Tuesday, October 10

Uhaba wa maji unavyotishia ndoa za wakazi wa Nanyumbu


Pembezoni mwa barabara kadhaa zinazoingia na kutoka katika mji mdogo wa Mangaka ambao ni makao makuu ya Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara, watu wa rika tofauti wameinama wakichota maji kwenye madimbwi na wengine kwenye visima vya kienyeji.
Baadhi waliopata maji hayo wapo pembeni wakiendelea kufua nguo zao kwa kuwa ni rahisi kufulia hapo kuliko kuyabeba maji hayo hadi nyumbani.
Madimbwi hayo wanayochota maji hujaa wakati wa mvua na huendelea kuwa na maji hadi nyakati za kiangazi.
Licha ya kwamba maji hayo rangi yake ni kama ya chai ya maziwa iliyozidiwa maji, wakazi hawa huyatumia kwa ajili ya matumizi mbalimbali majumbani mwao ikiwemo kunywa na kupikia chakula.
Baadhi ya wakazi wa Nanyumbu wanasema maisha haya wameyazoea na kwamba tatizo hilo la uhaba wa maji limesababisha migogoro mingi ikiwamo iliyosababisha kuvunjika kwa ndoa.
Sehemu kubwa ya vijiji hivi havina kabisa vyanzo vya maji safi na salama hivyo kufanya wananchi watembee umbali mrefu kuyasaka hata zaidi ya kilomita nne.
Kwa mfano, katika Kijiji cha Mnazi Mmoja katika Kata ya Michiga, visima vitano vilijengwa lakini hadi sasa kinachofanya kazi ni kimoja tu kiasi cha
INAENDELEA UK 24
INATOKA UK 23
kuwasababishia wanawake na watoto kutumia muda mwingi kusaka maji kwenye chemchemi au mabwawa yenye maji machafu.
“Akina mama na watoto ndio wanaohusika na suala nzima la kutafuta maji hivyo wanalazimika kwenda katika vijiji vingine kusaka maji,”anasema Mtendaji wa kijiji hicho, Tukae Ally.
Uhaba huo unaitafuna kata nzima ya Michiga baada ya diwani wake Hasheem Nassir kueleza kuwa kata hiyo yenye wakazi 10,886 ina visima 12 lakini ni kisima kimoja pekee hutoa maji.
Anasema pamoja na jitihada zilizofanywa na halmshauri kuna baadhi ya visima vilivyochimbwa lakini maji yake hayafai kwa matumizi ya binadamu hivyo kuzibwa.
Inadaiwa baadhi ya wanawake walioolewa huingia kwenye uhusiano na vijana wanaomiliki pikipiki na baiskeli ambao ‘huwahonga’ maji na kupunguza adha ya kutembea umbali mrefu kuisaka huduma hiyo muhimu.
Oscar, mkazi wa Kijiji cha Chipuputa katika kata hiyo ya Chipuputa, aliachana na mke wake miaka minne iliyopita kutokana na ugomvi ambao chanzo chake kikuu ni uhaba wa maji.
Anasema ndoa yake ilivunjika Februari 2013 kwa kile anachoeleza kuwa ni baada ya kugundua kuwa mkewe alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na kijana aliyekuwa akimchotea maji.
Oscar (siyo jina lake halisi) anasema mkewe alikuwa akilazimika kuamka saa 10 alfajiri kwenda kusaka maji kwenye visima vya kienyeji na alikuwa akitumia kati ya saa mbili hadi tatu na kwamba kadri siku zilivyozidi kwenda masaa ya kurudi nyumbani yalibadilika na kumpa hofu.
“Niliwahi kusikia maneno kwamba mke wangu ananisaliti, lakini sikutilia maanani ila kilichonipa wasiwasi kuna siku aliniaga majira ya saa 10:30 alfajiri kuwa anakwenda kutafuta maji lakini akarudi saa 11 asubuhi na maji yalikuwa ya chumvi tofauti na tulivyozoea hivyo akanipa maswali mengi yaliyokosa majibu ndipo nikaanza kumfuatilia,” anasema.
