Karibu kila siku jua linapochomoza kuanza safari yake ya kutoka Mashariki kwenda Magharibi ukifungua redio, ukiangalia runinga au ukisoma habari za magazeti na mitandaoni hadithi kubwa ni moja tu.
Nayo ni ya unyanyasaji, ubakaji, unyama na ujahili usioelezeka wanaofanyiwa watoto, unaokithiri kwa kasi katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Hata kuviita vitendo hivi ni unyama bado hujavipa maelezo yanayostahiki kwa sababu hata wanyama wakubwa na wakali huonyesha huruma na imani kwa wanyama wadogo.
Kwa mfano sijaona au kusikia katika umri wangu pandikizi la jogoo kumbaka kifaranga. Kubwa zaidi hata anapotaka kufurahisha mahitaji yake ya kimwili kwa kuku mwenye vifaranga jogoo huondoka shingo upande likitunisha mbawa kuonyesha kwamba koo huyo bado analea.
Lakini baada ya balaa la kusambaratisha mikutano ya wanaume wanaodaiwa kushabikia kuingiliana kimwili kati yao, pamezuka wimbi kubwa na lenye dhoruba la vijana na hata wazee kuwafanyia uchafu usioelezeka watoto wadogo wa kike na kiume.
Kinachosikitisha zaidi ni kwamba miongoni mwa wanaofanya huu udhalilishaji unaoweza kusema ni laana, ni wazee na wana wa familia na ungetarajia hivi vitoto kukimbilia kwao na kukumbatiwa kwa upendo. Lakini loo, salaale … huko ndiko unakoweza kusema kukimbia kuungua ndani ya kikaango na kutumbukia kwenye moto mkali wa vifuu vya nazi.
Maskini watoto wetu, wamegeuzwa mayatima wasiokuwa na walezi wa kuwategemea pale wanapopata shida.
Katika orodha ndefu ya matokeo zaidi ya 10 katika wiki moja iliyopita Unguja na Pemba, watu wazima zaidi ya miaka 50 na wengine wenye familia wamewanajisi watoto wadogo waliokuwa kwa raha na furaha wakiwaita babu.
Hapo mwanzo uchafu huu ulionekana kukithiri mijini, lakini sasa umetapakaa hata vijijini. Kwa mfano kule Pemba, katika Kijiji cha Kiungoni yupo mzee mmoja anayedaiwa kuwabaka watoto wake watatu wa kambo.
Maskini mama mzazi wa watoto hawa. Alipopata mume alitegemea kumsaidia kulea vitoto vyake kumbe kaingia katika tanuri la kumharibia wanawe.
Alipoolewa huyu mama aliona kama kaondokana na joto la karai liliokuwa jikoni liliokuwa na maisha magumu, lakini kumbe ametumbukia kwenye tanuri la moto la kumharibia wanawe.
Katika Kijiji cha Mkokotoni, Kaskazini Unguja, zimesikika taarifa za mtoto wa kiume wa miaka mitano kubakwa na kwenda kufanyiwa uchafu usioelezeka na kurudishwa nyumbani kwao alfajiri akiwa ameharibiwa vibaya sana.
Kwa tukio hili la Mkokotoni tunaambiwa hayo yamefanywa na hao ambao siku hizi wamepewa jina la watu wasiojulikana.
Hapa yanazuka maswala mengi, kama nini hasa kilichosababisha kuwepo hali hii mbaya Visiwani?
Mengine ni wanaofanya haya wanapata raha gani, nini lengo lao, nini kinafanyika kudhibiti hali hii na hatua gani zinafaa kuchukuliwa haraka kupunguza maafa zaidi siku za usoni.
Kwa kweli yapo mengi yanayolizunguka suala hili, kama ngoma ya mduara ambapo mchezaji kila akizunguka anajikuta anarudi palepale alipoanzia.
Lakini hii haina maana kuachia huu mzunguko kuendelea, lazima ukatwe kwa sababu si mzunguko wa kheri na hauna manufaa kwa Zanzibar na watu wake.
Kwanza ni vyema kukubali bila ya kutafuna ulimi au kupepesa macho kuwa maadili yameporomoka sana Visiwani na yanahitaji ukarabati mkubwa, kama si ujenzi mpya.
Hii litawezekana kwa kuongeza elimu ya kidini na dunia kwa jamii ili watu wawe na uelewa mpana wa suala hili lilivyo na athari zake za hivi sasa na baadaye.
Ni kwa kuwa na jamii yenye uelewa ndio itawezekana kupiga hatua moja mbele. Nayo ni kila mtu kuwa mchungaji wa haki za mtoto, kuachana na ukimya juu ya suala hili, kuondoa muhali kwa wanaotenda na kushabikia kwa ati mhusika ni ndugu, jamaa au rafiki yangu au kwa miaka mingi tumeishi vizuri na wazee wake.
Hapahapa suala la huruma, wema wala hisani bali haki. Hata siku moja haki haiwezi kufunikwa na kawa la wema na hisani. Haki lazima itafutwe na ipatikane kwa gharama yoyote ile.
Elimu pia iongezwe katika shule na madrasa ili watoto wawe na uelewa mzuri wa kuwepo janga hili na wajue njia za kujikinga na wafanye nini anapotokea mshenzi anayetaka kuharibu maisha yao.
Katika nchi nyingi za wenzetu hili inafanyika na
imepata mafanikio. ujifunze kutokana na uzefu wao.
Vyombo vyetu vinavyosimamia sheria, yaani polisi, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na mahakama nazo ziongeze kasi ya zionekane zinajitahidi kuhakikisha wakati wote haki inatendeka.
Wachache miongoni mwetu waliomo katika taasisi hizi ambao wanatiliwa mashaka ya kukosa uadilifu wawekwe kando ili wenye nia njema ya kunusuru maisha ya watoto wapate nafasi ya kusonga mbele. Lakini pia sheria zilizopo zimulikwe na kuangaliwa kama zinakidhi haja ya kuikabili hali hii.
Kwa muda mrefu kuna malalamiko juu yakesi hizi kuchukua muda mrefu na hata mashahidi kuchoka na nenda rudi mahakamani ya kesi kuahirishwa. Suala la posho ya usafiri kwa mashahidi nalo litupiwe jicho la huruma.
No comments:
Post a Comment