Wednesday, November 1

Hoja ya Nyalandu ya Katiba kama moto wa nyika


Unaweza kusema Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu ameacha hoja ya kufufua mchakato wa Katiba Mpya mezani.
Hii ni baada ya kutoa uamuzi ulio kinyume na ahadi yake ya kuwasilisha bungeni Muswada Binafsi wa Sheria kuhusu mchakato huyo.
Hivi karibuni Nyalandu aliyepata kuwa waziri wa Maliasili na Utalii katika awamu ya nne, aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter, “Nakusudia kuwasilisha kwa spika wa Bunge Mh. Job Ndugai. Azma yangu ya kuleta muswada binafsi wa sheria katika kikao kijacho cha Bunge itakayoweka sharti la kurejea upya mjadala wa Katiba Mpya ya Tanzania, kwa kuzingatia rasimu ya Katiba kama ilivyowasilishwa na Tume ya Jaji Warioba.
Kabla hajatimiza ahadi hiyo ameamua kujiuzulu ubunge na hivyo kukosa fursa hiyo. Pengine ndio ulikuwa mpango wake au kuna jambo limejitokeza katikati na kuvuruga mpango huo, lakini ukweli unabaki kuwa hoja hiyo imebaki mezani kwake.
Bila shaka watajitokeza wabunge wengine jasiri na kuibeba huku Nyalandu mwenyewe akipambana nayo kivingine baada ya kubadili jukwaa la siasa.
Wazo la kupeleka hoja hiyo bungeni lilikuwa jipya kabisa na lenye ngumu hasa linapotolewa na mbunge wa CCM, lakini kwenye majukwaa mengine lipo na linaendelea.
Sasa ni takribani miaka mawili tangu mchakato wa Katiba mpya ukwame huku hoja za jinsi ya kujinasua katika mkwamo huo zikiwa bado kitendawili.
Wadau mbalimbali wamekuwa wakiishinikiza Serikali ya CCM kufufua na kuhitimisha mchakato huo, kwa kuzingatia Rasimu iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji mstaafu Joseph Warioba.
Mjadala uliopamba moto sasa, ni wa kuhoji ni wapi mchakato huo unapaswa kuanzia.
Wakati baadhi ya wadau wanasema urudi nyuma na kuanzia ilipoishia Tume ya Jaji Warioba, wengine wanasema uendelee kwenye hatua ya kura ya maoni kwa kutumia Katiba Inayopendekezwa.
Wanaopendekeza Katiba Inayopendekezwa iliyopitishwa na Bunge Maalumu la Katiba iwekwe kando wanadai ni kwa sababu iliacha maoni mengi ya wananchi na kuingiza masilahi ya makundi na vyama vya siasa.
Katikati ya mijadala hiyo, Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF) iliwakutanisha wachambuzi na wasomi mbalimbali katika mdahalo wa kushauriana juu wa kuhamasisha, kusisitiza, kulinda na kudumisha amani, umoja na maridhiano nchini.
Miongoni mwa wachambuzi hao ni Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Ernest Kadiva anayekosoa mchakato uliopita wa Katiba akibainisha kosa lililofanyika ni kuwashirikisha wanasiasa na makundi mengine yaliyoweka kando masilahi ya Taifa na kutanguliza masilahi yao binafsi.
Anabainisha kinachopaswa kufanyika sasa kuwa ni kuyaweka pembeni makundi yaliyoshiriki awali na kutafuta wataalamu wachache, watakaotumia utaalamu wao kuhakikisha Taifa linapata Katiba Mpya yenye kubeba maoni ya wananchi ndani ya muda mfupi.
“Wataalamu hawa waongozwe na rasimu ya Tume ya Warioba kwani nyaraka hiyo ilitokana na maoni ya wananchi.
Wataalamu hawa wanapaswa kuwa wachache ambao hawatazidi 50 ili kuzuia matumizi makubwa ya fedha za walipa kodi wa Taifa hili,” anasema Mchungaji Kadavi.
“Ukiweka wanasiasa na watu wa makundi mengine tutarejea kwenye mkwamo unaotukabili sasa kwani watatanguliza masilahi yao badala ya masilahi ya Taifa. Kama ni sisi viongozi wa dini tutataka mambo yetu yaonekane, lakini tukiwatumia wataalamu, watatuandikia Katiba mpya tena nzuri kwelikweli.”
Kiongozi huyo wa kiroho, anasema tunapaswa kuheshimu maoni ya wananchi waliyoyatoa na tukubali kuambiana ukweli ili tuweze kupata Katiba mpya.
Anasema yote hayo yatawezekana ikiwa viongozi watakubali kukaa na kuzungumza na kupata mwafaka wa jinsi ya kutoka tulipo na kujikwamua kwenye mkwamo unaotukabili.
“Hata Mungu mwenyewe alimshusha mwanaye kuja kuzungumza na sisi, kuzungumza ni jambo kubwa na lenye tija. Tunapokaa na kuzungumza kila mtu anakuwa na nafasi ya kubainisha mambo kulingana na upeo wake, na ndiyo sababu hata kwenye ngazi ya familia mazungumzo yanapokosekana, familia huyumba,” anasema Mchungaji Kadavi.
