Wednesday, November 29

Lissu asherehekea miaka 20 ya ndoa kitandani Nairobi

Nairobi/Kenya. Utafanya kitu gani ukitimiza miaka 20 ya ndoa? Au ulifanya nini ulipotimiza miaka hiyo ya ndoa?
Kuna ambao hutumia siku ya kumbukumbu ya ndoa zao kwenda kwenye nyumba za ibada kumshukuru Mungu na wengine hufanya sherehe kwa kualika ndugu, marafiki na majirani.
Kila mmoja huwa na utaratibu wake ambao huambatana na uwezo wa kiuchumi ili kuiweka kumbukumbu hiyo ya ndoa vizuri na ndio maana kuna ambao hufanya sherehe kubwa na wengine hukumbuka kwa ‘maneno tu’.
Iwe ni kumbukumbu ya miaka mitano, 10 au 15, huwa ni muhimu kutafakari muunganiko wa watu wawili ambao wameishi pamoja wakipita milima, mabonde na kuvuka vihunzi vingi.
Iwe ni kwa sherehe au ‘maneno makavu’ tu, siku hiyo huwa ni muhimu kuitafakari na ikiwezekana wawili hao, huwa wanatathmini walikotoka na wanakokwenda.
Lakini, mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu na mkewe Alicia, wana stori tofauti kuhusu kumbukumbu ya ndoa yao.
Leo Jumatano, Novemba 29, Lissu na Alicia wanatimiza miaka 20 ya ndoa yao, lakini wanatafakari safari hiyo ndefu ya muunganiko wao wakiwa mazingira tofauti;Hospitali ya Nairobi.
Wanaweza kuitumia siku ya leo kulishana keki, lakini Lissu anatimiza siku 84 akiwa Hospitali ya Nairobi huku mkewe, Alicia akiwa kando ya kitanda kumhudumia kwa siku zote hizo.
Lissu aliyepigwa risasi zaidi ya 30 akiwa ndani ya gari lake nje ya makazi yake Area D mjini Dodoma Septemba 7, mwaka huu anazungumzia kumbukumbu ya miaka 20 akiwa amejilaza kitandani hospitalini hapo katika mahojiano na Mwananchi.
 “Mke wangu nikuzungumziaje? Lissu anamuuliza Alicia ambaye anamjibu, “kazi kwako.”
“Mke wangu mpenzi anaishi kiapo chake tulipooana Novemba 29, 1997,  tunatimiza miaka 20 …tulipooana nilimsikia anasema ‘kwa shida na raha, nitampenda, nitafanya nini na nini’, kwa hiyo mke wangu mpenzi anaishi katika kiapo chake,” anasema Lissu akiwa mwenye tabasamu.
 “Katika miaka hii 20, tumepitia majaribu mengi sana, lakini hili (kupigwa risasi) ndilo kubwa kuliko yote na nafikiri kama ni mtihani, mke wangu ameufaulu kwa daraja la juu kabisa kwa sababu amekuwepo hapa muda wote na mara nyingine ukimsikia anavyozungumza ana msimamo mkali kuliko mimi niliyeumizwa,” anasema mwanasheria huyo.
 “Ni mke wa kweli, aliyekubali kuchukua majukumu ya kuwa mke, najisikia faraja na furaha ya kipekee kwa sababu ya kuwa naye na ninamwomba tuendelee kuwa hivyo kwa miaka 20 mingine inayokuja,” anasema Lissu huku pembeni yake mkewe akitabasamu.
Anatumia muda huo kumpa ujumbe mke wake kuwa, “najisikia mwanamme mwenye bahati sana kuwa naye, ni mwanamke wa kipekee sana kuwa naye, tumetoka mbali sana na hii miaka 20 imekuwa mizuri sana katika maisha yangu kwa sababu ya kuwa naye.”
Alicia hakuacha mazungumzo hayo yapite hivi hivi tu, alikuwa na mtazamo wake kuhusu safari hiyo ya miaka 20.
“Miaka 20 ni mingi, lakini nikifikiria ni kama juzi tu, halafu nilikuwa sitaki kumkumbusha nilitaka kumfanyia ‘surprise,’” anasema huku Lissu akimsikiliza kwa makini na kutabasamu.
Alicia, ambaye kitaaluma ni wakili anasema, “lazima niwe mkweli kuna miaka mingine ilikuwa busy anasahau hata siku…Tundu ni mume wangu, kikubwa naweza kusema ni rafiki yangu wa karibu sana wa miaka mingi sana, nikiwa msichana mdogo, mrembo na smati, tumekuwa tukiishi hivyo.”
“Ujumbe wangu, Tundu siku zote aendelee kuwa Tundu tu, Tundu wa kabla ya tukio na baada ya tukio awe ni Tundu niliyemjua siku zote,” anasema.
Tundu Lissu ambaye ni Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), ametimiza siku 84 tangu alipopigwa risasi mjini Dodoma na kusafirishwa kwa ndege kwenda kutibiwa katika Hospitali ya Nairobi.

No comments:

Post a Comment