Wednesday, October 25

Uhuru Kenyatta alivyoiva baada ya kuanguka kwenye urais 2002



Rais Uhuru Kenyatta
Rais Uhuru Kenyatta
Kitabu maarufu cha ‘Not Yet Uhuru’ kilichoandikwa na Jaramogi Oginga Odinga, baba mzazi wa Raila Odinga, mpinzani mkuu wa Uhuru Kenyatta katika mbio za urais nchini Kenya kinaweza kuwa na mantiki katika siasa zinazoendelea sasa nchini Kenya.
Katika kitabu hicho, Oginga Odinga anazungumzia mengi yakiwamo maisha yake binafsi na siasa za Kenya na vipi hakuridhishwa na hakubaliani na mazingira ya Kenya baada ya uhuru.
Wakati hiyo ndiyo iliyokuwa dhamira yake, leo hii ‘Not Yet Uhuru’ ikimaanisha “Uhuru Bado” inabaki kuwa hadithi nyingine ya Rais Uhuru Kenyatta na safari yake ya kisiasa hadi alipofika sasa.
Kenyatta aliyezaliwa, Oktoba 26, 1961, anajianda kusherehekea miaka 56 ya kuzaliwa kwake hapo kesho, sherehe ambayo bila shaka itaandamana na ushindi wa kiti cha urais baada ya mpinzani wake mkuu Raila Odinga kususia uchaguzi.
Kwa Uhuru Kenyatta safari ya kufika alipofika ilikuwa ndefu, dhana isiyo rasmi ya Not Yet Uhuru ilitawala harakati zake za kisiasa tangu alipoanza kuchomoza hadi leo hii akiwa Rais wa Kenya.
Mwaka 1997 akiwa ndio kwanza ana miaka 36, Uhuru alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama tawala cha wakati huo, Kanu katika tawi la kwao, Gatundu na baadaye akawania ubunge wa jimbo la Gatundu.
Uhuru alipewa nafasi kubwa kushinda jimbo hilo ambalo baba yake Mzee Jomo Kenyatta aliyekuwa rais wa Kenya aliwahi kuwa mbunge kabla ya kufariki dunia mwaka 1978.
Wakati Uhuru akiwania ubunge kwa tiketi ya Kanu, chama kilichokuwa maarufu wakati huo, aliangushwa na msanifu majengo, Moses Mwihia, mtu ambaye hakuwa maarufu yeye pamoja na chama chake cha Social Democratic.
Huo ulidhaniwa kuwa ndio mwisho wa Uhuru katika siasa za Kenya, ilidhaniwa angejikita kwenye biashara kwani ilikuwa aibu kuangushwa katika jimbo ambalo si baba yake tu hata ndugu yake wa karibu, Ngengi Muigai aliwahi kuliongoza.
Hata hivyo, ukweli ni kwamba anguko hilo ni kama lilimuinua Uhuru na jambo la kufurahisha ni kwamba nyuma yake alikuwapo Rais wa Kenya wa wakati huo, Daniel arap Moi ambaye ni dhahiri alimkubali Uhuru na hivyo haikushangaza alipoanza kumpaisha katika siasa za Kenya.
Alimuingiza bungeni mwaka 2001 na baada ya hapo akawa waziri wa Serikali za mitaa na mwaka 2002 akachaguliwa kuwa mbunge wa Jimbo la Gatundu.
Baada ya hapo Uhuru akachaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa kwanza wa Kanu, ushindi ambao ulikuwa kama sehemu ya harakati zake za kuanza safari ya kuisaka Ikulu ya Kenya.
Katika hali ya kushangaza Rais Moi akafanya uamuzi mgumu kwa kumteua kuwa mgombea urais wa Kenya katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2002 kwa tiketi ya Kanu.
Uamuzi huo uliwakera wanasiasa maarufu waliokuwa Kanu ambao waliungana na mgombea mwingine wa urais, Mwai Kibaki na kumbwaga Uhuru. Kibaki alishinda kwa asilimia 62 dhidi ya 30 za Uhuru.
Hilo lilikuwa anguko jingine la Uhuru baada ya lile la kwenye ubunge lakini anguko hili nalo lilikuwa funzo, wakati huo akiwa na miaka 41, Uhuru alikubali matokeo kwa ujasiri wa aina yake na hivyo kuonekana ni mfano kwa viongozi wachache wa Afrika kukubali kushindwa.
