Saturday, November 4

AMOTEGRA WAJITOSA UCHUMI WA VIWANDA


JUMUIYA ya Wahitimu wa Shule ya Sekondari ya Ufundi Moshi (AMOTEGRA), wamejitosa kikamilifu kushiriki katika uchumi wa viwanda ili kuwaingizia kipato pamoja na ujenzi wa taifa lao kupitia uwekezaji wa miradi mbalimbali hasa inayozingatia utunzaji wa mazingira.
Kwa mujibu wa Katibu wa Kamati ya Mipango, Fedha na Uwekezaji, Emil Mkaki, wakati akiwasilisha ripoti ya mwaka ya mkutano mkuu wa jumuiya hiyo uliofanika mjini Dar es Salaam hivi karibuni, alisema Amotegra imepanga kutoa kipaumbele katika miradi mikubwa mitatu itakayosaidia kufikiwa kwa malengo hayo.
“Kwa kuanzia tumepanga kuanza na mradi wa uwakala wa bima, utengenezaji wa nishati mbadala ya mkaa kwa kutumia makaa ya mawe na nyinginezo pamoja na huduma mbalimbali za maofisini.
Akaongeza: “Hii pia italisaidia taifa katika kuepuka uharibifu wa mazingira kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye, kwa kuepusha ukataji miti ovyo na kusafisha mazingira kwa kutumia taka kavu ambazo tunashuhudia zikitupwa ovyo kwenye miji yetu.”
Kwa mujibu wa Katibu wa Amotegra, Masunya Nashon, katika mwaka 2018 jumuiya hiyo inatarajia kukusanya shilingi 138,250,000 kutoka vyanzo mbalimbali ikiwamo ada, miradi mbalimbali na wafadhili, ambazo sehemu kubwa zitatumika kuendeshea miradi, uzinduzi wa jumuiya na kumlipa mfanyakazi.
Katika mazungumzo tofauti, Mweka Hazina, Philomena Franco pamoja na mwanajumuiya Subira Upurute, walisema ni wajibu wa kila mmoja kutoa michango kwa wakati ili kuimarisha uanachama na kufanikisha malengo ya kuanzishwa kwa umoja huo.

No comments:

Post a Comment