Wednesday, October 4

Siasa na maendeleo nchini Tanzania



Wanasiasa wote wanalenga kuleta maendeleo. Ukisoma sera na itikadi za vyama vyote vya siasa, vinalenga kuwaletea watu wake maendeleo. Pia, hata wananchi wa Tanzania, wanavutiwa na vyama vya siasa vyenye kulenga kuleta maendeleo: Elimu bora, afya, miundombinu mizuri, makazi bora, umeme na kuelekea uchumi wa kati. Serikali ya Awamu ya Tano, imeweka wazi kabisa kwamba inalenga Tanzania ya viwanda.
Tanzania ya viwanda, inalenga kwa kiasi kikubwa, kuendeleza uchumi wa Taifa letu, kuuongeza ajira na kuliondoa Taifa letu kwenye umasikini. Kwa vile uanzishwaji wa viwanda unahitaji wataalamu na mitaji ya kutosha, maandalizi yake hayawezi kuweka pembeni elimu ya ufundi, kufufua tena vyuo vya ufundi ambavyo kwa bahati mbaya vimegeuzwa kuwa vyuo vikuu, kuendeleza miundombinu ya barabara, kujenga fikra na kuhakikisha tuna nguvu za nishati ya kutosha kuendesha viwanda hivi, lakini pia kutafuta masoko ndani na nje ya nchi.Ni maandalizi makubwa, yasiyohitaji aina yoyote ya ushabiki na propaganda za kisiasa.
Tukumbuke maneno ya Mwalimu Nyerere, kwamba maendeleo huletwa na watu. Kwa maana, ni muhimu watu kushirikishwa kwenye mipango ya kuwaletea maendeleo. Bila kuwashirikisha watu, ni vigumu kuanzisha miradi ya maendeleo endelevu. Bila kuwashirikisha wahusika, kwa maana ya wananchi, miradi inaanzishwa na kufa na kuzikwa na waanzilishi. Tuna mifano mingi, kwa vile sote tunaishi Tanzania, basi turejee kwenye mifano hiyo kila mtu ndani ya nafsi yake.
Ili kuifikia Tanzania ya viwanda, tunahitaji nishati ya umeme ya kutosha. Serika ya Awamu ya Tano imeanza kufikiria na kutafuta vyanzo vya kuzalisha nishati ya kutosha. Bahati nzuri Tanzania tuna vyanzo vingi vya nishati. Hata kabla ya kufikiria vyanzo vyenye hatari na vyenye kuhitaji rasimali fedha nyingi na utaalamu wa hali ya juu kama vile uranium, tuna vyanzo kama vile gesi ya Mtwara. Wataalamu wanasema gesi ya Mtwara ya nchi kavu na ya baharini inaweza kutumika kuzalisha umeme na matumizi mengine zaidi ya miaka 80! Lakini, pia tunaweza kuzalisha umeme kutoka kwenye vyanzo vingine kama vile Jua na upepo.
Miaka hiyo 80, Tanzania itakuwa imezalisha wataalamu wengi na tutakuwa kwenye hali nzuri ya kuweza kupambana na athari za uranium na nyuklia. Leo hii bado tuna uwezo mdogo wa kumudu miradi yenye hatari kubwa kama hiyo. Tuvute subira, Tanzania ipo leo, kesho na keshokutwa. Kazi yetu kubwa ni kuilinda na kuitunza na kuirithisha Tanzania iliyo bora na salama kwa vizazi vijavyo.
Uzalishaji wa nishati
Ingawa kuzalisha nishati ya umeme kwa kutumia maji, haina hatari kubwa kama vile uranium, kuna sehemu ambazo uzalishaji huu unaweza kuleta athari kubwa kwa mazingira na kusitisha kwa kiasi kikubwa vivutio vya utalii katika Taifa letu. Kama uzalisha wa umeme unameza ardhi kubwa kiasi cha kupoteza makazi ya watu na viumbe vingine, ni bora kabisa kuachana na mradi hama huo mpaka tutakapokuwa na utaalamu wa kuendesha mradi huo bila kuathiri watu na viumbe vingine.
