Wito huo umekuja takriban siku kumi baada ya Serikali kutangaza kuvirejesha viwanda nane ambavyo vilikuwa havifanyi kazi na kuonya wamiliki wa viwanda vingine vinane kuviendeleza ifikapo Agosti 22 na wasipofanya hivyo wavirejeshe serikalini.
Uamuzi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali kufufua viwanda vya umma ambavyo vilibinafsishwa lakini havifanyi kazi.
Tangazo la Msajili wa Hazina, Dk Oswald Mashindano lililochapishwa na vyombo vya habari jana linavitaja viwanda hivyo kuwa ni Sabuni Industries Limited, ambacho kilikuwa moja ya viwanda vitano vilivyopewa onyo Agosti 11 na Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage.
Vingine ni Ushirikiano Wood Product, Morogoro Shoe Limited, Tanzania Sewing Thread na Aminal Feeds Ltd.
Pia katika orodha hiyo kuna kiwanda cha Tanzania Germstone Industries, Kiltex-Dar, Northern Cremeries Ltd- Dar es Salaam na Tanzania Packaging Manufactures Ltd.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, wamiliki hao wametakiwa kuripoti ukumbi wa Wizari ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji mjini Dodoma.
Akizungumza na Mwananchi kuhusu viwanda hivyo, Dk Mashindano alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya mkakati wa kufufua viwanda nchini.
Dk Mashindano alisema baada ya kupata agizo la Serikali, ofisi yake imevigawa viwanda hivyo vilivyoshindwa kufanya kazi katika makundi mbalimbali.
Alisema kundi la kwanza linahusisha viwanda vyote vilivyoshindwa kuzalisha na baada ya kukutana na wamiliki wake jijini Dar es Salaam, Serikali iliamua kuvitwaa vinane baada ya kubainika kukiuka mikataba ya mauzo.
Uamuzi huo ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli alilotoa Agosti 7 mkoani Tanga akimtaka Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kunyang’anya viwanda ambavyo havifanya kazia baada ya kubinafsishwa.
Baada ya kauli hiyo, Agosti 11 Waziri Mwijage aliwaambia wanahabari mjini Dodoma kwamba Serikali imeanza utaratibu wa kuvitwaa viwanda hivyo baada ya mikataba ya mauzo kuchambuliwa.
Viwanda, ambavyo Waziri Mwijage alitangaza kuvirejesha serikalini ni Lindi Cashewnuts, Pugu Kaolin Mines, Mkata Saw Mills, Manawa Ginnery, Dabada Tea factory, Tembo Chipboards, Kilimanjaro Textiles Mills na Mang’ula Mechanical and Machines Tools.
Hata hivyo, Mwijage aliwaambia waandishi siku hiyo kuwa viwanda hivyo vitaendelea kuwa chini ya ulinzi wa wamiliki hao hadi Serikali itakapovichukua.
Jana, Msajili wa Hazina alisema baada ya awamu ya kwanza kukamilika, leo ofisi yake inaanza awamu ya pili ambayo ni kuonana na wawekezaji hao wakiwa na nyaraka zao zote.
“Hii inatokana na ukweli kwamba baada ya kuuziwa, hawa mabwana nao waliviuza na hata waliowauzia nao waliuza tena bila kufuata utaratibu,” alisema.
“Inafika mahali sasa hujui mmiliki halali ni nani hasa, ndiyo maana tukaamua kuwaita ili watupe ufafanuzi.”
Alisema baada ya kukutana nao ofisi yake itateua timu ya wakaguzi kwa ajili ya kufanya tathimini ya hali halisi ya viwanda hivyo kwa sasa.
“Tutapaleka timu ya watu wetu waende kukagua na kutuandalia ripoti nini wameona lakini pia itatupa mapendekezo yao,” alisema.
Alisema baada ya ripoti hiyo kukamilika ofisi yake itachukua uamuzi.
Mabadiliko ya kiuchumi
Viwanda vingi vya umma vilibinafsishwa wakati Serikali ikitekeleza mpango wa mabadiliko ya kiuchumi kwa kujiondoa katika uzalishaji na kubakia na kazi ya uratibu na usimamizi, ikiwa ni moja ya masharti ya taasisi za kimataifa za fedha wa kurekebisha uchumi.
Awali, Tanzania ilikataa kukubaliana na masharti hayo, ikitekeleza siasa ya ujamaa na kujitegemea ambayo ilihusisha Serikali kumiliki njia kuu za uchumi.
Hata hivyo, mabadiliko yaliyotokea katika nchi za Ulaya mashariki miaka ya themanini yaliambukizwa duniani kote, hasa katika nchi changa na zilizokuwa zinafuata siasa za ujamaa.
Utekelezaji wa sera ya ubinafsishaji ulianza kwa kusuasua mwishoni mwa miaka ya themanini, ukapamba moto miaka ya tisini, lakini ni viwanda vichache vilihimili ushindani wa bidhaa kutoka nje.
Akitoa mchanganuo wa hali ya viwanda nchini, Mwijage alisema vinavyofanya kazi vizuri ni 62, vinavyofanya kazi kwa kusuasua ni 28, vilivyofungwa ni 56 na vilivyobinafsishwa kwa kuuza mali mojamoja ni kumi.
Pia, Mwijage alisema wamiliki wa viwanda 14 wameonyesha utayari wa kuvifufua.
No comments:
Post a Comment