Wednesday, October 4

Wananchi Catalonia wasubiri uhuru wao



Kiongozi wa eneo hilo Carles Puigdemont

Kiongozi wa eneo hilo Carles Puigdemont 
Barcelona, Catalonia. Mustakbali wa eneo la Catalonia lililoamua kujitenga baada ya kupiga kura ya maoni Jumapili itajulikana siku chache zijazo, kiongozi wa eneo hilo ameviambia vyombo vya habari.
Kiongozi wa eneo hilo Carles Puigdemont aliyefanya mahojiano kwa mara ya kwanza na shirika la BBC juzi amesema serikali yake itachukua hatua mwishoni mwa wiki hii au mwanzoni mwa wiki ijayo.
“Tutachukua hatua mwishoni mwa wiki hii au mwanzoni mwa wiki ijayo,” alisema Puigdemont. “Ikiwa serikali ya Hispania itajaribu kuingilia kati litakuwa kosa kubwa ambalo litabadili kila kitu ".
Katika maandamano ya Jumanne watu wapatao 300,000 waliandamana katika mitaa ya jiji la Barcelona kupinga ukatili uliofanywa na polisi Jumapili eneo hilo lilipoitisha kura ya maoni. Klabu ya soka ya Barcelona FC pia ilishiriki maandamano hayo na kwamba klabu zote za eneo hilo zilizusia mazoezi.
Kampuni ya kutengeneza magari ya SEAT ilisitisha uzalishaji. Kaskazini mwa Barcelona, matrekta yalipangwa barabarani kuwazuia askari wa barabarani huku wakiimba “Uhuru” na “Mitaa yote itakuwa yetu”.
Makundi ya wafanyakazi wa zimamoto walitembea mitaani wakipiga filimbi zilizofungwa katika puto huku wakishangiliwa na watu.
Maeneo mengi ya vivutio vya utalii kama makumbusho na ubunifu na makanisa yalifungwa.
Mfalme wa Uhispnia Felipe VI, amewalalamikia waandaaji wa kura ya maoni akisema walikiuka sheria. Amesema hali ya sasa nchini Hispania si nzuri na ametaka uwepo umoja.
Maandamano hayo yaliitishwa na vyama vya wafanyakazi kupinga matumizi makubwa ya nguvu yaliyosababisha ghasa polisi walipokuwa wakizuia kura ya maoni. Takriban watu 900 wakiwemo polisi 33 walijeruhwia.
Hatua ya Catalonia imewapa nguvu viongozi wa maeneo ya Quebec (Canada) na Scotland (Uingereza) ambao wanaendelea na vuguvugu la kujitenga. Kiongozi wa shirikisho la Quebec, Martine Ouellet yuko Barcelona kuwatia nguvu wenzao wasirudi nyuma.
Kwa nini Catalonia
Catalonia ndiyo eneo tajiri zaidi na lina lugha yake, utamaduni na vyama vya siasa ambavyo vinaendesha harakati za kujitenga vimejichimbia mizizi kwa miaka ya hivi karibuni. Vyama hivyo vinavyounga mkono uhuru vinadhibiti serikali ya eneo hilo na ndivyo viliandaa kura ya maoni vikikaidi mahakama zilizotangaza kura hiyo kuwa ni batili.

No comments:

Post a Comment