Saturday, November 4

NAPE: KUHAMA KWA NYALANDU KUMENISHTUA

ALIYEKUWA Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, amesema uamuzi wa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu, kuondoka ndani ya chama hicho, umemshtua na kwamba si wa kuupuuza.
Nape aliyasema hayo alipotafutwa na MTANZANIA Jumamosi jana, baada ya andiko lake la kwenye mtandao wa twitter kuibua maswali, na hata kujenga hisia kwamba pengine alikuwa hakubaliani na uamuzi huo wa Nyalandu.
Akiwa ameambatanisha na picha inayomwonyesha akiwa na Nyalandu na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Nape aliandika: Chama cha siasa ni itikadi, itikadi ni imani. Siamini sana katika kubadili imani kienyeji. Nitashughulikia mapungufu nikiwa ndani.
Akifafanua andiko lake hilo, Nape alisema si kwamba alikuwa akibeza uamuzi wa Nyalandu, la hasha! bali alikuwa akitaka kueleza msimamo wake wa kutoondoka CCM baada ya kuwapo kwa ramli nyingi dhidi yake.
“Nyalandu ni rafiki yangu, ni ndugu yangu kwa sababu anatokea Singida na mimi mama yangu anatokea huko, sipondi uamuzi wake, sibezi, lakini imani yangu mimi kuhusu kuhama chama ni tofauti,” alisema Nape.
Nape, ambaye ni Mbunge wa Mtama kupitia CCM, tangu Rais Dk. John Magufuli amwondoe katika baraza lake la mawaziri amekuwa akitoa kauli ambazo kwa upande mwingine zimejenga hisia kama ataondoka ndani ya chama hicho na zaidi uamuzi wa sasa wa Nyalandu ndio uliochochea hali hiyo.
Katika hilo, alisema kuhama si jambo dogo na kwamba Nyalandu amechukua uamuzi mkubwa sana, vinginevyo hajui thamani ya uamuzi huo.
“Uamuzi wa kuhama chama hauwezi kuwa na sababu moja, bahati nzuri yeye ametoa sababu zake…mimi sina sababu hata moja ya kuhama CCM,” alisema Nape, huku akisisitiza kuwa, hajapata kuota wala kuwazia atafukuzwa ndani ya chama hicho na kwamba yeye ni muumini wa kubadilisha hali akiwa ndani.
Pamoja  na hilo, huku akirejea andiko lake jingine la kwenye twitter, Nape alihoji andoke CCM aende wapi? Kwa Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa? Mtu ambaye kwa zaidi ya miaka kumi amekuwa akiamini si msafi.
Alisema kamwe hawezi kuchukua uamuzi huo wa kwenda upinzani au kumfuata Lowassa, kwani hata dhamira yake itamsuta na zaidi akiamini bado CCM haijapata mbadala wake kiitikadi, umakini nk.
Alipoulizwa yeye binafsi aliposikia uamuzi huo wa Nyalandu alipata taswira gani, Nape alisema ulimshtua, kwa kuwa
hakutarajia mwanasiasa huyo kuondoka ndani ya chama hicho, kwani hakuwahi kumsikia hata siku moja akizungumzia suala hilo.
Akijibu swali kama kada wa CCM kwa miaka 16 anaangaliaje kuondoka kwa mtu kama Nyalandu, Nape alisema si jambo la kulipuuza na kufanya hivyo ni kujidanganya.
Wakati Nape akisema hayo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, alimponda Nyalandu akisema walikwishamweka pembeni siku nyingi, kwa kuwa hakuwa mtu muhimu kwao.
Polepole, ambaye alikuwa akizungumza kupitia Kituo cha Televisheni ya Channel Ten, zaidi ya kumtakia kila la heri, alisema Nyalandu amejimaliza yeye mwenyewe.
Kwa upande wake Nape, alipoulizwa anazungumziaje hoja sita zilizotolewa na Nyalandu kama sababu za yeye hasa kuondoka ndani ya chama hicho, alisema zinazungumzika na kusisitiza kuwa si busara kuzipuuza.
Katika hilo, alisema si busara kuzipuuza si tu hoja za Nyalandu, bali hata zile ambazo zimekuwa zikitolewa na wapinzani, kwani yeye anaamini ni wabia katika nchi.
“Hoja zake ingewezekana zikapata majibu, si vizuri kuzitupa wala kutukoroga,” alisema Nape.
Wakati akitangaza kujivua uanachama wa CCM mapema wiki hii, Nyalandu, ambaye alipata kuomba ridhaa ya kugombea urais kwa tiketi ya CCM katika uchaguzi uliopita, alizitaja hoja sita zilizomsukuma kuchukua uamuzi huo, ikiwamo kutoridhishwa na mwenendo wa hali ya kisiasa nchini, ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa haki za binadamu na ongezeko la vitendo vya dhuluma wanavyofanyiwa baadhi ya Watanzania.
Nyalandu, ambaye amepata kuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara kabla ya kushika wadhifa wa uwaziri wa Maliasili na Utalii katika Serikali ya Awamu ya Nne, alisema anaamini kwamba, bila Tanzania kupata katiba mpya sasa, hakuna namna yoyote ya kuifanya mihimili ya dola isiingiliane na kuwapo kwa ukomo wa wazi.
Alipoulizwa kuhusiana na barua ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kwenda Tume ya Uchaguzi akiitaarifu kwamba Jimbo la Nyalandu lipo wazi baada ya kufutwa uanachama na CCM Oktoba 30, siku ambayo Nyalandu alitangaza kujiondoa ndani ya chama hicho, kwamba haoni jambo hilo liliwalenga watu ambao wamekuwa wakisemasema kama yeye Nape?
Akijibu hilo, Nape alisema ingawa yeye si msemaji wa CCM, lakini chama hicho kinao utaratibu wa kuwafuta uanachama wanachama wake.
“Kama lipo tatizo CCM inao utaratibu wa vikao kabla ya kuwafuta uanachama, hiyo barua ya spika sijaiona, lakini ninachofahamu mimi kama CCM inaona kuna mwanachama anakwenda kinyume itamuita, mimi sijawahi kuitwa, nimekaa kwa miaka 16 sasa najua lipi baya lipi jema,” alisema Nape.
Jana Spika wa Bunge, Ndugai, alimwandikia Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Semistocles Kaijage, kumtaarifu kuwa Jimbo la Singida Kaskazini liko wazi, baada ya aliyekuwa mbunge wake tangu mwaka 2000, Nyalandu, kufutwa uanachama na CCM.
Taarifa iliyotolewa jana na Kitengo cha Habari, Elimu kwa Umma na Mawasiliano cha Ofisi ya Bunge, ilisema Spika Ndugai aliandika barua hiyo kwa mujibu wa kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Taifa ya Chaguzi (Sura ya 343, ya mwaka 2015).
Taarifa hiyo ilielezea kifungu hicho kwamba, pale ambapo mbunge atajiuzulu, atakufa au sababu nyingine yoyote tofauti na zilizoainishwa katika kifungu cha 113, Spika atamjulisha Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kutangaza kwenye Gazeti la Serikali kwamba kiti hicho cha ubunge kiko wazi.
“Kufuatia barua hiyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaweza kuendelea na mchakato wa kumpata mbunge wa kujaza nafasi hiyo iliyo wazi ya Jimbo la Singida Kaskazini,” ilieleza taarifa hiyo.

No comments:

Post a Comment