Hivyo, Watanzania wamehimizwa kufuga nyuki kwa wingi ili kukuza uchumi kwa kutumia fursa ya upatikanaji asali na nta.
Rais wa chama cha ushirika cha vijana wajasiriamali na wataalamu wa masuala ya nyuki, Philemon Kiemi alisema bidhaa zipatikanazo kutokana na nyuki zimekuwa zikiuzwa kwa bei ya kuanzia Sh500,000 kwa kilo.
Mtaalamu huyo alisema ushirika huo una hekta 4,000 zilizopo katika Kijiji cha Kisaki mkoani Singida na zinatumika kwa ufugaji wa nyuki sambamba na kuwa kituo cha mafunzo kwa vitendo.
“Bidhaa zinazotokana na ufugaji wa nyuki bei zake ni kubwa lakini zimekuwa hazitambuliki, hivyo zinatakiwa kupewa umuhimu wa kutangazwa na Serikali inaweza kuingizia mapato zaidi na kukuza uchumi,” alisema Kiemi.
Kuhusu dhana kuwa baadhi ya mikoa imeathiriwa na kemikali za sumu aina ya nikotini kutokana na kilimo cha tumbaku, Kiemi ambaye ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (Sua), alisema ni vigumu kwa nyuki kufyonza sumu kujitengenezea chakula ambacho ni asali.
Naye Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk Rehema Nchimbi alisema kumekuwa na tatizo la uchomaji mkaa kwa baadhi ya maeneo lakini kwa sasa kuna ushirikiano wa wananchi na Serikali.
Dk Nchimbi aliwataka wachomaji mkaa kuachana na kazi hiyo, badala yake kufuga nyuki ambao watakuwa na faida kubwa kwao na inaweza kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja, mkoa huo na Taifa.
“Nawasihi wananchi kuacha kukata miti ovyo kwa shughuli za uchomaji mkaa, badala yake wageukie ufugaji wa nyuki,” alisema.
Alisema wachomaji wengi wa mkaa wamekuwa na maisha duni kutokana na biashara hiyo kukosa mwelekeo na faida.
No comments:
Post a Comment