Uhuru akaahidi kurudi kukijenga chama chake cha Kanu ili kuhakikisha kinarudi madarakani katika uchaguzi wa mwaka 2007.
Nje ya siasa hizo, Moi aliutetea uteuzi wa Uhuru kuwa mgombea urais kwa tiketi ya Kanu akidai kwamba mwanasiasa huyo alikuwa chaguo sahihi katika kukabiliana na ukabila nchini Kenya.
Katika kipindi cha mwaka 2002 baada ya uchaguzi hadi mwaka 2007 kilichoonekana ni usahihi wa ile hadithi ya ‘Not Yet Uhuru’ kwa maana ya kwamba Uhuru hakuwa ameiva, hakutosha, muda wake ulikuwa bado haujafika.
Pengine kwa kuamini kwamba hajatosha au muda wake ulikuwa bado ndio maana alikubali haraka kushindwa na kujipanga upya kwa safari ya kuelekea Ikulu, safari ambayo ilianza kwa kuhakikisha anautwaa uongozi wa chama cha Kanu.
Katika kampeni za kuusaka uenyekiti wa Kanu katika uchaguzi wa mwaka 2005, Kenyatta alishirikiana na William Ruto, ambaye ndiye makamu wake wa rais, kwa pamoja waliendesha kampeni dhidi ya marehemu, Nicholas Biwott, mwanasiasa tajiri na mtu wa karibu wa Rais Moi ambaye pia aliutaka uenyekiti wa Kanu.
Uhuru alifanikiwa kumshinda Biwott ambaye licha ya kuupinga ushindi wa Uhuru, lakini wakati wote Uhuru alisema anamhitaji Biwott katika kuiimarisha Kanu na kuung’oa utawala wa Mwai Kibaki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007.
Ruto akiwa katibu mkuu wa Kanu, alishirikiana vizuri na Uhuru katika kuukosoa utawala wa Kibaki ambao wakati huo Raila alikuwa mmoja wa mawaziri akiongoza wizara ya ujenzi (barabara).
Katika kipindi hicho hicho likatokea tukio kubwa nchini Kenya la kampeni ya mabadiliko ya katiba, hiyo ikawa fursa nyingine ya Uhuru na Ruto kuonyesha msimamo wao katika kupinga katiba pendekezwa iliyokuwa ikipigiwa debe na utawala wa Kibaki.
Jambo la kufurahisha ni kwamba baadhi ya mawaziri wa Kibaki wakiongozwa na Raila walikuwa hawaiungi mkono Katiba hiyo, hivyo Uhuru akajikuta akiungana na Raila katika kampeni za kuipinga katiba hiyo huku wakizunguka nchi nzima.
Kampeni hizo zilihusisha alama za chungwa na ndizi, walioipinga Katiba ya Kibaki alama yao ilikuwa chungwa na walioiunga mkono alama yao ilikuwa ndizi, na hapo ndipo baadaye Chama cha ODM yaani Orange Democratic Movement kilipoibukia mmoja wa viongozi wake waandamizi akiwa ni Raila.
Kampeni za mabadiliko ya Katiba ya Kenya zilianza kuibua hisia kwamba katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2007, Uhuru na Raila wangekuwa kambi moja dhidi ya utawala wa Kibaki ambaye alimtimua Raila katika baraza lake la mawaziri kwa kosa la kuipinga Katiba aliyoitaka Kibaki lakini swali kubwa lilikuwa kati ya Uhuru na Raila nani angekuwa mgombea urais.
Hata hivyo, ilipofika 2007, Uhuru alijitoa katika mbio za urais akatangaza kumuunga mkono Kibaki akidai kwamba anataka kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2012 akiwa na uhakika wa kushinda, pengine pia aliamini muda wake bado au hakuwa ameiva.
Huo pia ukawa wakati mwingine wa kuachana na shwaiba wake wa kisiasa, William Ruto ambaye alitangaza kuwania urais kwa tiketi ya ODM lakini akaangushwa na Raila kwenye kura za maoni.
