Thursday, September 21

Askofu Chimeledya anena vifo vya Watanzania 13



Dodoma.  Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania, Jacob Chimeledya amesema vifo vya watu 13 vilivyotokea nchini Uganda viwe fundisho kwa waliobaki duniani kutenda mema.
Dk Chimeledya ambaye ni Askofu wa Dayosisi ya Mpwapwa amesema hakuna haja ya kulalamika kuhusu vifo hivyo.
Amesema hayo leo Alhamisi wakati wa ibada ya mazishi ya watu sita kati ya hao 13 ambao ni ndugu wa naibu waziri na mbunge wa zamani wa Mpwapwa, Gregory Teu katika Kanisa la Angalikana la Watakatifu Wote wilayani Mpwapwa.
Dk Chimeledya amesema msiba huo ni mpango wa Mungu ambao unalenga kuwaimarisha waliobaki dunia kuishi maisha yanayompendeza yeye.
"Hakuna haja ya kusema huyu aliyeolewa kule ndiye amesababisha haya yote yatokee au huyu aliyeoa Tanzania ndiye amesababisha haya yote yatokee. Waliotwaliwa, wametwaliwa tuliobakia tutengeneze maisha yetu. Msiba huu utuwezeshe kuyatenda yaliyo mema," amesema Dk Chimeledya.
Amesema, "Kwa sababu hatujui saa tutakapotwaliwa na bwana, yote haya tumuachie Mungu ni mpango wake anataka kutuimarisha katika maisha yetu duniani kwa kufanya yaliyo mema."
Amewaasa kukesha kila wakati kwa kutengeneza maisha katika kila eneo mtu alipo kwa kufanya yaliyo makusudi ya Mungu.
"Kama ni kwenye biashara yako ukeshe kwa kufanya yaliyo mema, kama ni uongozi ufanye yaliyo kusudi la Mungu, kama ni kiongozi wa dini uwaongoze vizuri waumini ili waweze kuyafanya yaliyo mema," amesema.
Amesema hakuna haja ya kufikiri kuwa tukio hilo lina mkono wa mtu, bali Mungu ameruhusu litokee kwa kuwa ana sababu nalo ambayo ni ushindi katika maisha ya watu wote.
Amewataka waumini kutafakari msiba huo kama fumbo ambalo halihitaji kutafakariwa pasipo Mungu.
"Tunatakiwa kuangalia kama Ayubu  alipopata madonda na mateso yote hayo bado hakumuacha Mungu. Mungu alitupa kwa hiyo amechukua, kuna kupigwa na kuanguka tujiimarishe," amesema.
Miili ya marehemu Paulina Ndagala; Ester, Rehema, Sakazi, George na Alfred Teu iliwasili jana Jumatano saa nne usiku wilayani Mpwapwa ikitokea Dar es Salaam.
Kabla ya kupelekwa kanisani, miili hiyo iliyolala nyumbani kwa Teu iliagwa na ndugu, jamaa na marafiki. Baada ya ibada, maziko yatafanyika katika makaburi ya Vinghawe mjini Mpwapwa.
Baadhi ya waliohudhuria ibada hiyo ni Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye ni mbunge wa Kongwa na George Simbachawene wa Kibakwe.
Wengine ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na watu wenye Ulemavu), Anthony Mavunde na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Suzan Kolimba.

No comments:

Post a Comment