Upinzani pia umekuwa ukitaka kampuni ya OT-Morpho inayosimamia upeperushaji wa matokeo kielektroniki, isiendelee kufanya kazi hiyo.
Lakini, juhudi za upinzani zinaonekana kuchukua mkondo mpya baada ya msururu wa matukio katika IEBC na ulingo wa uchaguzi 2017.
Maombi ya Nasa ya kutaka mabadiliko kabla uchaguzi mpya ufanyike, hayajafanikiwa ijapokuwa malalamiko yao yamethibitishwa na baadhi ya viongozi wa tume hiyo ya uchaguzi.
Wiki jana, Kamishna wa IEBC, Dk Roselyn Akombe alijiuzulu na kukimbilia Marekani anakofanya kazi ambapo alituma taarifa kueleza kwa nini aliamua kuondoka IECB.
Akome anasema ingawa IEBC inasisitiza kuwa uchaguzi mpya wa urais unafanyika Alhamisi wiki hii, kuna dosari si haba ambazo zitazuia uchaguzi huo utakuwa huru na haki.
Kwanza kabisa, Dk Akombe ambaye ana uraia wa nchi mbili, Marekani na Kenya, anasema IEBC imetekwa na wanasiasa ambao hutisha maisha ya wafanyakazi wa ngazi za juu kama vile makamishna na waliopewa majukumu ya kusimamia teknolojia za kuhakikisha uchaguzi huo unakwenda vizuri.
Dk Akombe amemlaumu Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO), Ezra Chiloba kwa kile anachokitaja kuwa kuhujumu uchaguzi wa Agosti 8 kwa kuwaruhusu watu wasiohusika kuingia kwenye kompyuta za matokeo ya uchaguzi na kusababisha wizi wa kura uliompa ushindi Rais Uhuru Kenyatta ambao ulifutwa na Mahakama ya Juu, Septemba Mosi.
Dk Akombe, ambaye anadai maisha yake yalikuwa hatarini baada ya kupokea vitisho vingi kuhusiana na msimamo wake kwenye Tume, alidai uchaguzi wa Oktoba 26 haufai kuendelea ikiwa viongozi wanajali hatma ya baadaye ya nchi.
Ijapokuwa Dk Akombe amehoji jinsi uchaguzi utakavyofanyika ikizingatiwa kuwa kuna vikwazo kadhaa, mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati anasema uchaguzi utafanyika ingawa hawezi kutoa hakikisho kuwa litakuwa la huru na haki.
Chebukati anakubaliana na Dk Akombe kuwa kuna dosari zinazoweza kuathiri matokeo ya kura hiyo. Lakini je, kama kuna dosari kwa nini uchaguzi huu ufanywe?
Chama tawala cha Jubilee kinasema uchaguzi huo hauna budi kufanyika kwa sababu Wakenya wako tayari kushiriki zoezi hilo.
Nasa yapinga
Matamshi ya Jubilee yanakinzana na za Nasa inayoongozwa na Raila Odinga ambayo inasema na kusisitiza kura hiyo haitafanyika kwa sababu njama za kutosha zimefanywa na Serikali ya Jubilee kuhakikisha Rais Uhuru anashinda uchaguzi huo.
Raila amewaambiwa wafuasi wake zaidi ya milioni sita unusu wasubiri tangazo lake la muhimu siku moja kabla ya uchaguzi. Wengi wanajiuliza Raila atasema nini siku hiyo Oktoba 25. Baadhi wanakisia kuwa atabadilisha uamuzi wake wa kutoshiriki uchaguzi huo.
Lakini, mazingara ya siasa humu nchini hivi sasa hayawezi kumpa kiongozi huyu wa upinzani nafasi ya kushiriki zoezi hilo. Hii ni kwa sababu ngome zake kisiasa zimekuwa zikijitenga na matayarisho ya uchaguzi huo.
Raila anakariri matamshi ya Dk Akombe kuwa hakuna tofauti kati ya Jubilee na IEBC kwa sababu taasisi hizi mbili zinashirikiana na tume hiyo haina uhuru wa kujisimamia na kufanya uchaguzi wa haki.
Chebukati amejaribu kufanya marekebisho kulingana na amri ya Mahakama ya Juu uliotolewa na Jaji Mkuu David Maraga aliyesema uchaguzi mpya ufanywe kulingana na uzingatiaji wa kikamilifu wa sheria za uchaguzi.
Ni masikitiko makubwa hata hivyo kung’amua kwamba, juhudi za Chebukati zimeambulia patupu kwa sababu ya tofauti miongoni mwa maofisa wa ngazi za juu katika tume hiyo.
Wengi, kulingana na Chebukati, wanaegemea upande wa Jubilee na kwa hivyo wakati wa kuamua jinsi mchakato mzima wa uchaguzi unafaa kufanywa, huwa maamuzi au mapendekezo yake yanatupwa ama kupuuzwa na makamishna wanaoegemea mrengo wa Jubilee.