Pamoja na kuangushwa, Ruto alimuunga mkono Raila katika mbio za kumng’oa Kibaki katika uchaguzi wa mwaka 2007 uliotawaliwa na vurugu na kuwa chanzo cha kuundwa Serikali ya mseto huku Raila akiwa Waziri Mkuu.
Uhuru aliteuliwa kuwa waziri wa fedha na baadaye naibu waziri mkuu, hiyo ikawa kete nyingine ya kuelekea Ikulu, bajeti yake akiwa waziri wa fedha ilisifiwa na wakati wote akawa makini katika kujenga hoja katika matukio mbalimbali.
Huu ni wakati ambao katika kampeni na mikutano mingi ya kisiasa Uhuru alikuwa akisifiwa na wafuasi wake kwamba ameiva. Ile dhana isiyo rasmi ya Not Yet Uhuru ikaanza kutoweka, Uhuru akaanza kuonekana ameiva, anatosha, muda wake umefika.
Na hata katika baadhi ya mikutano, wafuasi wake walifikia hatua ya kumsifia kwa kuimba kwamba ‘Uhuru ameiva’.
Uhuru alikuwa makini lakini alijikuta akiingia matatani akituhumiwa kuhusika na mauaji na mateso ya Wakenya zaidi ya 1,000 katika ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.
Uhuru na mwenzake Ruto na wanasiasa wengine walishitakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), Uhuru alidaiwa kuandaa kundi maarufu la Mungiki lililoshiriki kuua na kutesa wananchi lakini wakati wote alikuwa makini kupinga kuhusika kwake katika mauaji.
Alisikika akisema kwamba anakwenda ICC kujisafisha na kuthibitisha kwamba mkono wake haukuhusika kwa vyovyote katika mauaji na mateso yaliyowakumba Wakenya.
Kesi hiyo pia ilitafsiriwa kuwa pigo jipya kwa Uhuru katika harakati zake za kuwania urais mwaka 2012, kwamba Wakenya wangekubali vipi kuwa na kiongozi tena Rais ambaye anashtakiwa kwa uhalifu kwenye mahakama ya kimataifa.
Hoja hiyo, lilitawala mdahalo wa mwisho wa wagombea urais lakini Uhuru alikuwa makini akidai nafasi anayoitaka ni ya kuchaguliwa na wananchi si ya uteuzi: “Nafasi ninayoitaka ni ya kuchaguliwa si kuteuliwa, ni jukumu la Wakenya kuamua na naamini wataniamini.”
Uhuru akaibuka mshindi na kudhihirisha kwamba huo ulikuwa wakati wake huko nyuma alikuwa hajaiva, licha ya Raila kumpinga mahakamani lakini mahakama ilimpa Uhuru ushindi.
Katika kuelekea uchaguzi wa kesho ambao ni wa marudio baada ya ule wa awali uliofanyika Agosti kufutwa na Mahakama ya Juu, Jumapili, Uhuru alifanya mahojiano na kituo kimoja cha televisheni, aliulizwa uhalali wa ushindi katika uchaguzi huo hasa baada ya baadhi ya Wakenya kutangaza kuususia.
Akijibu swali hilo alisema kinachoangaliwa hapo ni ofisa wa tume ya uchaguzi kuandaa mazingira ya watu kupiga kura kwa mujibu wa Katiba halafu akisema watu hawakushiriki, hiyo ni haki yao watu hao ya kidemokrasia kwa kuwa hata kukataa kupiga kura ni haki ya mtu.
Ama kuhusu kufanya mazungumzo na Raila, Uhuru alikuwa wazi kwamba atakuwa tayari kwa mazungumzo hayo baada ya uchaguzi huku akisema, piga kura kwanza baada ya hapo mazungumzo.
Uchaguzi wa kesho unakamilisha ngwe yake ya mwisho ya urais kwa maana ya muhula wa pili, ni uchaguzi ambao haunogi kwa kuwa mpinzani wake mkuu ameususia.
Pamoja na yote hayo kinachoonekana ni kwamba Uhuru ataingia Ikulu ikiwa ni safari yake ya mwisho kikatiba, safari aliyoipigania kwa muda mrefu huku akipanda na kushuka na kesho anaikamilisha kwa ushindi unaoambatana na sherehe ya siku yake ya kuzaliwa.   

No comments:

Post a Comment