Monday, October 23

Wahadhiri Aga Khan wanolewa


Ugaidi na umaskini chanzo chakeWahadhiri na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Aga Khan nchini, wamenolewa namna ya kuisaidia jamii inayokosa haki ya kupata elimu kutokana na vikundi vya kigaidi, umaskini na vitendea kazi.
Mafunzo hayo yaliyotolewa juzi na Mtaalamu wa Historia ya Ulimwengu na Masomo ya Afrika kutoka Chuo cha New Hampshire Marekani, Profesa Funso Afolayah alisema nchi nyingi za Afrika zinakosa elimu kutokana na matukio mbalimbali ikiwamo kujiunga na vikundi vya kigaidi.
Profesa Funso alisema wanafunzi walitekwa nyara na kikundi cha Boko Haramu mwaka 2014 na kuwasababishia kukosa haki ya kupata elimu ambayo ingewasaidia kupiga vita umaskini.
“Wasichana katika baadhi ya maeneo ambako kikundi hicho kinatekeleza utekaji nyara hawaruhusiwi kusoma na shule zao zikichomwa na kupigwa mabomu jambo ambalo ni hatari kama hakutakuwa na mikakati ya kuzuia hali hiyo,”alisema.
Alisema katika kuhakikisha jamii za kiafrika zinapata haki zao ikiwamo elimu, walimu na wadau wanatakiwa kujifunza namna ya kuwaeleza umuhimu wa elimu na kupiga vita vitendo vya uvunjifu wa amani.
Naye Mkuu wa Chuo cha Aga Khan (Aku), Profesa Joe Lugalla alisema mafunzo waliyoyapata yatachagiza ufanisi kwa walimu watarajiwa kuishi katika mazingira halisi kwa kuona mfano ambao mtaalamu ameuonyeesha nchini Nigeria. Alisema vijana wengi wanashindwa kushindana katika ajira na wengine kukosa masomo kutokana na mazingira mabovu ya utolewaji elimu.
“Mazingira siyo rafiki ndiyo maana vijana wanajihusisha na ujambazi na dawa za kulevya, hivyo kupitia mafunzo haya wanafunzi watapatiwa maarifa ya kujikinga na matatizo hayo,” alisema.

No comments:

Post a Comment