OFISA wa benki, Khalid Mwinyi, dada yake, Rahma Mwinyi na Mchimba makaburi, Mohammed Maganga wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kumuua mwanaharakati wa kupinga ujangili na biashara haramu ya meno ya tembo, Wayne Lotter.
Washtakiwa hao walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.
Wakili wa Serikali, Adolf Mkini alidai washtakiwa wanakabiliwa na shtaka la mauaji kinyume cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu namba 19(C)sura ya 16 ya mwaka 2002.
Mkini alidai washtakiwa wote wanadaiwa Agosti 16, mwaka huu katika makutano ya barabara ya Chole na Haile Selasie wilayani Kinondoni, walimuua kwa kumpiga risasi mwanaharakati huyo kutoka Kampuni ya Pams Foundation ya Arusha.
Washtakiwa hawakutakiwa kujibu lolote kwa sababu mahakama hiyo, haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Oktoba 23, mwaka itakapotajwa tena.
Katika hatua nyingine, mshtakiwa Rahma Mwinyi, Mohammed Maganga na Mwanafunzi, Almas Swed walipanda kizimbani mbele ya Hakimu Mashauri kwa tuhuma za kupatikana na silaha na risasi 167.
Katika shtaka la kwanza washtakiwa hao wanadaiwa Septemba 16,mwaka huu maeneo ya Upanga, walikutwa na bunduki ya Uzigun na Rifle bila kuwa na kibali.
Shtaka la pili wanadaiwa kukutwa na risasi 167 walizokuwa wanamiliki bila kibali.
Wakili Mkini alidai katika shtaka la tatu kuwa washtakiwa wanadaiwa kukutwa na bomu la kutupwa bila ya kuwa na mamlaka ya kuwa nalo.
Washtakiwa walikana kutenda makosa hayo, upelelezi haujakamilika hivyo waliomba dhamana.
Wakili wa utetezi, Mluge Kaloli, aliomba mahakama iwape dhamana wateja wake kwa sababu mashtaka yanayowakabili yanadhaminika katika sheria.
Hakimu Mashauri, alikubali kuwapa dhamana washtakiwa naalikataa pingamizi la Jamhuri kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kufanya hivyo .
Mahakama iliwataka washtakiwa kuwa na wadhamini wawili, wawe na barua za utambulisho na wanatakiwa kusaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni 20.
Mshtakiwa mmoja, Almas ndiye anayepaswa kudhaminiwa na wadhamini walishindwa kutimiza masharti ya dhamana na hivyo alirudi rumande.
Washtakiwa wengine walirudishwa rumande hadi Oktoba 23, mwaka huu kwa ajili ya kesi yao kutajwa na hawatapata dhamana kwa sababu wanashtakiwa pia kwa mauaji.
No comments:
Post a Comment