Malengo ya Rais Magufuli, ni pamoja na kuendeleza utalii katika Taifa letu. Ina maana hawezi kukubalina na mpango wa aina yoyote ile wa kuvuruga vivutio vya kitalii. Mpango wake wa kununua ndege kubwa ambazo zinaweza kufanya safari za Dar es Salaam hadi Washington nchini Marekani, Dar hadi China bila kusimama popote zinalenga kuleta watalii.
Haina maana kuwa na mipango ya kuwaleta watalii wakati tunapanga kupunguza vivutio vya utalii. Lengo ni kuongeza vivutio na si kupunguza vivutio hivi. Ukweli ni kwamba hadi sasa utalii unaingiza fedha nyingi kuliko viwanda, mazao na madini. Tanzania inaingiza dola bilioni mbili, kutokana na utalii. Hakuna kitu kingine kinachoingiza mapato kama hayo. Hivyo ni muhimu kulinda na kutunza vyanzo vyote vya utalii.
Mbuga ya hifadhi ya Selous, inaingiza zaidi ya dola milioni sita kwa mwaka na hasa kutokana na utalii wa kupiga picha. Sote tunafahamu kwamba mbuga hii iko kwenye urithi wa dunia. Tanzania ililiomba Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco), na kukubaliwa mbuga hii kuwekwa kwenye urithi wa dunia. Ombi hili lilikubaliwa mwaka wa 1982. Pia, ni vyema kukumbuka kwamba wakati Tanzania inapambana kuiweka Selous kwenye urithi wa dunia, ni wakati huo Tanzania na Zanzibar, zilikuwa na mpango wa kujenga reli ya Tazara, ambayo inapita kwenye mbuga hizo.
Pamoja na faida za reli hiyo katika jitihada za kuleta ukombozi kusini mwa Afrika na kuendeleza uchumi wa Tanzania na Zanzibar, iliifunua Selous kwa dunia na hasa kwa majangiri wa tembo. Sote tunafahamu kwamba mbuga ya Selous, inaongoza kwa ujangiri wa tembo. Mwaka 1976, Selous ilikuwa na idadi ya tembo 110,000. Kufikia 2014, ilikuwa na tembo 15,000! Mwaka huo wa 1976 Selous, ilikuwa na vifaru zaidi ya elfu mbili. Leo ni aibu hata kutaja idadi ya vifaru. Ndiyo maana Unesco imeweka Selous kati ya urithi wa dunia wenye kutishiwa uhai wake.
Mipango ya Serikali
Serikali ya awamu ya kwanza, ilikuwa na mpango wa kujenga bwawa la kuzalisha umeme kwenye mbuga hizi, mradi huu ulijulikana kwa jina la Stiegler’s Gorge.
Mwalimu Nyerere, alikuwa na mpango wa kuzalisha umeme. Lakini, kwa bahati mbaya hakupata fedha za kutekeleza mradi huu. Kama mradi huo ungetekelezwa ungeweza kuzalisha megawati 4,000. Hata hivyo maoni ya Cleopa Msuya, amabaye alikuwa waziri wa viwanda na biashara, kwa wakati huo ni kwamba hatukuhitaji umeme mwingi hivyo wakati huo.
Serikali za awamu ya tatu na ya nne, zilifuatilia wazo la Stiegler’s Gorge, kwa nguvu zote, lakini pia fedha hazikupatikana. Rais mstaafu Jakaya Kikwete, alikuwa amefikia pazuri kabisa, kupata fedha za kutekeleza mradi huu Stiegler’s Gorge, kutoka serikali ya nchi ya Brazil, kama si Waziri Mkuu wa Brazil kukumbwa na kashifa ya rushwa na kuondolewa madarakani. Hii ina maana kwamba wazo hili la Stieglers’ Gorge, limekuwa likija na kupita.
