Wednesday, November 29

Halmashauri zatakiwa kuwatumia mafundi wazawa


Dar es Salaam. Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Joseph Kakunda ameziagiza halmashauri kutumia mafundi wa kawaida wazawa katika maeneo yao kutekeleza miradi midogo.
Kakunda ametoa agizo hilo baada ya kufanya ziara wilayani Mkalama mkoani Singida alikotembelea mradi wa maji Iguguno na Shule ya Sekondari Iguguno.
“Matumizi ya wakandarasi yabaki katika miradi mikubwa, lakini yote midogo tuwatumie mafundi waliopo katika maeneo yetu. Mafundi hawa wazawa wanatekeleza kazi kwa ubora kama huu ambao nimeuona kwa gharama ambazo ni za kawaida,” amesema.
Kakunda katika taarifa iliyotolewa leo Jumatano Novemba 29,2017 na ofisi ya katibu tawala Mkoa wa Singida amesema mradi wa Shule ya Sekondari ya Iguguno ambao unajumuisha ujenzi na ukarabati wa madarasa manane, mabweni mawili, vyoo vyenye matundu 11, bwalo na maabara umegharimu Sh416 milioni na unatosha kudhihirisha kuwa mafundi wa kawaida wazawa wanaweza kufanya kazi nzuri.
“Mradi huu endapo tungetumia utaratibu wa wakandarasi na wazabuni Sh416 milioni zingekuwa kama robo ya gharama, nasisitiza wakandarasi na wazabuni watumike katika miradi mikubwa tu,” amesema.
Pia, ameipongeza halmashauri kwa kutekeleza mradi wa maji ambao umewezesha huduma kupatikana katika kata yote ya Iguguno.
Awali, mbunge wa Mkalama, Allan Kiula alisema changamoto kubwa inayowakabili ni kutokuwa na hospitali ya wilaya.
Kiula amesema pia kuna upungufu wa watumishi katika sekta za elimu na afya unaokwamisha baadhi ya shughuli kufanyika kwa kasi inayotakiwa.

No comments:

Post a Comment