Saturday, November 4

TAASISI YA MIKOPO YAJITETEA KUHUSISHWA NA UTAPELI


SHIRIKA lisilokuwa la kiserikali la Tanzania Social Support Foundation (TSSF) linalojihusisha na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, limetolea ufafanuzi taarifa zinazoenea kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa shirika hilo ni la kitapeli na halijasajiliwa.
Akitoa ufafanuzi, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Donati Salla, alisema taarifa hizo zinalenga kuichafua TSSF na huenda zinatolewa na washindani wao ambao wamekuwa wakitoza riba kubwa kwa wanufaika wa mikopo hiyo kutoka kwenye taasisi zao.
Alisema TSSF imesajiliwa kwa mujibu wa sheria na imekuwapo nchini tangu mwaka 2011, na limekuwa likijihusisha na shughuli mbalimbali ikiwamo za bima ya afya na maendeleo ya elimu.
Ujumbe unaosambaa kuwa tunataka kuwatapeli wanafunzi wa elimu ya juu  si wa kweli, kwa sababu haujatolewa na Serikali wala shirika lenyewe na isitoshe sisi si kampuni kama walivyoeleza, sisi ni shirika na tumesajiliwa kisheria.
“Kabla ya kufikia uamuzi wa kutoa mikopo hiyo tulifanya utafiti na kubaini kuwa kuna idadi kubwa ya watu wenye uhitaji wa mikopo, lakini wanakosa fursa hiyo.
“Tulifanya semina kwa Serikali za wanafunzi na tulitoa taarifa katika taasisi za elimu zinazodahili kwa ngazi ya shahada,” alisema Salla.
Alisema katika mchakato wao walitumia njia zinazokubalika kisheria kutoa taarifa kwa umma, ambapo walitoa matangazo katika magazeti mbalimbali likiwamo MTANZANIA.
Alisema kabla ya kutoa matangazo hayo taarifa zao zilichapishwa katika magazeti mbalimbali nchini, zikieleza kuwa wanafunzi 50,000 walikosa mikopo kutoka katika Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu, wataweza kunufaika na mikopo kutoka katika shirika hilo.
“Tunaelewa kuna watu ambao tayari walikuwa wameomba mikopo na hawajapata, huenda taarifa hii inaweza kuwa imewasababishia ‘shock’, tunaomba waendelee kuwa watulivu na waendelee kuomba.
Kazi yetu si kukaa na kusema Serikali imeshindwa au kulaani, bali ni kuisaidia pale inapokuwa haina uwezo wa kutoa mikopo hiyo, maendeleo tunaweza kuyapata kwa kuungana pamoja, tukiendelea hivi hatutafika mbali,” alisema.
Alishangazwa kuona watu wanaamini taarifa zilizotolewa na vyanzo visivyo rasmi, huku zile zilizotolewa katika mfumo rasmi zikipotoshwa na kupuuzwa.
Alionya kuwa atakayebainika kulichafua shirika hilo atachukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani ili iwe fundisho kwa watu wengine wanaotumia mitandao vibaya.
Alisema hadi sasa jumla ya wanafunzi 256 walijitokeza kuomba mikopo katika taasisi hiyo na 198 kati ya hao wamepata mipopo hiyo.
Wakati huo huo, Salla alisema Novemba 30 mwaka huu, watakutana na makamu wakuu wa taasisi za elimu ya juu nchini kujadili namna ya kutekeleza mpango huo wa udhamini kwa wanafunzi waliokosa mikopo kutoka HESLB.

No comments:

Post a Comment