Rais Magufuli, anataka kufufua wazo la Stiegler’s Gorge. Kwa nia yake hiyo hataki kumsikiliza mtu yeyote mwenye nia na lengo la kukwamisha juhudi za jitihada zake za kuzalisha umeme kwenye mbuga za Selous. Katika harakati zake za Tanzania ya viwanda, amefikiri ni bora kufufua mradi huu ambao unaweza kuzalisha nishati ya kutosha. Wazo hili ni zuri sana. Sote tunaunga mkono maendeleo. Kama nilivyosema mwanzoni mwa makala hii ni kwamba wanasiasa wote na Watanzania wote wanatamani maendeleo.
Ninapoandika makala hii, tayari kampuni zaidi ya 50 zimejitokeza kutaka kutekeleza mradi huu wa Stiegler’s George, na wamekuja na kutembelea mbuga hizi. Ujenzi wa reli ya Tazara, uliifunua Selous kwa dunia na kusababisha tembo wetu kupungua kutoka 110,000 mwaka 1976 hadi elfu 54,000 mwaka 2014, je ujenzi wa Stieglers’s Gorge, mbali na kupunguza ukubwa wa mbuga hizi, utasababisha ujangiri zaidi? Je, hasara yake ni kubwa kuliko faida? Je, hakuna uwezekano wa kuzalisha umeme kutokana na vyanzo vingine? Kwa nini tukubali kufanya makosa ambayo tutahukuumiwa na vizazi vijavyo?
Hoja inayojengwa hapa ni je, tunaweza kuleta maendeleo na kulinda mazingira yetu? Ni lazima kupima faida na hasara kabla ya kuanza mradi wowote ule. Kama hasara ni kubwa, ni bora kuachana na mradi huo hata kama unaanzishwa nia njema. Tunasema tunza mazingira nayo yakutunze. Wataalamu wanasema mbuga za Selous, ni kama mapafu ya Dar es Salaam. Uharibifu wowote unaofanywa kwenye mbuga hizi ni lazima uleta athari kubwa kwa Jiji la Dar es Salaam, joto litaongezeka, mvua hazitafuata majira yake nk. Ukataji miti na kuodoa uoto wa asili, unaweza kuiingilia mabadiliko makubwa ya tabia nchi.
Lakini pia tukumbuke wajibu wa Tanzania kwenye kuzingatia na kutekeleza sheria za kimataifa. Tuliomba wenyewe kama Taifa, kuiingiza Selous, kwenye urithi wa dunia. Unesco, ilikubali. Hivyo Tanzania, haiwezi kufanya uamuzi wowote wa kubadilisha matumizi ya mbuga ya Selous, bila kujadiliana na Unesco. Miaka minne, iliyopita tulijadiliana na Unesco na kukubali kupunguza mbuga ya Selous, ili kuanzisha mradi wa uranium wa mto Mkunju. Sasa tunataka tena kumega mbuga hii kwa mita za mraba 1,500 na kuharibu kabisa mapitio ya wanyama kwenye mbuga hii na kwa kiasi kikubwa kupoteza urithi huu!
Mradi wa uranium
Makala juu ya mradi wa uranium mto Mkunju, inajitegemea. Ni bora watu wakafahamu athari ya uchimbaji wa uranium. Utafiti unaofanyika Mkunju na Bahi, umeacha mashimo ya uranium wazi, athari zake zimeanza kujitokeza. Serikali inakataa athari, hizi lakini wataalamu wanasema athari za uranium, zinajitokeza polepoe na zinachukua muda mrefu.
Mfano unga wa urenium, ukimwagika barabarani wakati wa kuisafirisha uranium, kwa maana Tanzania ni lazima kuisafirisha kwenda nje nya nchi, kwa vile bado hatuna kiwanda cha uranium, unga wa uranum, ukidondoka ardhini, athari yake ni zaidi ya miaka elfu moja. Ni hatari kuliko maelezo, sisi bado tunaangalia faida yake ya kuiuza uranium, na kupata afedha nyingi , lakini hatuangalii athari yake kwa watu, ardhi na viumbe.
