Wednesday, October 4

Uchaguzi ‘bandia’ Afrika unakwaza maendeleo


Ni jambo la kawaida kwa viongozi walio madarakani katika nchi zinazoendelea kutumia vyombo vya dola kutetea nafasi zao ili waendelee kutawala zaidi bila kuzingatia matakwa ya wananchi au Katiba za nchi zao.
Wengine wanabadilisha Katiba hizo ili kuhalalisha uharamia wanaoufanya wa kuwapoka wananchi mamlaka waliyonayo ya kuiweka Serikali madarakani ama kuiondoa kupitia Uchaguzi Mkuu. Miaka zaidi ya 50 ya kujitawala kwa bara la Afrika, bado huo siyo utamaduni wetu.
Mapambano dhidi ya wakoloni yalilenga kuleta haki kwa wananchi kujitawala wenyewe na kuamua mambo yao. Bahati mbaya, viongozi wengi katika bara hili na nchi nyingine za ulimwengu wa tatu hawawekwi madarakani na wananchi wao bali wanatumia mabavu.
Viongozi waliokaa madarakani kwa muda mrefu wanatoka Afrika, hata ukifuatilia namna walivyoendelea kukaa madarakani ni kupitia mabadiliko ya Katiba zao ili ziwaruhusu kugombea tena na tena.
Mfano mzuri ni Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, yeye aliingia madarakani mwaka 1986 baada ya kuipindua serikali iliyokuwa madarakani wakati huo. Yeye akiwa kiongozi wa kikundi cha waasi cha NRM ambacho sasa ndiyo chama tawala akawa kiongozi wa Taifa hilo.
Ni miaka 31 sasa tangu alipoingia madarakani na kila wakati akiulizwa kama atagombea tena, hujibu kwamba chama chake ndiyo kitakachoamua kama aendelee au asiendelee.
Hivi karibuni, Bunge la nchi hiyo lilifanya mabadiliko ya katiba na kuondoa kipengele kinachotaka mgombea urais asizidishe umri wa miaka 75 ili kumruhusu Rais Museveni kugombea kwa mara nyingine.
Mchezo huo unafanyika sehemu mbalimbali Afrika, siyo Uganda tu. Uchaguzi unaandaliwa lakini matokeo yanakuwa yamepangwa na watawala. Wanapokumbana na vikwazo vya kikatiba basi katiba hizo hubadilisha mara moja kwa sababu vyama vyao vina wabunge wengi.
Hakuna mtu mmoja mwenye hati miliki ya nchi, nchi ni mali ya wananchi wenyewe, viongozi wamepewa dhamana ya kuilinda nchi hiyo kwa mujibu wa sheria zao.
Ninaamini kwamba bara hili lingekuwa mbali kimaendeleo kama viongozi wangekuwa na utashi na uzalendo wa kuzijenga nchi zao. Uchu wa madaraka umekuwa ndiyo chanzo cha umasikini wa bara hili, hakuna anayejali maendeleo ya watu wake.
Ni bora basi kiongozi akawa dikteta lakini anafanya mambo ya maendeleo ambayo kila mtu anatamani kiongozi huyo aendelee kutawala. Bahati mbaya hakuna anayefikiria mustakabali wa nchi yake bali familia yake tu.
Ule usemi wa kimagharibi kwamba ‘Afrika ni bara lenye giza’ hauta koma kama viongozi wetu ambao ndiyo wamepewa mamlaka ya kupanga rasilimali za nchi hawataweka uzalendo na kutumia rasilimali za nchi zao kikamilifu.
Tunahitaji kujisahihisha na kuangalia mataifa ya Ulaya na Marekani yalifanya nini kufika walipo sasa. Ni safari ambayo inahitaji kujitoa mhanga kwa maslahi ya Taifa zima.
Bila kuwa na fikra za maendeleo, kiongozi hata akae madarakani kwa zaidi ya miaka 50 hawezi kufanya jambo lolote litakaloleta tofauti nchini mwake. Uzalendo ndiyo msingi wa maendeleo na demokrasia ya kweli. Kukaa madarakani muda mrefu siyo dhambi kama kiongozi husika atafanya mambo ambayo yatabadilisha maisha ya watu wake.     

No comments:

Post a Comment