Tuesday, October 10

Uhaba wa maji unavyoathiri mipango ya maendeleo Nanyumbu


Saa nne asubuhi nipo njiani kutoka mji mdogo wa Mangaka ambao ni makao makuu ya Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara, naenda katika Kijiji cha Mnunia Kata ya Kilimanihewa.
Hapa pana umbali wa takriban kilomita tano. Kwa kuwa nimeamua kutumia usafiri wa pikipiki basi ni mwendo wa dakika 15 tu.
Njiani nakutana na watu wengi; wanawake kwa wanaume, wazee kwa vijana na hata watoto wakiwamo wanafunzi waliovalia sare za shule. Wengi wamebeba ndoo na madumu ya maji.
Baadhi yao wameshikilia fito ndefu ambazo katika moja ya ncha zake zimefungwa bakuli. Baada ya kuuliza naambiwa fito hizo na bakuli zake zinaitwa ‘mkonji’ kwa lugha ya Kimakua. Hutumika kuchotea maji katika visima virefu.
Baadhi ya wananchi hao wameshapata maji huku wengine wakielekea kusaka huduma hiyo. Wengine wanatembea kwa miguu lakini pia wapo wanaotumia baiskeli au pikipiki. Misafara hii hufanywa kila siku na wakazi wa eneo hili kutokana na uhaba mkubwa wa maji.
Baada ya kufika Mnunia, wenyeji wangu wanaanza kunitembeza katika visima vya maji vya kijijini hapo ambavyo huchota maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali hususan kunywa, kufulia na kupikia.
Kutoka katika makazi yao kwenda kwenye kisima kimoja ambacho ni cha kuchimba na jembe la mkono ni mwendo wa dakika 40 hivi na barabara imejaa mashimo na nyasi zake ni ndefu.
Kutoka katika kisima hicho kwenda kisima kingine ni mwendo huo huo isipokuwa bwawa lililokuwa umbali wa mwendo wa dakika 15 kwa usafiri wa pikipiki.
Pembezoni mwa visima hivi na bwawa, wapo watu wa rika tofauti. Wengine wanafua nguo, wapo wanaochota maji na wengine wanasogea vichakani kwa ajili ya kuoga. Hata hivyo maji ya visima na bwawa hili si salama.
Mwonekano wake ni wa rangi ya udongo, isipokuwa yale yanayotoka katika kisima kimoja ambacho maji yake ni ya kusubiri kwani yanatoka taratibu sana.
Zuedi Akida mkazi wa Mnunia anasema ikiwa unataka kupata maji katika kisima cha chemchemi lazima ujihimu saa 10 alfajiri na bado uhakika wa kupata maji ni mdogo.
“Haya maji kama unavyoyaona, ukipikia ugali hupati ladha halisi ya chakula, hata ukichemshia mbaazi haziivi vizuri, kwa kweli ni shida tu. Tunayatumia tu lakini siyo safi na salama,”anasisitiza.
Hata hivyo, wanakijiji wanapata shida ya maji licha ya kifungu cha 4.4 cha Sera ya Maji ya Mwaka 2002 kuweka malengo ya kuwezesha upatikanaji maji vijijini katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi ya watu. Pia, sera hiyo inataka kituo kimoja cha maji kiweze kuhudumia watu 250 kwa kiwango cha kila mtu apate lita 25 kwa siku.
Mhandisi wa maji wa Mkoa wa Mtwara, Rejea Ng’ondya anasema ni theluthi moja tu ya wakazi wa Wilaya ya Nanyumbu wanaopata huduma za maji sawa na asilimia 34.8 tu.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) hadi kufikia mwaka 2016 wilaya hiyo inakadiriwa kuwa na wakazi wapatao 107,117.
Biashara taabani
Miongoni mwa shughuli zinazoathiriwa na uhaba wa maji ni biashara, ujasiriamali na ujenzi wa miundombinu ya huduma za kijamii.
Amina Kassimu ambaye hujishughulisha na biashara ya mama lishe, anasema kabla ya kufungua biashara yake hulazimika kutumia saa mbili hadi tatu kwenda kutafuta maji kwa ajili ya familia.
Mama huyo wa watoto wanne anasema licha ya kuamka saa 10 alfajiri kila siku, hana muda rasmi wa kufungua biashara yake kutokana na kutokujua muda wa upatikanaji wa maji hivyo kuna wakati anafungua saa 2 asubuhi hadi saa 3 asubuhi baada ya kutoka kutafuta maji.
“Ninapoamka saa 10 ningeweza kuanza kuandaa biashara yangu na ikifika saa moja wateja wakapata chai na vitafunwa, lakini napoamka lazima nitumie saa tatu hadi nne kutafuta maji…kutoka hapo mpaka nirudi kufungua biashara nakuwa tayari muda ushanitupa mkono,” anasema na kuongeza:
“Hapo fedha ya chai nakuwa nimeshaikosa.”
Anaamini kama si tatizo la maji angepata kipato zaidi tofauti na kiwango cha sasa ambacho ni kati ya Sh11,000 na Sh15,000 kwa siku.
Hata hivyo, wengine kama Amina Baraka, anayefanya biashara ya viungo vya chakula, hulazimika kutumia sehemu ya faida zao na wakati mwingine mtaji ili kununua maji kwa ajili ya familia ili wawahi kufungua biashara zao.
“Maji yanapatikana mbali kwa hiyo nikifikiria niende kuyatafuta mwenyewe nakuwa nachelewa kufungua biashara kwa sababu lazima pia niandae watoto waende shule hivyo ni bora ninunue Sh3,000 ambayo huwa ni faida na wakati mwingine ni mtaji,”anasema na kuongeza:
