Ndivyo ilivyokuwa kwa baadhi ya wakazi wa maeneo yaliyo kati ya Kimara na Kiluvya jijini Dar es Salaam ambao nyumba zao za ibada zilizokuwa ndani ya mita 121.5 kutoka katikati ya Barabara ya Morogoro, zimebomolewa kupisha upanuzi wa barabara hiyo.
Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) ulianza kubomoa nyumba na majengo eneo hilo Juni 18 kwa ajili ya kujenga barabara ya njia sita, tatu kila upande ili kuruhusu magari kuingia jijini Dar es Salaam bila ya msongamano.
Barabara hiyo ndiyo inayotumiwa na magari mengi, hasa yatokayo mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Mikoa ya Kanda ya Kati na kutoka Kanda ya Kaskazini.
Kwa mujibu wa Tanroads, takriban nyumba 1,300 za wananchi wa maeneo hayo zilizojengwa ndani ya mita 121.5 kutoka katikati ya barabara hiyo kwa kila upande zitabomolewa na tayari 1,000 zimebomolewa zikiwemo nyumba za ibada.
Ubomoaji huo utazikumba nyumba 24 za ibada, ikiwa ni misikiti 10 na makanisa 14.
Mwandishi wa gazeti hili aliyetembelea eneo hilo jana alishuhudia waumini wakiendelea na ibada chini ya miti na kwenye magofu.
Licha ya kuwepo manyunyu, waumini wa Kanisa la Assemblies Of God (TAG) lililopo Mbezi Inn waliendesha ibada kwenye mabaki ya jengo lao la ibada lililobomolewa. Waumini hao waliondoa mabati na kubakiza machache kwa ajili ya kuikinga madhabahu na vifaa vya muziki.
Hali ya mvua iliwalazimu waumini hao kujibanza kwenye kuta za jengo hilo lisilo na paa na baadhi yao kukaa karibu na madhabahu ili kujikinga wasilowane.
Akizungumza na waandishi wa Mwananchi mbele ya waumini, Mchungaji Godwin Mushi alisema wanamshukuru Mungu na hawana kinyongo na viongozi wa nchi bali wanawapenda na wanazidi kuwaombea.
“Tunaabudu katika mazingira magumu, mvua na jua ni letu, lakini pamoja na hayo tumepata kiwanja jirani na kanisa letu. Tunadaiwa zaidi ya Sh50 milioni ili kukilipia tuanze ujenzi,” alisema.
“Tunaomba wasamaria wema watusaidie. Tunahitaji fedha hizo haraka ili tulipie kiwanja. Kwa sasa hatuna mahali pengine pa kuabudia ndiyo maana tunasalia hapa, japo si salama sana.”
Alisema wanapenda maendeleo ndiyo maana wametii agizo la kubomoa nyumba yao ya ibada.
“Furaha yetu ni kuona nchi ikiwa na maendeleo,” alisema.
Mbali na waumini hao, wenzao wa Kanisa la Calvary Assemblies of God (CAG) lililopo Kimara Suka, walisali chini ya miti baada ya jengo lao la ibada kuvunjwa takriban wiki mbili zilizopita.
Walichofanya ni kuzungusha uzio wa vitambaa.
Mchungaji kiongozi wa kanisa hilo, Fredy John alisema kwa sasa hawajui mwelekeo wao kwa kuwa mahudhurio ya waumini yamepungua.
“Tuna hali mbaya. Sijui hata nisemeje. Waumini wamekimbia. Tulikuwa na waumini wengi zaidi ya mia moja lakini kwa sasa tunasali hata kumi hatufiki,” alisema.
“Hapa mvua ikinyesha tunaacha kusali tunasubiri ikiisha ndiyo tunaendelea na sala. Kama unavyoona hakuna paa, hakuna chochote ni chini ya miti tu.”
Baada ya Tanroads kubomoa Kanisa la Mlima wa Moto lililokuwa Kimara Mwisho, waumini sasa wanasali katika jengo la shule moja ya binafsi iliyopo eneo la Ubungo.
Neema Mussa, muumini wa kanisa hilo, aliiambia Mwananchi kuwa awali walikuwa wanasali katika ukumbi wa sherehe, lakini mwenzao anayemiliki shule aliwapa darasa ambalo wanalitumia kwa sasa.
Hata hivyo, Neema alisema hivi sasa amehama kanisa hilo kutokana na kuwa mbali, hivyo anasali Kimara.
Waumini wa Usharika wa Mbezi Louis wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na Parokia ya Mtakatifu Maria ya Kanisa Katoliki Kimara wameendelea na ibada kwenye majengo ya makanisa hayo ambayo yanatakiwa kubomolewa.
Awali, msimamizi wa kazi ya bomoabomoa kutoka Tanroads, Mhandisi Johnson Rutechula alilieleza gazeti hili Oktoba 15 kuwa wangebomoa nyumba 24 za ibada Oktoba 16.
Hata hivyo, kazi hiyo haikufanyika akisema wameongeza muda wa siku tatu kwa wananchi ili wabomoe wenyewe, lakini hadi jana majengo hayo hayakuwa yamebomolewa.
No comments:
Post a Comment