Wednesday, October 25

ISIWE SIASA YA KUJENGA NA KUBOMOA TAIFA LETU

Mkuu wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist
Mkuu wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo, akionyesha eneo la mradi litakapozalisha umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge Dam),ambao utakuwa na uwezo wa kuzalisha megawatts 2,100 za umeme. (Picha ya Mtandao) 
Serikali ya awamu ya tano, inayoongozwa na Rais John Magufuli, ina mipango mingi ya kuleta maendeleo katika taifa letu. Na ukweli ni kwamba Watanzania walio wengi wanaunga mkono mipango hii ya maendeleo.
Huwezi kupinga ujenzi wa viwanda, ujenzi wa mabweni ya wanafunzi, kupambana na ufisadi, barabara, umeme, treni na mengine mengi. Tunataka maendeleo.
Hata hivyo, bado ni haki ya kikatiba wananchi kuhoji na kutoa michango yao ya mawazo. Tunaamini Serikali hii ina nia njema kama ile tuliyonayo sote tunaoishi Tanzania. Na tunaamini kwamba Serikali hii itajenga maendeleo haya juu ya msingi uliopo na wala si kuanzisha utamaduni wa kujenga na kubomoa.
Hapa twapaswa kuunga mkono wale wote wenye mawazo ya Katiba mpya. Kwamba pamoja na mipango mizuri ya Serikali ya awamu ya tano, ili kuhakikisha kwamba kesho na keshokutwa wenye kutaka kubomoa wasifanye hivyo kwa mapenzi yao, bali mapenzi ya taifa zima, ni muhimu na ni lazima tuwe na Katiba Mpya.
Kwa maana ya Katiba iliyowashirikisha wananchi wote. Kesho na keshokutwa akija wa kutaka kubomoa, wananchi hao watakataa na kulindwa na Katiba yao. Katiba ya leo na ile iliyopitishwa kwa mbinde na Bunge Maalumu la Katiba, bado ina mapendo mengi ya kuruhusu kubomoa bila kusikiliza kilio cha wengi.
Tunajua sote kwamba kazi ya kubomoa ni nyepesi, ukilinganisha na kazi inayofanyika wakati wa kujenga. Hivyo kwa kuhakikisha tunatumia nguvu kidogo na rasilimali kiduchu, tusibomoe kwa lengo la kujenga tena.
Tukishikamana, ni bora kukarabati kuliko kujenga upya. Hoja hapa ni kwamba tusifishe kitu kimoja kwa kutaka kuendeleza kingine. Kama hakuna hatari ya kupoteza uhai, ni heri kuachana na mpango wa kuua kitu kimoja ili kuanzisha kingine. Kama kuna hatari ya uhai, basi hakuna jinsi, ndiyo maana tunasema hali kama hii ni lazima ionekane wazi kwenye Katiba na kuelekeza la kufanya endapo hali kama hiyo inajitokeza.
Mfano, mzuri hapa ni ule wa Selous. Wazo la kutaka kujenga bwawa la kuzalisha umeme, ni wazo la kubomoa. Ninaomba kukosolewa kama nimekosea. Ni kutaka kubomoa Selous, kwa lengo la kuzalisha umeme.
Ni wazi tutapata umeme na utachangia kuleta maendeleo, lakini tutakuwa tumebomoa yale ambayo watu wengine wameyajenga kwa miaka mingi. Kama na wao wangetawalia na mfumo huu wa kujenga na kubomoa, leo hii tusingekuwa na mbuga za wanyama.
Kuweka shughuli zozote ambazo zitaharibu mazingira na kuwafukuza wanyama, vyovyote vile ni kubomoa. Mfano, tulioutoa hapo juu wa hatari ya kupoteza maisha. Je, bila kujenga Bwawa la kuzalisha umeme Selous, kuna uhai utapotea? Ni wazi sasa hivi hatuna Katiba ya kutetea na kuelekeza hili. Lakini, katika hali ya kawaida ya kuzungumza na kuulizana maswali, tusipojenga bwawa, ni nani atakufa? Bwawa likijengwa, pamoja na faida nyingi, kuna athari kibao. Hivyo, kwa kujiuliza nani anakufa na nani anapona kwa hatua ya kuamua kujenga bwawa la Selous, jibu la wazi ni kwamba kifo ni kujenga na uhai ni kuachana na ujenzi huo.
