Dar es Salaam. Siku mbili kabla Taifa halijaadhimisha kumbukumbu ya miaka 18 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere msaidizi wa karibu ameutaja utawala bora kuwa ndiyo unaoweza kuisaidia nchi katika uchumi wa viwanda.
Msaidizi huyo wa Mwalimu, Joseph Butiku ambaye kwa sasa ni mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere alisema hayo katika kongamano la kumbukizi ya Mwalimu Nyerere lililofanyika katika Chuo cha Kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere, Kivukoni jijini Dar es Salaam jana.
Alisema Afrika ina viongozi wengi ambao hawajaendelea akimaanisha kuwa mtu hawezi kuendelea kama hana elimu itakayomsaidia kupambanua vizuri mambo mbalimbali.
Butiku aliongeza kuwa, “ukiona nchi ina viwanda vingi na vijana wapo ujue hiyo nchi ina watu walioendelea.”
Butiku aliwahi kufanya kazi kwa karibu na Mwalimu Nyerere akiwa ni msaidizi wake katika masuala mbalimbali.
Kwa upande wake, spika mstaafu wa Tanzania, Anne Makinda alisema wakati wa utawala wa Mwalimu mojawapo kati ya sera alizotaka ni asilimia 60 ya pamba iliyolimwa nchini iwe inafanyiwa usindikaji nchini na kutokana na hilo viwanda mbalimbali vilianzishwa ikiwa ni sehemu ya maono yake.
Msajili wa Hazina, Oswald Mashindano ambaye alitoa mada iliyoelezea maana ya nchi yenye uchumi wa kati kuwa ni ile iliyofikia kiwango cha juu cha kutumia rasilimali watu ambao kipato cha chini kwa mtu mmoja ni kati ya Dola 2,500 za Marekani (sawa na Sh5,613,000) hadi Dola 3,000 (Sh 6,735,600).
Naibu Waziri wa Elimu, William Ole Nasha alisema maono ya Mwalimu Nyerere yaliwekeza nguvu katika kuimarisha viwanda vilivyopo nchini kwa kuwa ndiyo njia pekee ambayo nchi inaweza kujinasua kiuchumi na kuepukana na kutegemea uingizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
“Viwanda tunavyovihitaji kwa sasa ni vile vinavyotumia malighafi kutoka nchini zinazotokana na shughuli wanazozifanya Watanzania,” alisema.
No comments:
Post a Comment