Anasema tofauti na kipindi cha mfumo wa chama kimoja, mfumo wa vyama vingi unahitaji mazungumzo na maridhiano ili kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa.
Kwa upande wake Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum anasema ingawa hakufuatilia mchakato huo kwa undani hadi ulipofikia, lakini Watanzania ndiyo wenye maamuzi kuhusu mwelekeo mpya wa mchakato huo.
“Wananchi ndiyo wanaopaswa kuamua kama uendelee au usiendelee na hatua ambayo unapaswa kuanzia. Viongozi wanapaswa kuheshimu maamuzi ya Watanzania, huwezi kuua mawazo ya Watanzania kutokana na maamuzi waliyokwishayafanya,” anasema Sheikh Salum.
Wakati wachambuzi hao wakitoa kauli hizo, Jaji Warioba aliyeongoza Tume kukusanya maoni ya wananchi anasita kutoa maoni yake sasa akisema ipo siku atazungumzia suala hilo kwa undani zaidi.
Lakini, badala yake anaamua kutoa maoni kuhusu amani ya nchi akiwataka viongozi wa kisiasa kujenga utamaduni wa kukutana mara wanapogundua mambo yanayoashiria kuwepo dalili za uvunjifu wa amani nchini na kuwataka waige mafanikio yaliyofikiwa na viongozi wa dini.
“Viongozi wa dini wamekuwa na kawaida ya kukutana kila wanapoona mambo hayaendi sawa jambo ambalo ni zuri na linapaswa kuendelea, wanasiasa nao waige mfano huu mzuri wa viongozi wa kiroho,” anasema.
Warioba ambaye ni Jaji mstaafu amesema kuna viashiria vya kutoweka kwa amani na viongozi wa kiserikali na kisiasa wanapaswa kukutana na wenzao wa upinzani ili kutafuta maelewano na maridhiano kwa masilahi ya taifa.
“Amani ikivunjika, itakuwa shida kuirudisha na kuiendeleza. Viongozi hasa wa kisiasa waache malumbano kwani tukiendelea hivi wanaweza kutufikisha kubaya,” anasema Warioba na kuongeza.
“Waache kujibishana kwa kutumia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari. Hatuwezi kuendesha nchi kwa kujibizana kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, viongozi wanapaswa kukutana, kuzungumza na kuridhiana.”
Anawataka washiriki wa kongamano hilo, kujadili matatizo yanayolikumba taifa na kupeleka ujumbe kwa viongozi husika kuhusu umuhimu wa wao kukutana na kuzungumza.
Katika hilo, Sheikh Salum anasema kauli ya Jaji Warioba imetolewa katika kipindi mwafaka na inapaswa kufanyiwa kazi, huku akibainisha siri ya mafanikio yao ni dhamira ya dhati waliyonayo kutumia jukwaa la mazungumzo kumaliza tofauti zao.
“Sisi tunayo kamati ya amani inayojumuisha viongozi wa dini zote nchini. Kamati hii hukutana mara kwa mara kujadili na kuafikiana namna ambavyo tutatoa mchango wetu katika kuendeleza amani nchini mwetu,” anasema.
Anawataka wanasiasa wakutane pasipo kuogopana na kubainisha kuwa watu wanaojuana hawapaswi kuogopana kwani hakuna mtu mwenye hatimiliki na Taifa hili, hivyo wakutane na kuzungumza.
“Wote ni Watanzania, kukosoana ndio ubinadamu na hakuna binadamu aliyekamilika, Tanzania ya amani inapaswa kuendelea,” anabainisha.
Mbali maoni hayo, msomi wa masuala ya siasa, Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu Katoliki Ruaha- (Ruco) anaelezea umuhimu wa kufikia makubaliano kabla ya mchakato wa Katiba kufufuliwa.
“Tunapaswa kukubaliana kuwa sasa mchakato uanze na tuanze na rasimu ya Jaji Warioba. Haihitaji kusubiri kwani rasimu iliyoandaliwa na iliyokuwa Tume ya katiba ilikuwa na mambo mengi mazuri ikiwemo tunu za taifa na mengine, hivyo mchakato unapaswa uanze mara moja,” anasema Profesa Mpangala.
Profesa Mpangala anaungwa mkono na Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), James Mbatia anayesema, “hatuhitaji kuwa na nchi inayoongozwa kwa matakwa ya watu, msingi mkubwa uwe ni Katiba ya wananchi itakayopatikana kwa majadiliano na maridhiano ya pamoja.”
“Maoni ya Tume ya Jaji Warioba yarudishwe na yatuongoze kupata Katiba mpya kwani taifa lenye mgogoro haliwezi kuendelea na niwasihi vyama wenzangu, CCM, Chadema, CUF, ACT- Wazalendo na vingine wawe tayari kwa majadiliano,” anaongeza Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi.
Huu si mjadala pekee unaogusa mchakato wa katiba na Rasimu ya Warioba, hata Jukwaa la Katiba limekuwa linazungumzia suala hilo mara nyingi kama ambavyo pia imekuwa hoja ya kudumu ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

No comments:

Post a Comment