Anasema kilichomshangaza ni jinsi mkewe alivyoweza kupata maji katika muda wa nusu saa tu. Anasema siku iliyofuata alfajiri alimfuatilia, lakini kabla ya kufika kisimani alimpotea.
“Sikujua alipoelekea nikaamua kwenda kukaa kwenye njia ya kwenda kisimani lakini sikumwona hivyo nikaamua kurudi nyumbani, nikamkuta yuko kitandani amelala akaanza ugomvi akisema kumbe akitoka na mimi huwa natoka hakujua kwamba nilikuwa namfuatilia,”anasema.
Oscar, ambaye ameshaoa mke mwingine, anasema uchunguzi wake ulibaini kwamba mkewe alikuwa na uhusiano na kijana mwendesha pikipiki aliyokuwa akiitumia kumchotea maji na kuyahifadhi ndani kwake na pale alipomuhitaji kimapenzi alikuwa akimwita nyumbani kwake na kumpa maji baada ya kuisaliti ndoa.
Maumivu zaidi kwa wanawake
Kwa kuwa wanawake ndiyo wachotaji wakuu wa maji, athari kubwa za kijamii zinawakumba wao hasa kwa wale wenye wanaume wenye wivu kupindukia katika ndoa zao.
Zuedi Akida, mkazi wa Kijiji cha Mnunia, Kata ya Kilimanihewa anasema kuna wakati hushindwa kuhudumia ndoa zao vyema hususan wakati wa kiangazi kwa kuwa hutakiwa kwenda mbali kuyasaka maji.
“Kiangazi kinapofika tunakosa muda na mambo ya ndoa, muda wote tunakuwa tunatafuta maji na muda wa kupikia watoto wetu unakuwa pia haupo. Hapo ukikuta mwanaume ana wivu ndio ugomvi hauishi siku akijisikia ndio anachukua baiskeli anaenda kutafuta maji,”anasema Akida.
Naye Zabibu Rashid wa Kitongoji cha Raha Leo, Kata ya Nangomba anadai kwamba amekuwa akipigwa na mume wake anapochelewa kurudi wakati wa kutafuta maji hali iliyomlazimu kupeleka malalamiko yake polisi.
“Tunapochelewa visimani tunapigwa na kuumizwa lakini hata wanaume tukiwapeleka polisi hawasikii. Mimi nimepeleka kesi mbili kituoni lakini hakuna kinachoeleweka,”anasema Zabibu.
Wazee wanasema wanaume wa sasa wana wivu kiasi cha kushindwa kufahamu halisi ya hali ya shida ya maji inayowakabili kijijini hapo ambayo wanaomba Serikali iwatatulie.
Mzee Athumani Naliwa (72) mkazi wa Kitongoji cha Raha Leo anasema amekuwa akipokea kesi za wanandoa wengi kwa ajili ya usuluhishi mmoja wapo akiwemo mtoto wake wa kuzaa aliyepigwa na mumewe baada ya kuchelewa kisimani.
“Unajua hawa wanaume wa kisasa wana wivu sana sio wote wanakuwa waelewa shida hii ya maji,”anasema Naliwa.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kilimanihewa, Abasi Mwira anasema hupokea kati ya kesi moja hadi mbili kwa mwezi zinazohusiana na masuala ya ndoa na kuzitafutia suluhu, nyingi chanzo chake ni kuchelewa kisimani.
“Mwanamke unakuta anaamka alfajiri anakwenda kisimani, akifika anakuta tayari wenzake washawahi hivyo analazimika kukaa foleni, sasa mpaka aje kurudi nyumbani muda unakuwa umeenda, akikutana na mwanaume aliyezidiwa wivu ndipo unaanza mgogoro,”anasema Mwira.
Diwani wa Kata ya Nangomba, Arabi Rabana anakiri kuwepo kwa migogoro ya ndoa inayochochewa na tatizo la maji
“Mtu mwingine utakuta amechoka tu na anaona uvivu kutembea umbali mrefu kutafuta maji, hivyo akipatikana wa kumchotea maji anaweza akasaliti ndoa yake au mahusiano,”anasema Rabana.
