Nimeamua kuuliza maswali yafuatayo, maana ni lazima atokee mtu wa kuyauliza. Haiwezekani tukasubiri miti na mawe kuuliza maswali haya. Kila Mtanzania aliyesoma, kila anayeguswa na uhai wa taifa letu ni lazima aulize maswali haya.
Nimeamua kuuliza maswali haya maana tunaelekea kujenga utamaduni wa kushangaza, utamaduni wa kusema “Yakitokea nitakuwa nimeondoka”; utamaduni wa kuishi leo bila kufikiria maisha ya vizazi vijavyo.
Tunaitaka Tanzania ya leo bila kuweka maanani Tanzania ya kesho na keshokutwa; tunaipiga kisogo historia ya Baba zetu waliopigana kufa na kupona ili tupate uhuru, ili tuishi kwa heshima kama binadamu na kuurithisha uhuru huu na neema zote kwa vizazi vijavyo.
Nimeamua kuuliza maswali haya kwa vile tumejenga utamaduni wa kuogopana na kuoneana aibu; tumejenga utamaduni wa kutanguliza vyama vya siasa badala ya kulitanguliza taifa letu.
Tumejenga utamaduni wa kuwatanguliza marafiki zetu na ndugu zetu badala ya kulitanguliza taifa. Ni lazima ajitokeze mtu wa kusema liwalo na liwe. Ni lazima ajitokeze mtu wa kukemea na kuonya.
Kuna rafiki yangu wa karibu ameniambia leo hii Tanzania hakuna wa kusimama na kukemea, maana sote tumetumbukia katika shimo la ufisadi; kama wewe si fisadi basi ndugu, rafiki au jamaa wa karibu atakuwa anajishughulisha na ufisadi.
Ukibahatika kuwa na ndugu, jamaa na marafiki wasiokuwa kwenye mchakato wa ufisadi, basi chama chako cha siasa au taasisi unayoshughulika nayo itakuwa inajishughulisha na ufisadi.
Ninauliza maswali haya nikijua wengine wataguswa, wataumia na kuchukia, nazingatia ukweli kwamba baadhi yao ni rafiki na ndugu zangu wa karibu; sipendi kabisa kuwasaliti, lakini kwa suala la kitaifa niko tayari kumsaliti baba, mama, kaka, dada na rafiki wa karibu. Nauliza maswali haya kwa kutambua kwamba taifa letu limeanza kuyumba.
Maswali yenyewe
Inakuwaje watumishi wa umma kushiriki kwenye kampeni za uchaguzi? Wanafanya hivyo kwa vile wao ni wanachama wa CCM au kwa vile wao ni watumishi wa umma? Kama wanafanya hivyo kwa vile wao ni wanachama wa CCM, je, walikuwa kwenye likizo?
Tunaweza kuhakikishiwa bila shaka yoyote kwamba walikuwa kwenye likizo? Kama walikwenda huko kama watumishi wa umma, je ni hatua gani imechukuliwa dhidi yao? Ni sahihi kwa mtumishi wa umma kutumia muda wa kutoa huduma kwa wananchi ili kufanya kampeni zenye manufaa kwa chama chake? Je, maadili ya utumishi wa umma yanamruhusu mtumishi wake kuacha majukumu yake kufanya mambo mengine kama vile ya chama chake na familia yake?
Leo hii wamefanya kampeni za chama chao, kesho wanaweza kutakiwa kuendesha shughuli za familia, ukoo au kabila lao. Mipaka iko wapi ya mfanyakazi wa umma kufanya kazi zake na kufanya kazi za umma?
Kama walikwenda huko kama watumishi wa umma, je, ni fedha za walipakodi zilizotumika kuwalipia usafiri, malazi na posho? Hili linaweza kuonekana kama swali la kijinga, lakini kwanini uwajibikaji usianzie hapo? Ni ipi mipaka ya mtumishi wa umma, ni lini yuko huru kufanya mambo binafsi?
