Wednesday, October 4

Besigye asema mtuhumiwa wa kwanza serikali

 

Kampala, Uganda. Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Dk Kizza Besigye ameituhumu serikali ya Uganda kuwa ndiyo iko nyuma ya mashambulizi ya magruneti yaliyofanywa wiki iliyopita kwenye nyumba za wabunge wa ypinzani.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, mashambulizi hayo yamefanywa na serikali kwa lengo la kuwatisha wabunge hao wa upinzani na kuwatia hofu wananchi wanaopinga mpango uliopo wa kufuta ukomo wa umri wa rais.
“Hii ni hatua iliyochukuliwa na serikali ya Rais Yoweri Museveni kuwatisha wabunge na jamii nzima ogope kushiriki kampeni za kupinga kuondoa ukomo wa umri wa rais. Hata hivyo, hili lisiwatishe,” amesema Besigye.
Matamshi ya Dk Besigye yamekuja wakati huu ambao polisi wamesema kuwa wanafanya uchunguzi mazingira ambapo nyumba za wabunge wawili wa upinzani zilishambuliwa kwa magruneti alfajiri ya Jumanne iliyopita siku chache tu baada ya mbunge mwingine wa upinzani kunusurika katika shambulio kama hilo.
Nyumba zilizoshambuliwa ni za Allan Ssewanyana (Makindye Magharibi) na Robert Kyagulanyi (Kyaddondo Mashariki). Watu wasiojulikana walirusha magruneti kwenye nyumba zao.
Wiki iliyopita, magruneti mawili yalirushwa na kulipuka pia alfajiri katika nyumba ya Mbunge wa Rubaga Kaskazini Moses Kasibante. Wakati wa shambulio hilo mbunge huyo alikuwa anashikiliwa na polisi katika kituo cha Kibuli baada ya kubanduliwa kutoka bungeni na polisi walioshirikiana na wanajeshi baada ya kuibuka zogo kuhusu ukomo wa umri wa rais.
Hata hivyo, msemaji wa serikali, Ofwono Opondo aliwageuzia kibao wanasiasa wapinzani akisema kuwa ni mbinu zao za kuichafua serikali.
“Magruneti yaliyorushwa kwenye nyumba za wapinzani zinaweza kuwa mbinu zao za kuichafua serikali. Hakuna rekodi wala historia ya serikali ya chama cha NRM kuua mwanasiasa wa upinzani,” amesema Opondo.

No comments:

Post a Comment