Inaaminika kwamba bwawa la kuzalisha umeme kwenye mbuga za Selous, litakuwa na ukubwa wa nchi ya Zanzibar. Kilomita za mraba 1,500, wakati Zanzibar ina kilomita za mraba 1,300. Eneo hili ni kubwa sana kwenye mbuga ammbayo ni urithi wa dunia na ina vivutio vya utalii.
Uwanja wa ndege kwenye mbuga hizi utamezwa na bwawa hili na kusababisha mbuga hii ambayo ilikuwa ikiliingizia taifa letu zaidi ya dola milioni sita kwa mwaka isifike kwa urahisi na hasa wakati wa masika. Ukubwa wa bwawa hilo utafunika sehemu kubwa ambayo iliwatunza wanyama na ilikuwa sehemu nzuri ya watalii kupiga picha. Pia, hoteli kubwa iliyo kwenye mbuga hii itaathirika kutokana na ujenzi wa bwawa hili.
Kuipunguza Selous
Miaka minne iliyopita Unesco, ilikubali kupunguza mbuga ya Selous, kwa kiasi cha mita za mraba 350, kwa ajili ya mradi wa mto wa Mkunju, wa uranium. Ingawa mradi huu ni wa hatari kubwa kuliko faida zake, hakukuwa na ulazima wa kuanzisha mradi huu jirani na vivutioa vya utalii. Hoja hapa ni kwamba mradi wa uranium wa Mkunju na mradi huu wa chanzo cha umeme kwenye mbuga za Selous, ni kutaka kuiua kabisa mbuga hii ambayo inaleta faida kwenye taifa letu na kulitangaza taifa letu duniani.
Ukweli ni kwamba tuiitunza Selous, Ruaha na Katavi, tunaweza kuwavutia watalii wengi kwenye maeneo ya kusini hata kuzidi wale wanaokwenda kaskazini Serengeti na mbuga nyingine za huko kuuzunguka mlima Kilimanjaro.
Mwezi wa sita mwaka huu, Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Serikali ya Ujerumani na mashirika ya WWF, Frankfurt Zoological Society na KFW yote ya Ujerumani, jirani na mtoto Tagalila, walizundua nguvu za pamoja za kulinda uhai wa Seolus, ambao ulijulikana kama SECAD (Selous Ecosystem and Conservation Development Project).
Kupitia mradi huu, Ujerumani peke yake tayari imetoa Euro milioni 18, ili kuendeleza miundombinu ya Selous. Sasa hivi, utalii wa Selous, unafanyika kwenye kiangazi na kufungwa Desemba hadi mwezi wa tano kwa sababu ya mvua na barabara kutopitika. Kwa msaada huu, Selous, itafikika mwaka mzima na kuongeza pato la Taifa.
Kama tungekuwa na mfumo wa kumfikishia rais wetu maoni ya wanananchi, tungefanya hivyo. Kupitia kwenye makala, ni kwamba hatukufanikiwa kufanya hivyo njia nyingine na wala haina lengo la kumpinga Rais au uchochezi wa aina yoyote ile. Tuna imani kwamba kumuunga Rais wetu mkono ni pamoja na kumueleza ukweli, kumficha ukweli kwa lengo la kumfurahisha na kutafuta sifa kutoka kwake, ni dhambi kubwa. Tanzania ni yetu sote na ilazima tushirikiane kuijenga.
Maoni yetu na kusema ukweli yanaungwa mkono na Watanzania walio wengi. Ni kwamba kwa vile tuna vyanzo vyingi vya kuzalisha nishati ya umeme, ni bora kusitisha mpango wa kufufua mradi wa kuzalisha umeme wa Stiegler’s Gorge. Tuangalie uwezekano wa kutumia gesi ya Mtwara, upepo wa Singida na miradi ya kuzalisha nishati ya juu kama vile mradi wa kule Kigoma. Pia kuzalisha nishati ya umeme kwa kutumia maji ambayo hayana athari kwa watu na viumbe.
Padre Privatus Karugendo
pkarugendo@yahoo.com
+255 754 633122     

No comments:

Post a Comment