Nauliza: Ni sahihi mtumishi wa umma kutambulishwa rasmi kama mwanachama wa chama cha siasa? Katibu mkuu wa wizara yoyote ile ni mtumishi wa umma. Inawezekana, yeye kama binadamu na kama Mtanzania, ana mapenzi na chama chochote cha siasa. Lakini je, ni utaratibu mtumishi wa umma kuwa kada? Huyu atawatendea haki Watanzania wote, bila kwanza kuangalia maslahi ya chama chake cha siasa?
Nauliza: Ni sahihi Rais wa nchi, ambaye ni kiongozi wa Watanzania wote, akiwa kwenye kazi za kitaifa, na wala si kazi za chama, kukipigia debe chama chake? Au kuwapokea wanachama wapya, ambao kwa kiasi kikubwa wanatoka kwenye vyama vingine vya siasa? Kwa mfumo huu, Rais atawatendea haki Watanzania wote, bila kuangalia kwanza maslahi ya chama chake?
Tumemsikia Rais akirudia mara kwa mara kwamba maendeleo hayana chama! Lakini kila kukicha anawapokea wanachama wapya wanaohama kutoka vyama vingine na kujiunga na chama chake. Hii ni kweli kwamba maendeleo hayana chama?
Nauliza: Muhimu ni chama cha siasa au ni Taifa? Tushughulikie nini, kuendeleza vyama vya kisiasa au kuliendeleza taifa letu la Tanzania? Wenye mawazo yanayofanana, mfano kwa suala wa ufisadi, kwanini wasiungane na kuwa na sauti moja hata kama wanatoka vyama tofauti?
Tunashuhudia kwamba baadhi ya wabunge wa vyama vya upinzani wana mawazo yanayofanana juu ya ufisadi. Lakini saa ikiwadia, vyama vinakuwa na nguvu zaidi ya utaifa. Tunajua wazi kwamba ndani ya vyama vya upinzani kuna watu wenye mawazo kama yale ya Rais Magufuli. Hawapendi ufisadi! Na kwa vile maendeleo ya taifa letu hayana chama, kwa nini watu hawa wasibaki kwenye vyama vyao vya upinzani na kujenga nguvu za pamoja kupambana na ufisadi? Kwani ni lazima waingie CCM ndipo wapambane na ufisadi?
Nauliza: Je, tunaifuata Katiba yetu? Je, tunailinda na kuitetea Katiba? Sote tunafahamu kwamba Katiba hiyo inatambua uwepo wa mfumo wa vyama vingi vya siasa. Katiba yetu inatambua uwepo wa demokrasia. Lakini tunasikia na kushuhudia “uhamaji”, watu wakihama kutoka chama kimoja na kujiunga na kingine.
Mbaya zaidi wanahama wale ambao kuhama kwao ni lazima Taifa, liingie kwenye gharama za uchaguzi. Mfano, madiwani wanaohama na wengine tunasikia wananunuliwa. Hatuwezi kusema uchaguzi wa jana, ndio mwisho, bado wengine wataendelea kuhama na tutaendelea kutumia fedha nyingi kuwachagua hawa watu muhimu katika mfumo wa serikali za mitaa. Kama Katiba yetu inatambua uwepo wa vyama vingi vya siasa, ina maana gani watu kuhama vyama baada ya uchaguzi? Kazi ya diwani ni kushughulikia maendeleo ya kata yake na kuisimamia Serikali kwenye ngazi ya Halmashauri ya wilaya. Diwani anaweza kuifanya kazi hii akiwa upinzani au chama tawala. Lakini wimbi la kuhama, na hasa katika utawala huu wa awamu ya tano, ni lazima utufikirishe zaidi. Ina maana sasa hivi udiwani ni zaidi ya udiwani?