Lakini siyo wanaume wote ni wakatili kwa wake zao, baadhi kama Yusuph Mrope hulazimika kuwachotea maji wake zao.
“Kiutamaduni tumejijengea dhana wanawake ndio watafutaji wa maji na ni kweli lakini inapofikia msimu wa kiangazi mimi kama baba huchukua baiskeli na kwenda kutafuta maji kwasababu unakuta mama ni mgonjwa au anahitaji kumpeleka mtoto hospitali lazima nichukue majukumu yake kwa siku hizo,”anasema Mrope anayeishi kitongoji cha Raha Leo.
Mchango wa Benki ya Dunia
Katika jitihada za kutatua kero ya maji katika kijiji hicho cha Chipuputa, tayari Serikali imechimba kisima kwa msaada wa Benki ya Dunia katika mradi uliohusisha vijiji kumi vya Wilaya ya Nanyumbu ambacho kinahudumia na vijiji jirani. Hata hivyo, kisima hicho hakitoshelezi mahitaji yote ya maeneo hayo.
Mbunge wa Nanyumbu, Duwa Nkurua anasema kero ya maji inachangia migogoro katika familia kwasababu ushawishi unaweza ukasababishwa wakati watu wakiwa kwenye maeneo ya kutafuta maji.
Mkoa wa Mtwara ni miongoni mwa mikoa mitano inayoongoza kwa kiwango cha talaka huku ukiwa na kiwango cha zaidi ya asilimia nne ambacho ni juu ya wastani wa kitaifa wa asilimia tatu kwa Takwimu za Sensa ya Mwaka 2012 ingawa vyanzo vya talaka hizo havijawekwa bayana.
“Si vizuri mkeo atoke usiku kwenda kutafuta maji na kukaa huko muda mrefu. Hilo pia linaweza likachangia magonjwa kama Ukimwi kwasababu ushawishi unaweza ukapatikana visimani. Tatizo la maji linatoa mwanya kwa watu wengine kurubuniana,”anasema Duwa.
Kauli ya Mkuu wa Mkoa
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendego anasema hajafanya utafiti kujua ni kwa kiwango gani tatizo la maji linaathiri ndoa mkoani kwake, lakini amewataka wanandoa kushirikiana kutafuta maji hasa kipindi cha kiangazi.
“Niwaambie tu wanandoa wasivunje ndoa zao sababu ya maji, washirikiane mume na mke kuhakikisha nyumba zao zina maji katika kipindi ambacho maji sasa hivi yanapatikana mbali,”anasema Dendego.
Dendego anakiri kuwa upatikanaji wa maji hasa maeneo ya vijijini uko chini ikiwa ni asilimia 56 tu ndiyo wanaopata maji safi salama na katika wilaya moja moja kiwango hicho kinaweza kushuka hata kufikia asilimia 34.
Hata hivyo anasema mkoa una miradi 56 inayoendelea, kati ya hiyo 28 imekamilika na kwamba miradi mingine inayoendelea itakuwa imekamilika ifikapo Desemba mwaka huu hivyo kusaidia kupunguza tatizo la maji.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) hadi kufikia mwaka 2016 wilaya hiyo inakadiriwa kuwa na wakazi wapatao 107,117.
“Unaweza kuchimba visima lakini baada ya miaka mitatu vikakauka hata kama ni mita 100 na hasa wakati wa kiangazi visima vingi vinakauka.
Anasema wanapotoa huduma ya maji huzingatia vigezo vya kitaifa na kimataifa na WHO.
Rejea anasema mipango iliyopo ni uchimbaji wa mabwawa makubwa matano kati ya sasa na 2021 yatakayowanufaisha watu 37,000 na uchukuaji wa maji kutoka mto Ruvuma ulioanza mwaka 2015 na kwamba utakamilika kulingana na watakavyopata fedha na kwasasa mradi huo umeishafanyiwa upembuzi yakinifu.
Mradi huo kwa mujibu wa Rejea, utahusisha vijiji 29 pamoja na mji wa Mangaka ambapo wananchi wapatao 61,000 watanufaika. Hata hivyo gharama za ujenzi wake zinasubiri usanifu unaoendelea kufanywa.

No comments:

Post a Comment