Mpango huo umebainishwa mwishoni mwa wiki wakati taasisi hizo zilipokuwa zinaadhimisha wiki ya huduma kwa mteja. Pamoja na mambo mengine, CRDB iliahidi kuongeza ofisi za posta zinazotoa huduma za fedha za kibenki.
Ofisa Mwandamizi wa Fahari Huduma ya CRDB, Nonat Mushi ushirikiano wa benki hiyo na TPC ulianza tangu mwaka 2012 na mpaka sasa matawi 77 yanatoa huduma za CRDB.
“Mpaka Januari mwakani, tunatarajia kuongeza matawi ya TPC yanayotoa huduma zetu yafike 100,” alisema Mushi.
Pamoja na mpango huo, CRDB yenye zaidi ya mawakala 3,800 ambao wanapaswa kuwa ndani ya kilomita 100 kutoka lilipo tawi la benki hiyo, imesema inatarajia kuimarisha mtandao huo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dk Charles Kimei alisema ushirikiano wa taasisi hizo mbili utakua na manufaa kwa wananchi katika vita dhidi ya umaskini. “TPC bado ni wakala wetu mkubwa nchini,” alisema Dk Kimei.
Dk Kimei alioyasema hayo akiwa pamoja na Kaimu Postamasta Mkuu, Deo Kwiyukwa walipokuwa wakiadhimisha wiki ya huduma kwa mteja jijini hapa.
Kwiyukwa aliishukuru CRDB kwa kushirikiana nao kwenye maadhimisho hayo na kubainisha kwamba uhusiano wao utakuwa na manufaa mengi kwa wateja wanaowahudumia kukuza kipato chao na taifa kwa ujumla.
“Tutaendele akuboresha huduma zetu ili kuwavutia wateja wengi zaidi,” alisema Kwiyukwa.
CRDB ni miongoni mwa benki tatu kubwa zaidi nchini kwa amana, ukubwa wa mtaji na wateja inayowahudumia. Ndani ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwake imekuwa ya kwanza kuwa na tawi nje ya nchi huku ikpata tuzo za kimataifa ikiwamo ya huduma bora kwa wateja pamoja na ubunifu kwa wateja wadogo.
Kukiwa na zaidi ya benki 50 nchini na kampuni saba za mawasiliano, ripoti ya Mfuko wa Kuendeleza Huduma za Fedha (FSDT) inaonyesha matumizi ya huduma hizo yameongezeka kwa asilimia 6.5 mwaka 2013 mpaka asilimia 65 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment