Wednesday, October 4

Aliyesimamishwa kazi kwa uzembe akutwa na vyeti feki


Mmoja wa wauguzi wanne waliosimamishwa kazi kwa tuhuma za uzembe uliosababisha kifo cha mtoto mchanga katika Hospitali ya Wilaya ya Kongwa, amekumbwa na sakata la vyeti feki wakati taratibu za kushughulikia kosa lao zikiendelea.
Wauguzi hao walisimamishwa kazi baada ya kamati iliyoundwa na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deogratius Ndejembi kuchunguza malalamiko ya kifo cha mtoto mchanga Juni 29, kugundua kuwa kulikuwa na uzembe katika uangalizi wa mjamzito mara baada ya kupewa dawa ya kuongeza uchungu.
Waliosimamishwa kazi kwa kosa hilo ni Mariam Mhando, Happy Limelela, Maria Costa na aliyekuwa msimamizi mkuu wa wauguzi hao siku ya tukio, Edna Rodgers.
Kwa mujibu wa agizo la Rais John Magufuli la kuondolewa kwenye utumishi wa umma kwa kosa la kughushi vyeti kwa watumishi 9,932, muuguzi huyo atakuwa miongoni mwa watu waliopoteza ajira yake.
Akizungumza jana, Ndejembi alisema kwamba mmoja wa wauguzi hao alikutwa na vyeti feki katika ukaguzi uliofanywa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
“Waligundua (wajumbe wa kamati) kwamba kweli matatizo yalikuwapo na uzembe ulifanyika kwa wao kutokuwa makini katika kazi yao, sasa ni mwezi tangu libainike hilo. Lakini mmoja amekutwa na janga la vyeti feki kati ya wauguzi wanne walioshikwa na vyeti feki,” alisema.
Mkuu huyo wa wilaya alisema utaratibu wote ulifuatwa kwa yeye kuunda kamati ya kuchunguza tukio hilo na kisha kutoa ripoti ya kubaini uzembe.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Ngusa Izengo alisema kuwa wauguzi hao wamesimamishwa kazi na kwamba taratibu nyingine za kiutumishi zinaendelea kufanyika.
“Kwa mujibu wa taratibu za ajira serikalini, iwapo mtumishi anatuhumiwa inabidi asimamishwe, kisha umuombe maelezo halafu ndio uamue hatua ya kuchukua,” alisema.
Alisema ingawa yeye kama mwajiri ameshachukua hatua ya kuwasimamisha, lakini watumishi hao wana bodi yao ya kitaaluma ambayo pia inashughulika na masuala yao.
Kamati hiyo iliundwa na Ndejembi kuchunguza sakata la madai ya wauguzi hao kusababisha kifo cha mtoto mchanga baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya watu wilayani humo.
Miongoni mwa hadidu za rejea ilizopewa kamati hiyo na mkuu huyo wa wilaya ilikuwa ni kuchunguza pia madhara ya kiafya kwa mama wa kichanga hicho baada ya tukio hilo.
Akisoma ripoti ya uchunguzi, Katibu wa kamati hiyo, Celina Fundi alisema wamebaini kuwa wauguzi hao walihusika kwa namna moja kufanya uzembe kwa kutompa uangalizi mjamzito huyo baada ya kumpa dawa ya kuongeza uchungu.     

No comments:

Post a Comment