Tumeshuhudia vurugu nyingi kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani. CCM ina madiwani wengi ukilinganisha na wale wa vyama vya upinzani. Labda, kama CCM, wanataka wao wawe na madiwani wote na wabunge wote, vinginevyo kuna haja gani, CCM kupambana kufa na kupona kwenye chaguzi hizi ndogo ambazo hata wapinzani wakipata madiwani wote bado hata hawafikii nusu ya wale wa CCM?
Kama ni kweli maendeleo hayana chama na Tanzania ni yetu sote, tunajenga nyumba mmoja, kwanini tugombanie fito kiasi cha kuumizana kama tulivyoshuhudia kule Arumeru?
Swali langu la mwisho:
Nauliza: Ni nani anatupumbaza na kutuaminisha kwamba Tanzania ni nchi maskini? Wimbo uliozoeleka kwenye masikio ya kila Mtanzania ni kwamba Serikali yetu haina fedha: Watu kule vijijini hawana huduma ya maji kwa vile Serikali haina fedha.
Kila ikisomwa bajeti, maelezo yanayofuata ni kwamba Serikali haina fedha, hivyo haiwezi kutekeleza kila lengo na tegemeo la wananchi. Kwa ufupi ni kwamba Serikali yetu haina fedha, ni Serikali Maskini inayotegemea misaada kutoka nchi za nje. Ni kweli Tanzania ni maskini? Naomba jibu!
Nauliza: Je, si kweli kwamba wimbo huu wa Serikali haina fedha umetufikisha mahali pa baadhi ya watumishi wa Serikali kama walimu kutolipwa mishahara na mafao yao kwa wakati, wastaafu kutolipwa kwa wakati, Serikali kushindwa kutoa mikopo kwa baadhi ya wanafunzi wa elimu ya juu, serikali kukwepa wajibu wake wa kutoa huduma kwa wananchi kwa kisingizio cha ubinafsishaji na ushirikishwaji wa wadau katika maendeleo.
Haya yanajitokeza katika kutoa elimu kwa umma, matibabu, huduma za kusimamia usafiri, kilimo, kuanzisha na kuvisimamia viwanda, kutoa elimu ya uraia na kulinda haki za wanaonyanyaswa kama vile watoto, wanawake, walemavu.
Nauliza: Swali langu ni juu ya ukweli huu kwamba serikali yetu haina fedha. Hivi ni kweli au ni matatizo yaliyo kwenye vichwa vyetu. Iwe vipi nchi tajiri kama Tanzania; ardhi kubwa ya kilimo na ufugaji, maziwa, mito na bahari kwa wingi wa samaki, misitu yenye mbao na wanyama wa kila aina, madini mengi iwe maskini? Umaskini huu unatoka wapi? Nani anayaweka mawazo haya ndani ya vichwa vyetu? Nani huyu anayetaka kutuaminisha kwamba sisi ni maskini, hatujiwezi ili afanye mbinu za kutuibia kila kitu?
Nauliza: Inakuwa vipi Serikali maskini, isiyokuwa na fedha za kuendesha huduma kwa watu wake, iwe na magari ya kifahari, iwe na uwezo wa kuwatibu wakubwa Ulaya, iwe na uwezo wa kununua ndege ya rais, iwe na uwezo wa kuwasafirisha watendaji wake daraja la kwanza kwenye ndege, iwe na uwezo wa kuwatunza watendaji wake kifahari?
Mbona matumizi ya Serikali hayaonyeshi umaskini wa aina yoyote ile? Kwanini tuendelee kuomba kufikia hatua ya kupoteza heshima yetu kama binadamu?
Nauliza: Kwanini Serikali haina fedha, lakini chama tawala kina fedha? Mipango ya Serikali inakwama, huduma kwa wananchi zinakwama, lakini mipango ya chama haikwami na huduma kwa wanachama wa CCM hazikwami. Ni imani yangu kwamba kila Mtanzania mwenye uchungu na taifa letu, ni lazima ajiulize maswali kama ninayojiuliza mimi. Nani anaendesha dola? Serikali au chama?
No comments:
Post a Comment