Wednesday, October 4

DED aagizwa kudhibiti ombaomba


Katibu Tawala wa Wilaya ya Nyamagana, Yonas Alfred amemuagiza Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba kuwadhibiti ombaomba wanaotupa vinyesi hali inayotishia usalama wa afya za wakazi.
Akizungumza mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa utekelezaji agizo la Rais John Magufuli la kila mwisho wa mwezi kufanya usafi, Alfred alisema ombaomba hao ni wachache lakini wanaongoza kwa kuchafua mazingira.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Hosiana Kusiga alisema wamekamilisha taratibu zote za kuanzisha vikundi vya vijana kwa jina maarufu la Sharifu watakaokuwa wanazunguka mitaani kuwadhibiti wanaochafua mazingira, kazi itakayokwenda sambamba na kutozwa faini ya Sh50,000 kwa atakayebainika kulingana na sheria ndogo za halmashauri.
“Tunatafuta dawa za kuwadhibiti wanaotupa taka ovyo, kwa kuwa hata tukiweka vyoo hawavitumii hivyo tunaamini vikundi hivyo vitakavyoanza kazi ndani ya mwezi mmoja, vitasaidia kudhibiti hali hiyo,” alisema Hosiana.
Baadhi ya wakazi jijini Mwanza, walisema huenda zoezi hilo likasaidia kutunza mazingira kwa sababu kwa sasa kila kona inatoa hewa ukaa.
“Huenda vikundi hivyo vikasaidia kudhibiti ombaomba hao na wakapungua mjini, kwa sababu ndiyo wanaoongoza kwa kutupa uchafu sehemu mbalimbali,” alisema Martha Mlole.
Pia, mkazi mwingine wa Mtaa wa Uhuru, James Stia aliiomba halmashauri hiyo kuhakikisha wanadhibiti Wamachinga wanaopanga bidhaa zao kandokando mwa barabara kwa kuwa wanaondoa hadhi ya jiji na ndiyo chanzo cha uchafuzi mazingira.
Naye mfanyabiashara wa Soko la Kamanga jijini hapa, John John alisema hawezi kutupa takataka hizo kwa sababu wameshaandaa mapipa ya uchafu.     

No comments:

Post a Comment