Wednesday, October 25

Kenya haijatulia lakini iko mbali kisiasa

Mahasimu wa kisiasa nchini Kenya, Rais Uhuru
Mahasimu wa kisiasa nchini Kenya, Rais Uhuru Kenyatta wa Jubilee na Raila Odinga wa muungano wa National Super Alliance (Nasa). Picha ya Maktaba 
Waswahili wanasema ukiona maharage yanarukaruka kwenye chombo ujue ndiyo yanaiva. Kinachoendelea sasa nchini Kenya ni ishara kwamba demokrasia imepamba moto na muda mrefu nchi hiyo itakuwa imeiva kidemokrasia.
Ni tofauti na nchi nyingi barani Afrika zinazofuata mfumo wa vyama vingi tangu uliporejeshwa mwanzoni mwa miaka ya 1990.
Walau Kenya naweza kusema imepiga hatua, japo nayo haikuwa rahisi. Siasa za Kenya mara nyingi huwa hazitabiriki, japo wanasiasa ni walewale lakini vyama vimekuwa vikibadilishwa mara kwa mara huku pia kambi zao nazo zikibadilishwa.
Awali wakati mfumo wa vyama vingi unaanzishwa, Rais aliyekuwepo madarakani Daniel arap Moi aliendelea kushinda kupitia chama tawala cha Kanu hadi mwaka 2002 alipoamua kumwachia Uhuru Kenyatta ambaye ni mtoto wa mwasisi wa Taifa hilo, Jommo Kenyatta.
Hata hivyo, uteuzi wa Kenyatta wakati ule ulionekana kama upendeleo hivyo kusababisha wanachama wengi wa Kanu kujitoa huku kambi ya upinzani iliyoundwa wakati huo (National Alliance of Rainbow Coalition – (NARC) ikipata nguvu.
Muungano huo uliundwa na vyama vya NAK (sasa NAPK) na chama cha Liberal Democratic- LDP na ulimsimamisha Mwai Kibaki kuwa mgombea wao, akipigiwa debe na wanasiasa maarufu wakati huo kama Raila Odinga.
Haikushangaza Kibaki akimshinda Kenyatta kwa kupata asilimia 62 za kura dhidi ya asilimia 31 za Kenyatta.
Hata hivyo, Narc wakati wa mabadiliko ya Katiba ya Kenya mwaka 2005 viongozi wa LDP walitupwa nje ya Serikali ya Kibaki, jambo lililosababisha waunde Vuguvugu la Chungwa (Orange democratic Movement ikiwa chini ya Raila Odinga.
Wafuasi waliomuunga mkono Kibaki wakaunda chama cha Narc Kenya, huku Narc ya asili ikibaki chini ya uenyekiti wa Charity Ngilu.
Katika uchaguzi wa mwaka 2007, Ngilu alimuunga mkono Raila Odinga katika urais ambapo alifanikiwa kupata wabunge watatu wa Narc. Uchaguzi huo ndiyo ulishuhudia mauaji ya kutisha ya zaidi ya Wakenya 1,000 baada ya Mwai Kibaki wakati huo akiwa na chama cha Party of National Unity (PNU).
Kibaki aliyepata asilimia 46 za kura aliapishwa Ikulu Desemba 30, 2007 huku pia Odinga akidai kushinda, jambo lililosababisha vurugu na kisha mauaji.
Mvutano huo ulimalizwa kwa kuundwa kwa sheria ya mapatano na usuluhishi huku Odinga akiteuliwa kuwa Waziri Mkuu.
Kufuatia machafuko hayo, Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Kivita (ICC) iliwatuhumu Rais Uhuru Kenyatta na Makamu wake William Ruto kuhusika.
Wengine waliotajwa kwenye kesi hiyo iliyokuwa ikisikilizwa The Hague nchini Uholanzi ni mtangazaji wa radio, Joshua arap Sang.
Kesi hiyo ilikuja wakati Kenya ikijiandaa na uchaguzi wa mwaka 2013, huku Kenyatta na Ruto wakiunganisha vyama vyao na kuunda umoja wa Jubilee na kumshinda Odinga na kundi lake la ODM.
Baada ya tu ya kushindwa wawili hao waliandamwa na kesi hiyo ambayo hata hivyo ilikuja kuyeyuka. Licha ya kuyeyuka, kesi hiyo iliwapa doa kubwa. Watawashukuru sana marais wa Afrika waliopambana kuishutumu ICC kuwa inaonea viongozi wa Afrika.
Sasa umekuja uchaguzi wa mwaka huu ambao awali Jubilee ilitangazwa kushinda Agosti 10, lakini matokeo yake yakabatilishwa na Mahakama Kuu ya Kenya, kufuatia kesi iliyofunguliwa na Odinga na wenzake.
Uchaguzi wa marudio unatarajiwa kufanyika Oktoba 26, lakini tayari Odinga na timu yake wameshajitoa na wamepanga kufanya maandamano kuhakikisha uchaguzi huo haufanyiki.
Kuna mambo muhimu ya kujifunza katika siasa za Kenya mwaka huu. Kwanza, machafuko yaliyotokea Kenya mwaka 2007 yameweka doa kubwa kwa nchi hiyo, hivyo viongozi wao hawataki yajirudie, kwa maana hiyo wanakuwa na nidhamu kwa wananchi.
Pili, kitendo cha Uhuru na Ruto kushtakiwa ICC pia kimewapa kitisho na wasingependa hilo litokee tena. Kwanza wanahofia kuitwa tena kwenye mahakama hiyo, kwa hiyo wanakuwa na nidhamu na madaraka waliyonayo.
Tatu, mabadiliko ya Katiba ya Kenya yameifanya nchi hiyo kuwa na utawala bora ambao viongozi wake wanaheshimu mihimili ya Dola na sheria. Ndiyo maana Mahakama ya Kenya inaweza kubatilisha matokeo ya urais na hivi karibuni imetengua amri ya kukataza maandamano ya wafuasi wa ODM.
Kwa Tanzania hali ni tofauti, pengine ni kwa sababu haijapitia historia ya Kenya. Leo mikutano na maandamano ya vyama vya siasa yamezuiliwa, uhuru wa vyombo vya habari uko shakani, uhuru wa maoni nao unaelekea wapi? Nani anasimama kuitetea demokrasia ya Tanzania?  

No comments:

Post a Comment