Baadhi wa watafiti wa magonjwa yanayotoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu kutoka nchi za Afrika wakiwa katika mkutano wa kujadili mbinu mbalimbali za kuweza kuzuia magonjwa hayo mkutano unaendelea jijini Arusha.
Utafiti wa wataalamu unaonyesha asilimia kati ya nne na 30 ya wanyama hao wana magonjwa yanayoambukiza kwa binadamu, miongoni mwa hayo ukiwemo brusela unaofahamika kitaalamu Brucellosis.
Mkurugenzi wa shirika lisilokuwa la kiserikali linalojishughulisha na utafiti la Afrique One Aspire, Bassirou Bonfoh amesema magonjwa ya wanyama yanayoambukiza binadamu yana athari kubwa kwa afya na uchumi.
Amesema ugonjwa wa brusela unatokana na matumizi ya mazao ya wanyama na husababisha waliougua kupata homa za vipindi.
Rudovick Kazwala ambaye ni mtafiti kiongozi wa mradi wa kufuatilia magonjwa yanayotoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu katika shirika hilo, amesema brusela unashika nafasi ya sita kati ya maradhi 36 yanayotoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.
Kutokana na hilo amesema wanakusudia kufanya utafiti kuangalia ni aina gani ya bakteria anayeathiri binadamu.
Amesema wanaendelea kutafiti juu ya ugonjwa huo ambao wanyama wanaofugwa mijini asilimia 30 wanasumbuliwa na brusela na vijijini ambako mifugo hutembea umbali mrefu ni asilimia nne ya mifugo yenye tatizo hilo.
Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua), Coletha Mathew amesema brusela ni ugonjwa unaotokana na kutumia maziwa au nyama yenye bakteria wa ugonjwa huo, hivyo alishauri jamii kupima nyama kabla ya kuitumia kwa chakula.
Rosamystica Sambu, mtafiti mwingine kutoka Sua amesema uwindaji haramu pia unachangia kusababisha kuenea kwa magonjwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu ikiwemo ugonjwa huo.
“Mwingiliano wa wanyamapori na wanyama wa kawaida pia unaweza kusababisha hatari ya wanyama kupata ugonjwa huo ambao husababisha wanyama kuharibu mimba jambo ambalo linawaumiza wafugaji,” amesema.
Amesema ni vyema wafugaji wakajiepusha kuchanganya mifugo na wanyamapori.
No comments:
Post a Comment