Miongoni mwa mambo rasilimali zilizopo chini ya wizara hiyo ni wanyamapori na misitu zinazoelezwa kuwang’oa wengi walioingoza ama kwa kutokuwa makini kuzisimamia au kutozilinda ipasavyo.
Hata hivyo, waziri mpya wa wizara hiyo Dk Hamis Kigwangalla amesema ataendelea kuwapo ndani ya wizara hiyo kama kilichowafanya watangulizi wake kuondoka ni masilahi binafsi, kwa kuwa hahongeki, hashawishiki na aliyemteua analifahamu hilo.
Amewatahadharisha wadau akisema wanapofika ofisini kwake wajiandae vyema, vinginevyo anaweza kusimama na kumwacha mtu kama atagusa suala la rushwa.
“Mimi sihongeki, kwa hivyo siko tayari kung’oka kwa sababu yoyote ile, kama ni umaskini ni bora kufa njaa, kwangu fedha haiwezi kunitolea heshima licha ya kuwa wote tunazitaka,’’ alisema Kigwangalla.
“Sitakuwa tayari kupoteza heshima yangu, aliyeniteua anajua kuwa mimi ni mwarobaini wa hayo yote, hata nilipoteuliwa walianza kunidhihaki kupitia mitandao ya kijamii kuwa ninakwenda kuharibikiwa huko, eti kwa sababu mawaziri hawadumu, haipo hiyo.”
Dk Kigwangalla jana alisema hayo alipojibu kauli ya meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro aliyemtahadharisha kuwa mawaziri wamekuwa hawadumu ndani ya wizara hiyo kutokana na kununulika na wadau kwa kuwa kuna ushawishi mwingi.
Hayo yalitokea kwenye mkutano wa wadau wa sekta mbalimbali zinazofanya kazi na wizara hiyo ambao Dk Kigwangalla alikutana nao akiwa na naibu wake, Japhet Hasunga.
Katika mchango wake, Lazaro alisema, “Niliwahi kumtahadharisha waziri mwenzako (anamtaja jina)kuwa hatadumu katika wizara hiyo kutokana na wadau kuwa na vishawishi vingi, leo hii naomba kukuambia kuwa sheria hizo mnazosema kuwa ni mbovu si kweli, bali zinakosa usimamizi wa kutosha kwa sababu ya masilahi ya watu.”
Meya huyo alimtaka waziri kukutana na kila sekta ili kusikiliza kilio chao akisema kuwa ndani ya wizara hiyo kama atapatikana mtu wa kuisimamia vizuri inaweza kutoa mchango mkubwa ambao haujapata kutokea, lakini akaahidi kuwa watamsaidia ili adumu kuliko mawaziri wengine.
“Napenda uendelee kubaki katika wizara hii, wewe ni kijana mdogo nisingependa uwe geti la kutokea, hivyo napendelea uendelee kuwapo,” alisema Lazaro.
Meya huyo alisema baadhi ya mawaziri wamekuwa wakiitwa na makundi mbalimbali akitoa mfano wa wawindaji na kuzungumza nao lakini hushawishika kuegemea huko na wakiitwa na watu wengine huegemea huko, hivyo kushindwa kubaki katikati ya sekta zote.
Akijibu hoja hiyo, Dk Kigwangalla alisema hana shaka yoyote kuhusu kupewa wizara hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga aliyeteuliwa kushika wadhifa huo akitokea Idara ya Mambo ya Kale alisema sheria za sekta nyingi ni nzuri, lakini kinachokwamisha ni siasa kuingizwa katika masuala ya utendaji.
Dk Kigwangalla aliteuliwa kushika wadhifa huo akitokea kuwa naibu waziri wa afya ambapo amemridhi Profesa Jumanne Maghembe.
No comments:
Post a Comment