Rais wa 16 wa Marekani, Abraham Lincoln alipata kusema: “Uchaguzi ni kwa ajili ya watu. Kwa hiyo watu wenyewe wanatakiwa kuachwa waamue, ikiwa wanaamua wao wenyewe kukalia moto, itawalazimu kukaa kwenye malengelenge ya moto.”
Mwaka 1997, Liberia waliamua kukalia moto kwa kumchagua Charles Taylor kuwa Rais wao licha ya kuonywa sana. Miaka miwili baadaye (1999), Liberia ilirejea kwenye vita vya pili ya kiraia na kusababisha vifo vya watu wanaotajwa kufikia 300,000. Kilichowakuta Liberia ndiyo kukalia malengelenge ya moto.
Uchaguzi si kuangalia matakwa ya wakati peke yake, bali jicho pana linapaswa kumulika kizazi kinachokuja. Uharibifu wa uchaguzi una tafsiri ya moja kwa moja kuwa haki ya watu inaingiliwa. Hasara kubwa zaidi ni kutoa mafunzo mabaya kwa watoto.
Aprili mwaka jana baada ya kutimiza mwaka mmoja ofisini, Mwanasheria mkuu wa 83 wa Marekani, Loretta Lynch, alipohojiwa na waandishi wa habari wa Texas, kuhusu kesi za uchaguzi ambazo huibuka kwenye majimbo mbalimbali, alisema shabaha kuu ya uchaguzi lazima iwe kuheshimu matakwa ya watu.
Lynch alisema: “Kupiga kura ni namna ya kushiriki katika jamii za kiraia. Iwe kwa Rais, iwe kwa uchaguzi wa manispaa. Ni jinsi ambavyo tunawafundisha watoto wetu kuhusu uchaguzi wakiwa shuleni, namna ya kuwa raia na umuhimu wa sauti zao.”
Ukishika maneno ya Lincoln na Lynch, utaweka akilini kwamba uchaguzi ni mali ya watu. Tatizo wanasiasa hujidanganya kwa kudhani kwamba uchaguzi ni mali yao na hujaribu kupora. Huharibu mchakato au kuvuruga hatua ya kuhesabu kura, hivyo kusababisha matokeo yaliyo kinyume na matakwa ya watu.
Mipango ya wanasiasa kwenye uchaguzi ipo sawasawa na maneno ya dikteta wa zamani wa Urusi na Dola ya Umoja wa Nchi za Kisovieti (USSR), Joseph Stalin aliyesema kuwa matokeo hayaamuliwi na wanaopiga kura, bali wanaohesabu.
Stalin alisema: “Inatosha tu watu kujua kuwa kulikuwa na uchaguzi. Watu wanaopiga kura hawafanyi uamuzi wowote. Wanaohesabu kura ndiyo humaliza kila kitu.”
Maneno hayo ya Stalin ndiyo ambayo yameteka akili za wanasiasa, kwamba hata kama hawajachaguliwa lakini ukifanyika udanganyifu kipindi cha kuhesabu kura na kuwapa ushindi atafurahia japokuwa anajua si haki. Wao huwaza kuwa wanawakomoa washindani wao, wakati ni kuwakosea heshima wananchi.
Wananchi ndiyo hupaza sauti kupitia masanduku ya kura kwamba ni kiongozi gani wanamtaka. Inapotokea anayetangazwa ni tofauti na waliyemchagua maana yake haki za watu zinaingiliwa, vilevile ni kuwasumbua watu kupanga foleni kupiga kura wakati matokeo yapo kwa wanasiasa na ndiyo mwanzo wa vurugu na ghasia.
Uchaguzi wa madiwani
Jumapili iliyopita (Novemba 26), kulifanyika uchaguzi mdogo wa madiwani kwenye kata 43 zilizokuwa wazi kutokana na sababu mbalimbali. Kilichojiri kwenye uchaguzi huo ndicho kinatuleta kwenye mjadala, je, wanasiasa wapo kwa ajili ya uchaguzi wa wananchi?
Ghasia, vitimbi na wingi wa malalamiko siku ya uchaguzi ni kipimo dhahiri kuwa wanasiasa walikuwa wakichuana kutafuta ushindi nje ya matakwa ya watu. Maana kama sauti za wananchi ndizo zenye kutakiwa kuamua, haiwezekani kusuguana kiasi hicho bila sababu.
Matukio ya watu kuumizwa, wengine kukamatwa na polisi, malalamiko ya mawakala wa vyama ama kuzuiwa au kuondolewa kwenye vituo vyao, ni kielelezo kwamba ushindi unatafutwa kwa njia aliyoisema Stalin kuwa wapigakura hawana cha kuamua, kazi yao ni kupiga kura tu.
Uchaguzi huu wa madiwani umetia fora kwa kulalamikiwa kwa wingi na hata kususiwa maeneo mengi kuliko wakati wowote ule katika historia ya nchi. Ukifika hapo unaweza kujiuliza swali; imekuwaje hali iwe hivyo wakati huu?
Bila hata kupima ukweli wa malalamiko na hoja za kujitoa kwa maeneo ambayo wagombea walijitoa, kila mpenda demokrasia na amani atajiuliza maswali zaidi ya matatu; kwa nini malalamiko? Kwa nini wahusika wakose dirisha la mazungumzo mpaka rabsha zitawale? Ni kama zinajengwa zama za uchaguzi ni kufa au kupona. Kwa njia hiyo, ni somo gani ambalo vijana na watoto wanapewa?
