Wednesday, November 1

Mkataba wa huduma ya maji wasainiwa


Arusha. Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe amewataka wakazi wa Jiji la Arusha kushiriki kikamilifu kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi.
Kamwelwe amesema hayo wakati wa utiaji saini mradi wa kuboresha huduma za maji safi na usafi wa mazingira jijini Arusha.
Mradi huo unaotarajiwa kuzalisha lita zaidi ya 200 milioni kwa siku utagharimu Sh476 bilioni, fedha ambazo zimetolewa na  Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania.
Amesema maendeleo hayana vyama, hivyo ni muhimu kwa kila Mtanzania kuhakikisha anashiriki katika juhudi za kutafuta maendeleo.
Waziri Kamwelwe jana Jumanne Oktoba 31,2017 alisema ni muhimu kwa kila mkazi wa Jiji la Arusha kuwa mlinzi wa miundombinu na kutoa taarifa inapobainika kuwepo viashiria vya kihujumu.
"Mradi huu umegharimu fedha nyingi, ni jukumu letu kuhakikisha miundombinu haiharibiwi au kuhujumiwa kwa namna yoyote ile," amesema.
Ameagiza vyanzo vya maji katika Bonde la Mto Pangani kulindwa na kuhifadhiwa kwa kuwa vingi vimeanza kukauka.
Kuhusu mkandarasi wa mradi huo, amemtaka kufanya kazi kwa ufanisi na kuzingatia muda. Amesema matarajio ni kuuzindua kabla ya mwaka 2020.
Akitoa taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha (Auwsa), Lucy Koya amesema mradi huo utakapokamilika utaongeza upatikanaji wa maji kutoka lita 40 milioni za sasa hadi lita 200 milioni kwa siku.
Amesema wakazi wa Arusha wanaopata huduma ya  maji itaongezeka kutoka watu 325,000 hadi 600,000.
Mradi huo unaotarajiwa kukamilika mwaka 2019 utahusisha uchimbaji wa visima virefu 11, ujenzi wa mabwawa ya kutibu maji taka, ukarabati na upanuzi wa mtandao wa maji safi na maji taka katikati ya Mji wa Arusha.
Akizungumzia mradi huo, Meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro amewataka wakazi wa Arusha kuitunza miundombinu hiyo.

No comments:

Post a Comment