Upatanisho wakwama
Mwenyekiti wa IEBC amejaribu kuwapatanisha Raila na Uhuru ili kuwe na msimamo mmoja juu ya uchaguzi huo, lakini mambo yameshindikana.
Wiki tatu zilizopita, Rais Uhuru alimtuma naibu wake William Ruto kwenye mkutano na Chebukati. Hata hivyo, Ruto alifika kwenye mkutano huo akiwa amechelewa na Chebukati na Raila wamekwisha maliza mazungumzo.
Kwenye wito wa juzi wa Chebukati kwa viongozi hao wawili kukutana ili kuwe na mtazamo mmoja wa nchi kuhusu zoezi hilo, Rais Uhuru hakufika huku taarifa kutoka Ikulu ya Nairobi zikisema kiongozi wa nchi hatofika mkutanoni kwa sababu yeye ni Rais na haifai kuitwa na watu walio chini yake.
Ingekuwa jambo la maana kwa viongozi hao kukutana, ili hali ya taharuki inayogubika nchi wakati huu iweze kuyeyushwa. Si vyema kwa viongozi kujipiga kifua ilhali hatma ya nchi haieleweki.
Kisheria, Chebukati ana uwezo wa kwenda Mahakama ya Juu kuomba aongezewe siku zaidi, ili uchaguzi ufanyike kwenye mazingara tulivu na ambayo Wakenya wote wana imani nayo.
Kwa wakati huu, hali ya anga ya uchaguzi huo inaashiria mandhari ya kusikitisha. Maeneo yenye ufuasi mkubwa wa Nasa yameapa hayatafanya uchaguzi. Maofisa wa kusimamia kura katika sehemu hizi wamekuwa wakikumbwa na matatizo chungu nzima wanapojaribu kuandaa matayarisho.
Baadhi yao wametishiwa maisha na kuonywa wasithubutu kufika kwenye vituo vya kupigia kura ama wataona cha mtema kuni. Wiki jana, warsha za maofisa wa IEBC mashinani zilivurugwa katika maeneo mbalimbali na kulazimisha maofisa wa polisi kuingilia kati na kuwakinga.
Je, uchaguzi utafanywa vipi katika sehemu hizi ambazo hazijafurahia warsha za watakaosimamia zoezi hilo?
Licha ya Nasa kupinga zabuni iliyopewa kampuni ya Al Ghurair kuchapisha karatasi za kupigia kura, kilio chao kilipuuzwa. Mnamo Oktoba 20 (Siku kuu ya Mashujaa) karatasi ziliwasili nchini tayari kwa uchaguzi wa Alhamisi.
Upinzani umeituhumu kampuni hii kwa kuwa na uhusiano wa karibu na familia ya Rais Uhuru tangu zamani. Pia, Nasa inasema katika uchaguzi wa Agosti 8, Al-Ghurair ilidaiwa kuchapisha karatasi ambazo hazikuwa zimeidhinishwa kuchapisha ikiwa na njama za kuhujumu kura na kumpa Uhuru ushindi.
Yote tisa, ya kumi ni kwamba, wasiwasi uliokuwa umewaangukia baadhi ya Wakenya kuhusu ikiwa Chebukati anaweza kujiuzulu kabla ya uchaguzi, sasa umedidimia kwa sababu mwenyekiti huyo wa IEBC amewahakikishia Wakenya kuwa hawezi kujiuzulu kwa sababu Kenya inamuhitaji sasa kuliko wakati mwingine wowote ule.
Wiki jana, Chebukati alikuwa ametishia kujiuzulu ikiwa wanasiasa hawataacha kuingilia shughuli na mipango ya tume hiyo.
Licha ya vizingiti vyote, ishara zote sasa zinaonyesha uchaguzi utafanyikwa inagawa sehemu nyingine zinaweza kukosa kupiga kura.
Ikiwa kuna sehemu ambazo hazitapiga kura, sheria inakubali mwenyekiti wa tume ya IEBC kutayarisha kura katika maeneo hayo kwa muda usiozidi siku saba.
Hata hivyo, Raila huenda akaelekea katika Mahakama ya Juu kwa mara nyingine kupinga ushindi wa Rais Uhuru kwa sababu mazingira ya uchaguzi huo yamesheheni dosari na hitilafu mbalimbali.
Lakini upande wa Jubilee, kupitia kwa wabunge wao na maseneta, wamepitisha hoja ambayo inasubiri Rais Uhuru kuiidhinisha na kuifanya sheria.
Ikiwa Rais ataidhinisha hoja hiyo, Raila atakumbana na vigingi vingi anapoelekea kortini. Jubilee imetumia wingi wake bungeni kupitisha sheria hizo mpya ikiwa na lengo la kuondoa vizuizi vinavyoweza kuhujumu ushindi wake wakati huu.
Mahakama ya Juu iliamuru uchaguzi wa Alhamisi ni kati ya Raila na Uhuru, lakini mgombea wa Nasa alipotangaza hatashiriki, Mahakama Kuu iliwakubalia wagombea wengine sita kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho.
No comments:
Post a Comment