Na hapa hakuna suala la kumpenda mtu au kumchukia mtu. Hakuna uchochezi au kitu kingine kinachofanana na hicho. Hapa ni hoja na ukweli ambao unapokuwa mchungu, tunatafuta visingizio. Na mwenye nguvu, anazitumia nguvu zake kunyamazisha upande mwingine. Ndiyo maana tunaandika, maana wahenga wanasema kilichoandikwa kimeandikwa, historia itakuwa hakimu.
Hapa ni lazima kuelewana na kukubaliana kwamba kila hoja inalenga kulijenga taifa letu. Wanaokazania kubomoa, wana nia njema, lakini pia na wale wanaosema tusibomoe, wana nia njema pia. Sote ni Watanzania na sote tuna haki ya kuishi. Ili tukubaliane, ni lazima kuongea na kujadiliana. Tunahitaji jukwaa la majadiliano, si jukwaa la kuimba na kupiga makofi, bali jukwaa la kusikiliza, kusikilizwa na kufikia uamuzi wa pamoja.
Na msisitizo hapa ni kwamba jukwaa huru, ni lile linaloongozwa na Katiba mpya.
Tanzania ina vyanzo vingi vya kuingiza mapato. Ukiachia mbali madini, mazao ya kilimo, gesi na mengine mengi, tuna utalii. Chanzo hiki cha utalii ni kikubwa na kuna takwimu zinazoonyesha jinsi utalii unayoingiza fedha za kutosha kwenye taifa letu.
Hivi karibuni, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, wakati akifungua SITE (Swahili International Tourism Expo), alisema kwamba miaka minane kutokea sasa, 2025, Tanzania inategemea kupata bilioni 16 ( kama milioni 7 USD) kutoka kwenye utalii.
Ingawa hiki bado ni kiwango kidogo kutoka kwenye utalii, ukilinganisha na vivutio vingi tulivyonavyo kwenye taifa letu, lakini huwezi kukivuruga chanzo hiki chenye mapato kiasi hiki bila kuwasikiliza wananchi.
Na ili kutenda haki, ni muhimu kuangalia maamuzi ya leo yanaathiri vipi vizazi vijavyo. Sisi tumevipokea vyanzo hivi vya mapato kutoka kwa wazazi wetu na ni jukumu letu kuvirithisha kwa vizazi vijavyo.
Ni bahati mbaya kwamba kuna dalili za kutaka kujenga utamaduni wa kuishi leo, bila kuangalia kesho. Utamaduni ambao unafumba macho kwa vizazi vijavyo. Utamaduni wa kutotaka kurithisha vizazi vijavyo. Utamaduni unaotupelekea hata kudanganya umri ili watu waendelee kufanya kazi serikalini bila kuwarithisha vijana.
Hata kwenye nafasi kama ubunge, tunaona wazee bado wanataka kuendelea. Ni utamaduni uleule wa kutotaka kurithisha wengine. Tujifunze kurithisha, tumepata bure tutoe bure. Maandiko matakatifu yanatufundisha hivyo.
Selous peke yake inaingiza dola milioni sita kwa mwaka. Kiasi hiki ni kidogo ukilinganisha na nchi nyingine zinazotegemea kuingiza mapato yake kupitia kwenye utalii. Nchi hizi hazina vivutio vingi kama sisi, lakini kwa vile zimekwepa mfumo wa kujenga na kubomoa, zinafanya vizuri sana.
Mfalme wa Morocco, Mohammed VI alipoitembelea Tanzania kwa mwaliko wa Rais Magufuli, tulielezwa kwamba nchi yake inaingiza dola 12 milioni kwa mwaka kutoka kwenye utalii.
Kwa nini Morocco, wanafanya vizuri zaidi yetu? Ndiyo maana baadhi yetu tunaleta hoja ambazo zinaonekana ni za upinzani, pale tunapoona mifumo ya kuendeleza utalii katika taifa letu inavurugwa. Tunaitetea Selous, kwa misingi hii. Tunaamini kwamba Selous ikiachwa ikaendelea na kazi zake bila kuingiza ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme, tunaweza kupata fedha nyingi kutokana na utalii. Pia, hii itatusaidia kukabiliana na wimbi kubwa la mabadiliko ya tabia nchi.
