Wengi wetu tunaishi katika mazingira ambayo yanaathiri amani yetu ya moyoni. Yamkini tunaonekana tuna furaha, tunacheka tunahusiana vyema na wanaotuzunguka lakini ukweli ni kwamba ndani yetu hatuko sawa. Wengi tunawaona wana maisha mazuri kwa jinsi ya nje, wana majumba mazuri ya kuishi, magari ya kutembelea, watoto wazuri na kazi nzuri. Pia, tukiwaangalia tunadhani wana furaha ndani yao lakini nimepata bahati ya kuzungumza na wengi wa aina hii na kugundua kuwa hawakuwa na furaha ya maisha yao kama wengine walivyofikiri. Viko vitu vingi vinavyoweza kuiathiri amani ya moyoni mwako, kwa mfano; hali mbaya ya mahusiano baina yako na umpendae, matatizo ya tabia za watoto wako, matatizo ya kazini kwako, kushindwa kufikia malengo binafsi, historia yako binafsi, maumivu ya moyo, mambo ya ndugu na mengine mengi
Dhumuni langu katika makala hii ni kujaribu kuzibua kanuni chache za kusaidia kuishulikia hali hii ili uweze kupona katika tatizo hili.
Jitahidi kutokuingilia mambo ya wengine, labda tu uruhusiwe na mhusika
Wengi tumejikuta katika matatizo sababu tu ya kuingilia mambo yasiyokuwa yetu, tunafanya hivyo sababu mara nyingine tunafikiri tunavyojua sisi ndio sawa, na mtazamo wetu ndio uko sahihi zaidi, na yeyote asiyeafikiana na mtazamo wetu anastahili kupingwa. Lazima tutambue kwamba Mungu amemuumba kila mmoja wetu tofauti. Hakuna watu wawili watakaowaza au kutenda sawa sawa. Jali yaliyo yako kwanza na utailinda amani ya moyo wako.
Jifunze kusamehe na kusahau
Hii ni nguzo na msaada mkubwa katika kutafuta amani ya moyoni. Mara nyingi tunaweka hisia za maumivu moyoni dhidi ya mtu aliyetuumiza au kutuudhi, taratibu tunaumba na kulea chuki kali moyoni. Matokeo yake wengine wanakosa usingizi, wanapata vidonda vya tumbo, wengine shinikizo la damu (BP) n.k. Chuki au maumivu haya ya moyo yalifanywa mara moja, lakini matokeo yake yanaeendelea kuharibu maisha na afya kwa muda mrefu kwa sababu tu ya wewe kuikumbuka chuki au uchungu. Achana na tabia hii mbaya. Maisha ni mafupi sana hustahili kuyaweka katika matatizo yote haya. Samehe, sahau na tembea mbele. Upendo wakati wote huchanua katika tendo la kutoa na kusamehe (love flourishes in giving and forgiving )
Kamwe usijitutumue kutafuta umaarufu, kujulikana au kutambulika
Fahamu kuwa ulimwengu huu una wabinafsi wengi sana, mara chache watakusifia pasipo kuwa na wivu. Wanaweza kukusifia leo kwa sababu unanafasi au uwezo fulani, lakini subiri utakaposhuka chini. Watasahau kabisa yote mema uliyofanya na kuanza kutafuta kila chafu na ovu ulilotenda, hata kama lilitendeka mafichoni. Kwa nini unataka kujiua ukitafuta kutambulika na kukubalika. Kwamwe kukubali kwao hakulingani na kero zao. Kero zao zinazidi sana. Jitahidi kufanya majukumu yako kwa nidhamu ya hali ya juu na moyo wote, ukimwogopa na kumheshimu Mungu na sio mwanadamu.
Usiwe na wivu
Wote tunajua jinsi wivu unavyoweza kusumbua amani yetu ya moyoni. Unajua kabisa kuwa unafanyakazi zaidi ya wenzako ofisini lakini wao wanapata kupandishwa cheo au faida zingine za kikazi na sio wewe.
Wewe umeanza biashara miaka mingi iliyopita, lakini haujafanikiwa kama jirani yako ambaye ana mwaka tu katika biashara. Iko mifano tele kama hii katika maisha ya kila siku. Je ndio inakufanya uwe na wivu? Hapana, kumbuka kuwa kila maisha ya mtu hutegemezwa na mustakabali wake utakavyokuwa, ambao ndivyo unavyompeleka yeye hivyo alivyo. Kama umepangiwa kufikia hatua fulani hakuna atakayeweza kusimamisha. Kama hujapangiwa hivyo, hakuna atakayeweza kukusaidia kufikia pale pasipo pako. Hakuna utakachokipata kwa kulaumu wengine kwa bahati zako mbaya. Wivu hautokupeleka kokote, zaidi utakuondolea amani moyoni mwako.
Jifunze kubadilika kutokana na mazingira
Kama unadhani utaweza kushindana na mazingira na kuyabadilisha, kuna uwezekano mkubwa kuwa utafeli. Badala yake jifunze kubadilika wewe kwanza ili kuendana na mazingira yanayokuzunguka, ambayo unadhani yako kinyume na matakwa yako. Kwa kufanya hivi hata mazingira yaliyoonekana kuwa magumu taratibu yatabadilika na kuwa ya kuridhisha.
Jitahidi kustahimili vile visivyoweza kubadilika
Hii ni njia bora yakugeuza bahati mbaya kuwa bahati nzuri. Kila siku tunakutana na matatizo, balaa, magonjwa, hofu na hata ajali ambazo ni zaidi ya uwezo wetu. Kama hatuwezi kufanya chochote dhidi ya mambo haya magumu wala hatuwezi kuyabadilisha basi ni vema tujifunze kustahimili, kukubali na kuchukuliana na hali tukiwa bado wenye tumaini. Jiamini wakati wote unapoyapitia haya na utaona mbegu ya ujasiri na uvumilivu inaota ndani yako na taratibu nguvu ya kuendelea mbele itaibuka.
No comments:
Post a Comment