“Asubuhi nikiamka nawaandaa watoto wanakwenda shule na mimi nakuja kufungua biashara yangu mapema kwasababu mama lishe wengi wanakuwa wanahitaji vitu kwa ajili ya kupikia.”
Uhaba wa maji hauwaathiri tu wafanyabiashara za rejareja, bali hata wale wanaofanya shughuli za ujenzi kama Said Khamis ambaye ni fundi ujenzi wa nyumba katika Kijiji cha Michiga.
“Unaweza kupewa kazi ya ujenzi na mwenye kazi mkafanya usanifu kila kitu, mkafahamu ni vitu gani vinahitajika na ukakabidhiwa vifaa vyote, lakini mwisho wa siku tunajikuta tunakwama kwenye ufyatuaji wa tofali kwa sababu ni vigumu kupata maji hasa kiangazi,”anasema Khamis.
Anasema huwa wanawashauri waajiri wao kabla ya kuanza ujenzi wahakikishe wanachimba visima, lakini mara nyingi hukauka hata kabla ya kuanza ujenzi rasmi jambo linaloongeza gharama za mradi husika na kumfanya fundi atumie muda mwingi kwenye nyumba moja.
Kauli ya Mkuu wa Mkoa
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendego anakiri kwamba ikiwa mtu anatumia muda mrefu kutafuta maji ni dhahiri atachelewa kufanya shuguli nyingine za uzalishaji na maendeleo, lakini akasema Serikali inalitambua hilo na kuna jitihada za utatuzi zinaendelea kufanyika.
“Upataji wa maji hasa maeneo ya vijijini tuko chini, kimkoa tuko katika asilimia 56 lakini ukienda wilaya moja moja unaweza ukakuta kuna wilaya ina asilimia 34, kwahiyo hii bado ni changamoto,”anasema Dendego.
Hata hivyo, anasema mkoa una miradi 56 inayoendelea, kati ya hiyo 28 imekamilika na kwamba miradi mingine inayoendelea itakuwa imekamilika ifikapo Desemba mwaka huu hivyo kusaidia kupunguza tatizo la maji.
Hali ya maji
Kaimu Mhandisi wa Maji Wilaya ya Nanyumbu, Frank Athakwani anasema hali ya upatikanaji maji wilayani hapo si ya kuridhisha kutokana na hali ya jiolojia.
Athakwani anasema wilaya hiyo ina visima 38 ambavyo vimechimbwa na halmashauri (17) na wafadhili (21) na kwamba kati ya hivyo 15 vinaendeshwa kwa jenereta na 23 vimewekwa pampu za mkono na kwamba baadhi ya visima havifanyi kazi kutokana na kukauka na vingine maji yake yanakuwa hayafai kwa matumizi ya binadamu na kuyazuia.
Hali hiyo inathibitishwa na diwani wa Michiga, Hasheem Nassir ambaye anasema kati ya visima 12 vilivyochimbwa na halmashauri kwenye kata yake, ni kimoja tu kinachotoa maji kwa sasa kikihudumia watu 10,886.
Nassir anasema kutokana na hali hiyo, baadhi ya wananchi wamekuwa wakitumia maji kutoka kwenye visima wanavyochimba kwa jembe la mkono kutokana na kutomudu gharama za mitambo na kuzalisha maji yasiyo salama.
Hata hivyo, Kaimu Mhandisi wa Maji halmashauri ya Nanyumbu, Athakwani anasema gharama zinategemea eneo alilopo mwombaji kwa maana ya usafiri wa kuufikisha mtambo kufika pamoja na zile za utafiti wa maji ardhini.
“Mtu anapoomba mtambo, taratibu ni mpaka wapate watafiti wa maji chini ya ardhi wajue kama maji yapo, kwa sababu maeneo mengine ni mbali, huwezi kupeleka mtambo halafu ukose maji unakuwa hujawasaidia na hivi katika wilaya yetu unaweza ukachimba kisima ukakuta maji lakini baada ya muda mfupi yanakauka,” anasema.
Utatuzi wa kero
Mhandisi wa Maji wa Mkoa wa Mtwara, Rejea Ng’ondya anasema wilaya hiyo ina changamoto ya kipekee tofauti na wilaya nyingine hivyo Wizara ya Maji iliwapa kibali cha kutumia teknolojia ya mabwawa matano ya kuvuna maji ya mvua na kwamba moja la mfano tayari limekamilika katika Kijiji cha Sengenya, hivyo watatumia teknolojia hiyo katika maeneo mengine.
Anasema kukamilika kwa mabwawa hayo ifikapo 2021 kutawezesha wananchi 37,000 wa Wilaya ya Nanayumbu kupata maji.
Mhandisi huyo anasema mpango wa muda mrefu ni kuchukua maji kutoka Mto Ruvuma kutokana na wilaya hiyo kukosa vyanzo vya uhakika vya maji na kwamba mradi huo uko katika hatua ya usanifu baada ya upembuzi yakinifu kukamilika.
Anasema mradi huo ukikamilika utahudumia wananchi wapatao 61,000 katika vijiji 29 na mji wa Mangaka.
“Kwa sasa hivi kinachoendelea kufanyika ni usanifu na baada ya kukamilika utatueleza ni miundombinu kiasi gani itajitajika na gharama zake ni kiasi gani ndipo suala la fedha linafuata,”anasema Ng’ondya na kuongeza;
“Nanyumbu tulikuwa na mradi wa Program ya Maendeleo ya sekta ya maji awamu ya kwanza (WSDP 1) na umekamilika kwa asilimia zote 100 lakini bado tatizo liko pale pale wanaopata maji ni 38.4 pekee.

No comments:

Post a Comment