Monday, October 23

UVCCM kuwamulika wanaobeza juhudi za Rais Magufuli


Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge, Sera, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu), Antony Mavunde amesema vijana wa CCM hawatakaa kimya kuona baadhi ya Watanzania wakibeza juhudi zinazofanywa na Rais John Magufuli za kupigania rasilimali za nchi.
Mavunde alisema hayo jana katika mkutano wa vijana wazalendo kutoka mikoa mbalimbali.
“Wapo Watanzania wanaobeza na kukejeli kazi ya Rais. Hatupo tayari kukaa kimya kuona baadhi ya watu wachache wanaokebehi kama vijana tusikae nyuma tukemee, tumuombee Rais wetu mungu amjalie hekima, uvumilivu na ujasiri,” alisema Mavunde.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana aliwataka wawabeze na kuwapuuza watu ambao wamekuwa wakipinga jitihada za Rais Magufuli.
Alisema tangu Rais aingie madarakani amefanya mambo mengi ambayo Watanzania wanatakiwa kujivunia.
Akisoma tamko kwa niaba ya vijana hao, Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Shaka Hamdu Shaka alisema wamelazimika kukutana mkoani Dodoma kwa lengo maalumu lenye kujali masilahi mapana ya nchi.
“Lengo letu la hafla hii fupi ya uzalendo ni kupongeza ujasiri na uthubutu ulioonyeshwa na Rais wetu kwa jinsi anavyobeba dhima na jukumu la kupigania masilahi ya Taifa ili kupata maendeleo ya pamoja kwa watu wote,” alisema. Alifafanua kuwa vijana wameridhishwa na juhudi za Serikali katika kudhibiti vitendo vya wizi wa mali za umma ambavyo vilikuwa vikifanywa hapo awali.
“Vijana tunaipa mkono wa heko Serikali kwa kuanzisha mazungumzo na wawekezaji wa Barrick Gold Mine na kufikia uamuzi ya haki na usawa katika mgao wa faida utokanao na mapato ya madini yaani asilimia 50 kwa 50,” alisema Shaka.
Katika hatua nyingine, Jumuiya ya Wanawake wa CCM (UWT) imempongeza Rais kwa jitihada zake za kulinda rasilimali na kufanikisha Tanzania kupata gawio la nusu kwa nusu kwenye madini. Katibu Mkuu wa UWT, Amina Makilagi alisema hakuna sababu ya UWT kubaki nyuma na wanapaswa kumwombea Rais kwa sababu kazi anayofanya ni kubwa na inastahili kuigwa.
Alisema kila mwanamke anapaswa kushiriki katika maombi ya Rais huyo kutokana na kile anachokifanya.

No comments:

Post a Comment