Wednesday, October 25

TBL yazidi kukata mbuga mauzo DSE


Dar es Salaam. Gawio la Sh470 kwa hisa limeendelea kuvutia uuzaji na uwekezaji katika hisa za Kampuni ya Bia ya Tanzania (TBL) ambayo imeongoza tena katika mauzo kwa wiki tatu mfululizo.
Tangu Oktoba 6 kampuni hiyo imekuwa ikiongoza kwa mauzo katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), huku kwa majuma matatu mfululizo mauzo yake yakikuwa zaidi ya asilimia 70 ya mauzo yote.
Kwa mujibu wa takwimu za DSE wiki iliyoishia Oktoba 6 kampuni hiyo iliuza asilimia 74 na wiki iliyoishia Oktoba 13 asilimia 99.6 kabla ya kuuza asilimia 89 wiki iliyoishia Oktoba 20.
Baadhi ya wachambuzi wa soko hilo wanasema wawekezaji wengi wamevutiwa na gawio la awamu ya pili lililotangazwa na kampuni hiyo la Sh470 kwa hisa moja zaidi ya mara nne ya gawio la awamu ya kwanza la Sh100.
Mtendaji mkuu wa kampuni ya Zan Securities, Raphael Masumbuko alisema hisa zinanunuliwa zaidi na wawekezaji wa nje ambao hupenda kuwekeza katika kampuni ambazo zipo imara.
Hata hivyo, wakati TBL ikiendelea kuongoza katika mauzo ya hisa, hisa za Kampuni ya Sigara ya Tanzania (TCC) zimeongoza kwa kuimarika zaidi sokoni baada ya bei yake kupanda kwa asilimia saba, ambayo ni kubwa kuliko nyingine zilizoorodheshwa katika soko hilo.
Bei ya hisa za TCC ilianza wiki kwa kuuzwa Sh14,600 lakini ilimaliza kwa kuuzwa Sh15,600, ikifuatiwa na TBL iliyoongezeka kwa asilimia tatu kutoka Sh13,500 hadi Sh15,900 na Benki ya CRDB kwa asilimia moja.
Pia, tathmini ya DSE kwa wiki iliyoishia Oktoba 20 inaonyesha thamani ya mauzo ya hisa imepungua kutoka Sh30 bilioni kwa wiki iliyoishia Oktoba 13 hadi Sh23 bilioni, huku idadi ya hisa zilizouzwa na kununuliwa zikiongezeka kutoka milioni 2.5 hadi milioni 2.8.
Ukubwa wa mtaji wa kampuni zilizoorodheshwa DSE umeongezeka kwa Sh463 bilioni kutoka Sh20.4 trilioni hadi Sh20.9 trilioni ndani ya wiki iliyoishia Oktoba 23.
Ongezeko hilo limetokana na kupanda kwa bei za hisa za Uchumi Super Market (USL) kwa asilimia 14, Shirika la Ndege la Kenya (KA) kwa asilimia 10 na Kampuni ya Acacia kwa asilimia tisa.

No comments:

Post a Comment