Thursday, October 12

Dawati la ulinzi kuhudumia mimba shuleni

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jinsia, Watoto na
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jinsia, Watoto na Wazee, Ummy Mwalimu  
Tarime. Baada ya polisi kuanzisha dawati la jinsia na kuonyesha mafanikio, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jinsia, Watoto na Wazee, Ummy Mwalimu ametoa miezi sita kwa shule zote nchini kuanzisha madawati ya ulinzi na usalama ili kuzuia mimba za utotoni.
Waziri Ummy alitoa agizo hilo wakati wa maadhimisho ya kimataifa ya siku ya mtoto wa kike duniani jana, yaliyofanyika kitaifa Uwanja wa TCC wilayani Tarime.
Alisema ana imani ndani ya miezi hiyo mchakato huo utakamilika ili kuwaokoa watoto wa kike waliopo maeneo mbalimbali, kuondokana na mimba za utotoni na hatimaye kuendelea na masomo na kutimiza ndoto zao.
“Mimba za utotoni ni tatizo katika mikoa mbalimbali, madawati haya yatasaidia kufanikisha kuzuia kwa kuwa yatapokea matatizo yanayowakabili hasa kutoka kwa wazazi na mazingira yanayowazunguka kisha kufanyiwa kazi,’’ alisema.
Waziri huyo aliwataka wadau mbalimbali kuisadia Serikali katika mchakato wa kutokomeza mimba za utotoni na ndoa ili kufanikisha azma ya Tanzania ya viwanda.
Wakati huohuo, WaziriUmmy aliwaagiza wakuu wa shule za msingi na sekondari kutoa taarifa kwa kamishna wa elimu kila baada ya miezi mitatu kuhusu watoto wa kike wanaopata mimba, au kuolewa wakiwa shuleni.
“Takwimu hizi tutazichapisha na tutakuwa tukizitoa kila baada ya miezi mitano ili kujua mkoa, halmashauri na shule zenye watoto wa kike walioacha masomo kwa sababu ya mimba na ndoa za utotoni,” alisema.
Naye Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef) nchini, Maniza Zaman aliipongeza Serikali kwa kuona umuhimu wa kuanzisha siku hiyo kwa kutumia kauli mbiu ya ‘Tokomeza Mimba za Utotoni Tufikie Uchumi wa Viwanda’.
“Leo napenda kusisitiza umuhimu wa mtoto wa kike katika kuifanya Tanzania iwe imara na yenye maendeleo ya kiuchumi, umri wa kupevuka ni kipindi muhimu cha kuelekea katika utu uzima,” alisema Zaman na kuongeza:
“Watoto wa kike wakiandaliwa na kuvuka kipindi hicho kwa usalama, wana fursa ya kuchangia maendeleo ya taifa.”
Awali, Mwakilishi wa Shirika la Plan International, Martha Lazaro alisema wataendelea kuiunga mkono Serikali katika kuhakikisha vikwazo vinavyowakabili watoto wa kike vinakwisha.
Naye Mkurugenzi wa kupambana na kutokomeza ukeketaji, Sista Stella Mgaya alisema kwamba mangariba 63 wa wilaya hiyo wameacha kazi hiyo, badala yake wamejiunga na ujasiriamali.     

No comments:

Post a Comment