Nchi kama Morocco, zimefanikiwa kiasi hicho kwa kuendeleza vyanzo hivi vya mapato kupitia utalii. Wametengeneza miundombinu na kuhakikisha watalii wanaweza kwenda na kuangalia vivutio hivi bila matatizo ya usafiri.
Hivyo utalii unafanyika muda wote, kiangazi na masika. Kinyume na ilivyo kwa upande wetu, mfano Selous, inatembelewa wakati wa kiangazi tu.
Sote tunajua kwamba Serikali ya Ujerumani tayari imetenga fedha kiasi cha Euro milioni 18, kuendeleza miundombinu ya Selous. Pia, imetoa vifaa vya kuilinda hifadhi hiyo kutokana na majangili. Wakati Makamu wa Rais Mama Samia, anasema ndani ya miaka minane kuanzia sasa tunategemea kupata zaidi ya bilioni 16, kutoka kwenye utalii kwa mwaka, ukweli ni kwamba kiwango hiki bado kiko chini ukilinganisha na Morocco. Serikali ya Ujerumani, kwa msaada wake wa kuendeleza miundombinu ndani ya hifadhi ya Selous, inalenga kupandisha kipato chetu kutoka kwenye utalii.
Tukisaidiwa ujenzi wa miundombinu kwenye mbuga za Selous, na sisi tukavuruga miundombinu hii kwa kujenga bwawa la kuzalisha umeme, pamoja na nia njema nyuma ya ujenzi wa bwawa hili, hatutaeleweka na kusema ukweli tutakuwa tunaendeleza utamaduni wa kujenga na kubomoa. Ndiyo maana tunasisitiza kwamba kabla ya kujenga bwawa hili, maana kama Serikali imesema na inataka, litajengwa tu. Sisi tunasema ni bora ufanyike utafiti kwanza na kujihakikishia changamoto zilizopo na njia ya kusaidia kuziondoa. Ni bora bwawa lisijengwe, lakini likijengwa ni bora kufahamu changamoto zilizopo na jinsi ya kuzitatua.
Hadi sasa mapato makubwa yanayotokana na utalii, yanapatikana kutoka Kaskanini, mbuga za Manyara, Serengeti. Lakini, mbuga za Ruaha, Katavi na Selous zenye vivutio vingi, bado hazijaendelezwa. Kinachohitaji na kuendeleza mbuga hizi na kuvuna mapato kutokana na utalii.
Tukiongeza nguvu upande wa kusini, na kuhakikisha tuna barabara nzuri, madaraja na viwanja vya ndege, tunaweza kuwa na uhakika wa kupata watalii zaidi milioni mbili kwa mwaka. Kiwango hiki kikubwa cha watalii, kitaupaisha uchumi wa taifa letu.
Tumeeleza kwenye makala zilizopita kwamba kiwanja cha pekee kwenye mbuga za Selous, kiko jirani kabisa na sehemu itakayojengwa bwawa la kuzalisha umeme. Kwa ukaribu uliopo, hakuna jinsi ya kukitunza kiwanja hiki. Kitafunikwa na maji baada ya kujenga bwana la kuzalisha umeme. Athari nyingine tulizitaja kwenye makala zilizotangulia.
Hivyo kwenye suala hili la Selous, ni bora hekima ikatumika. Si haki kabisa kujificha kwenye kivuli cha chuki na kupenda. Ni lazima tuanzishe utamaduni wa kujadiliana na kusikiliza usiyopenda kuyasikia. Watanzania tuko milioni zaidi 50, hivyo mawazo yatakuwa tofauti, ila ni muhimu kuhakikisha mnalenga pamoja kama taifa. Na muhimu zaidi ni kuwa makini na kuhakikisha siasa za kujenga na kubomoa zinawekwa pembeni.
Padre Privatus Karugendo
pkarugendo@yahoo.com
+255 754 633122 

No comments:

Post a Comment