Harare, Zimbabwe. Taarifa za hivi punde kutoka vyanzo vya ngazi ya juu ni kwamba Rais Robert Mugabe “anajiandaa kujiuzulu” baada ya usiku uliotawaliwa na mlio wa risasi na makazi yake kuzingirwa na jeshi.
Hakuna maelezo zaidi isipokuwa Jeshi limesema asubuhi leo kwamba Rais Mugabe na mkewe Grace wamehifadhiwa mahali na kwamba linalinda usalama wa ofisi za serikali na linafanya doria kwenye mitaa mbalimbali baada ya usiku wa ghasia uliohusu kuzingirwa kwa majengo ya shirika la utangazaji la Zimbabwe (ZBC).
Matukio ya usiku kucha yamesababisha watu kuvumisha kwamba yamefanyika mapinduzi huku wanaounga mkono hatua hiyo wakisifu kwamba ni “marekebisho yasiyo ya umwagaji damu.”
Askari wenye silaha wakiwa kwenye magari yao walijipanga kwenye maeneo muhimu katika jiji la Harare na asubuhi Wazimbabwe walionekana kwenye mistari mirefu kwenye mabenki kwa lengo la kuchukua fedha utaratibu ambao hutokea mara nyingine kunapotokea mgogoro wa kifedha.
Wengine walionekana wakitazama simu zao kusoma habari juu ya jeshi kunyakua madaraka huku wengine wakienda kazini.
Katika hotuba iliyorushwa asubuhi baada ya kudhibiti shirika la utangazaji, msemaji wa jeshi alisema jeshi limewalenga “wahalifu” wanaomzunguka Mugabe na liliwahakikishia raia kwamba utulivu utaimarishwa.
Shauku ya kujua alipo Mugabe, 93, na mkewe ilikuwa kubwa lakini inaelekea wamewekwa chini ya kizuizi cha jeshi. "Usalama wao ni wa uhakika," amesema msemaji wa jeshi.
"Tunapenda kuweka wazi kuwa jeshi halijatwa madaraka,” alisema msemaji wa jeshi. "Sisi tunawalenga wahalifu wanaomzunguka (Mugabe) ambao wanafanya uhalifu na kusababisha mateso ya watu kijamii na kiuchumi nchini na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria."
No comments:
Post a Comment