikakati kabambe, janga hilo liliepushwa.
Hali yatishia kuwa mbaya zaidi
Hata hivyo takwimu za hivi karibuni za Umoja wa Mataifa na pia kutoka halmashauri ya takwimu za Sudan Kusini kuhusu chakula na usalama zinaonesha hali ni mbaya.
Katika mwezi wa Septemba, watu milioni 6, ambayo ni aslimia 56 ya idadi jumla ya watu nchini humo walikuwa wakikabiliwa na njaa kali, 25,000 kutoka kaunti za Ayod na Greater Baggari wakikabiliwa na janga la kibinadamu.
kutanuka  kwa vita kumefanya uzalishaji wa vyakula kutowezekana na uwasilishaji wa vyakula vya msaada kuwa ngumu na hatari. Kaunti za Ayod na Baggari zinadhibitiwa na waasi, na wakaazi wanasema hali ni mbaya mno.
Mkaazi mmoja wa Baggari ambaye hakutaka kutambulishwa jina na ambaye hivi karibuni alikimbia na familia yake hadi mji ulioko karibu Wau kwa sababu hawakuwa na chakula, amesema "Tunakimbia nje kwa sababu ya njaa." Jamaa huyo mwenye umri wa miaka 52 na ambaye ni baba wa watoto wanne ameliambia shirika la habari la AP kuwa watu wanaaga dunia kwa sababu ya njaa na katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita, aliwaona watoaji misaada wakiingia Baggari mara tatu pekee.
Jamaa akichukua chakula baada ya kudondoshwa na ndege ya Umoja wa Mataifa
Jamaa akichukua chakula baada ya kudondoshwa na ndege ya Umoja wa Mataifa
Ameongeza kusema kuwa "kama serikali haitawaruhusu watu wanaokuja kusaidia, sisi tutafanya nini? Hatuna lolote, tunaweza tu kuomba"
Chakula kutumiwa kama silaha ya vita!
Isaiah Chol Aruai ambaye ni mwenyekiti wa halmashauri ya kitaifa kuhusu takwimu amesema "serikali haina sera ya kibaguzi na kwamba imejitolea kuwasaidia raia wa Sudan Kusini.
Makundi ya wanaharakati wa haki za binadamu yanazitaka pande zote husika katika machafuko kuyaruhusu mashirika yatoayo misaada kuweza kuwafikia watu mara moja na bila pingamizi
Pande zote mbili, ya serikali na upinzani zimetumia suala la chakula kama silaha ya vita, kuanzia kuwazuia raia kufikia chakula, kuzuia chakula kuwafikia raia, kupora mara kwa mara vyakula, masoko na nyumba za watu na hata kuwalenga raia wanaobeba kiasi kidogo cha chakula wanapopita katika maeneo ya mapigano. Hayo yamesemwa na Alicia Luedke ambaye ni mtafiti wa shirika la Amnesty International nchini Sudan Kusini.
Katika ziara yake ya kwanza nchini Sudan Kusini mwezi Oktoba, balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley alizusha wasiwasi katika mkutano wake na rais Salva Kiir kuhusu misaada kuwafikia raia.
Watu watafuta vyakula katika misitu
Baadhi ya watoto wapiganaji wa kundi la waasi katika kijiji masikini Lekuangule mashariki mwa Sudan Kusini. Picha hii ilipigwa 2015
Baadhi ya watoto wapiganaji wa kundi la waasi katika kijiji masikini Lekuangule mashariki mwa Sudan Kusini. Picha hii ilipigwa 2015
Huku msimu wa kiangazi ukiingia Sudan Kusini wakaazi na maafisa wa kutoa misaada wanatarajia hali kuwa mbaya zaidi.
Ripoti hiyo ya REACH imesema jamii zinazidi kufadhaika kuhusu jinsi ya kuzilisha jamii zao na watu wameanza kutumia mikakati ya kupindukia ya kustahimili, ikiwemo kuingia katika misitu isiyokalika na vinamasi kutafuta mimea ya misitu wakitafuta chakula.
Serge Tissot ambaye ni afisa wa shirika la  Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa amesema mwaka 2018 utakuwa mgumu na  njia pekee ya muda mfupi ya kuzuia hali kudorora ni "Amani.”
David Shearer ambaye ni mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini amesema mgogoro wa sasa kuhusu chakula nchini Sudan Kusini ni wa kujitengenezea. Ni kuhusu watu ambao wameyakimbia makwao kwa sababu ya machafuko. Shearer ameongeza kuwa sehemu nyingi za Sudan Kusini zimekuwa na  mvua za kutosha, kwa hivyo tatizo si  tabia nchi bali ni  vita.

No comments:

Post a Comment