Katika hali ya kawaida, wanasiasa wanapogombea, ushiriki wao kwenye uchaguzi na namna yao ya upokeaji matokeo, ni ujenzi wa kizazi cha viongozi wenye kuheshimu uamuzi wa watu kupitia sanduku la kura.
Ikiwa tunakuwa na wagombea ambao wanashiriki uchaguzi wakitegemea msuli wakati wa kuhesabu na kufanya majumuisho ya kura kuliko kujinadi kwa sera na kushawishi wapiga kura kwa matarajio bora, nchi itakuwa na wagombea wapenda fujo. Kile ambacho hufundishwa shuleni kuhusu demokrasia ya uchaguzi, nguvu ya sanduku la kura, ndicho mtoto au kijana anatakiwa kushuhudia nyakati za uchaguzi, lakini sasa kujana huyo anashuhudia mambo tofauti.
Leo anaona lugha za vitisho na viapo vya damu ili kulinda kura. Mtoto akikua na kutamani kuwa kiongozi, hatakuwa mgombea mstaarabu. Wanasema mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.
Uharibifu wa nchi na watoto wetu kwa sababu ya uchaguzi ni ubinafsi na kuhatarisha nchi. Maisha ya binadamu katika kizazi kimoja ni wastani wa miaka 60, ikizidi sana ni miaka 80, lakini nchi itaishi miaka mingi ijayo kama ambavyo imeshaishi, hivyo hatutakiwi kujali mambo yetu kuliko ustawi wa nchi yetu.
Hali mbaya kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 43 ni kipimo kuwa wanasiasa ni wabinafsi na hawataki kufanya siasa na uongozi wenye kukijenga kizazi kijacho. Watoto wa shule ya msingi na sekondari wanashuhudia watu wakitoana damu, ni kama kuwafundisha kuwa siku zijazo wafanye siasa kwa damu.
Ustaarabu katika kufanya uchaguzi kwa amani, utulivu na mzani wa uhuru na haki wakati wa kupiga na kuhesabu kura, hauji wenyewe, hutokana na nidhamu ya viongozi waliopo katika kutambua na kuheshimu sauti za watu pale wanapoamua kinyume na matakwa yao.
Nidhamu hiyo inahitajika pia kwa wapinzani pale wanaposhindwa, badala ya kukimbilia kulalamika kuwa wameibiwa kura na kuanzisha zogo, wanatakiwa kuwa wepesi kukubali matokeo yenye kuonyesha wameshindwa. Huko ndiko kukijenga kizazi cha wanasiasa na viongozi wakweli na waaminifu.Kiongozi wa vuguvugu la kudai uhuru wa India, Mahatma Gandi analiweka vizuri hili la ustaarabu wa kupokea matokeo kama yalivyoamuliwa na wapigakura aliposema: “Kushinda au kushindwa kwenye uchaguzi havina maana yoyote mbele ya kuibakisha nchi ikiwa imara.”
Hatari iliyopo
Uchaguzi umefanyika katika kata 43 na matokeo yameonesha kuwa kata 42 zimekwenda CCM na Chadema wameshinda moja. Kwa matokeo yaliyotangazwa au haki ambayo imepatikana kila upande inavyoweza kujengewa hoja. Swali ni moja; je, haki imeonekana kutendeka?
Malalamiko ni sehemu ya kwanza ya kukaribisha tafsiri kuwa haki haijaonekana kutendeka. Ingekuwa walalamikaji wameibua malalamiko baada ya matokeo kutangazwa, pengine ingekuwa rahisi kutafsiri kuwa wanachokilalamikia ni fikra baada ya kushindwa.
Lakini katika sehemu nyingi malalamiko yalianza mapema, Arumeru Mashariki, Arusha, kulikokuwa na uchaguzi wa kata nne, Chadema ilitangaza kujitoa wakidai kubaini hujuma. Ukijumlisha na taarifa nyingine, unaona dhahiri kwamba mazingira hayakumrahisishia mwananchi kuamua.
Mambo hayo ya vurugu kwenye uchaguzi yanapaswa kulaaniwa na kila mtu. CCM waliopata ushindi mkubwa, wasijipongeze tu, bali wakemee udhaifu huo uliojitokeza. Waonyeshe kujuta, maana wao kama chama kinachoongoza nchi wanawajibika zaidi kuilinda Tanzania kwa ajili ya kizazi kijacho.
Uchaguzi mdogo wa madiwani umepita. Unakuja uchaguzi mdogo wa ubunge katika majimbo matatu ambayo yapo wazi, mwaka 2019 uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu 2020.
Tusifanye vyama kuingia kwenye uchaguzi kama majeruhi ambao wanaweza kuamua kujitetea na kusababisha ghasia zitokee kwenye vituo vya majumuisho ya kura. Nani haioni hatari ya damu kumwagika? Mfumo wa utoaji haki yenye kuonekana ukiwekwa katika chaguzi zetu tutazuia hisia za kufa au kupona kwenye uchaguzi.
No comments:
Post a Comment