Wednesday, August 23

Tanroads yabomoa nyumba zilizowekewa kinga ya Mahakama


Mkazi wa Kimara Bakery, Nicomed Leo akiondoa

Mkazi wa Kimara Bakery, Nicomed Leo akiondoa mabaki ya mbao katika nyumba yake baada ya tingatinga la Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuibomoa licha ya kuwepo kwa zuio la Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi jijini Dar es Salaam jana. Picha na Ericky Boniphace 
Dar es Salaam. Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), jana ulibomoa nyumba tatu zilizopo Kimara Stop Over, jijini hapa ambazo ni kati ya 286 zilizowekewa kinga ya muda na Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi.
Hiyo ni sehemu ya operesheni ya kubomoa nyumba zaidi ya 1,300 zilizo ndani ya hifadhi ya Barabara ya Morogoro kuanzia Kimara hadi Kiluvya.
Wakati kazi ya kubomoa nyumba hizo ikiendelea, diwani wa zamani wa Saranga, Ephrahim Kinyafu alisema kinga ya muda kuzuia nyumba kubomolewa ilitolewa Agosti 18 baada ya wananchi 286 kwenda mahakamani na kwamba wamesikitishwa kuona zinabomolewa licha ya hati ya kuzuia kutolewa.
“Kwa uamuzi huu uliofanywa na Tanroads wa kubomoa hizi nyumba kwa kukaidi agizo la mahakama, tunajiuliza huu ndiyo utawala bora?” alihoji.
Kinyafu alisema walikwenda mahakamani kwa kuwa ndicho chombo chenye mamlaka ya kusimamia sheria.
Mbunge wa Kibamba, John Mnyika alisema uamuzi huo ni kinyume cha sheria na ameitaka Mahakama kuingilia kati na kuchukua hatua dhidi ya Tanroads.
Mhandisi wa wakala huyo Kimara, Johnson Rutechura alisema, “Hatuna taarifa juu ya nyumba ambazo zina kinga.”
Msimamizi huyo wa bomoabomoa alisema hawakupewa barua yoyote kutoka mahakamani hivyo hawatambui kama kuna nyumba zenye zuio.
Waliobomolewa
Kati ya nyumba hizo tatu, moja ni ya Nicomed Leo (61). Mbali ya nyumba hiyo, mzee huyo alikuwa na nyumba nne, mbili zikiwa za kawaida na nyingine za ghorofa. Iliyobomolewa na Tanroads ni ya kawaida iliyokuwa karibu zaidi na barabara.
“Nilikuwa na kinga ya mahakama, niliibandika getini lakini nashangaa wamebomoa hapa haki iko wapi,” alisema na kuongeza kuwa baada ya kupata kinga, aliamini atakuwa salama lakini alishangaa jana asubuhi kuona akipigiwa simu kwamba nyumba yake inabomolewa.
“Nilijua wananitania, lakini nilipofika hapa nikakuta kweli wanabomoa na nilibandika karatasi za kinga getini na ukuta wa nyumba,” alisema.
Kutokana na tukio hilo, Leo, ambaye baada ya nyumba zake kuwekewa alama ya X alihojiwa na waandishi wetu na kusema “Nimeshajiandaa kisaikolojia hata wakija kubomoa mimi nitajenga kibanda hapahapa maana sina pakwenda,” jana alisema amekosa amani na hana imani tena hivyo ameamua kubomoa mwenyewe.
“Wanataka kuniua kabla ya wakati,” alisema huku akitetemeka na jasho likimtiririka usoni. Mzee huyo ambaye katika mahojiano ya awali alisema nyumba zake zilikuwa na thamani ya Sh900 milioni hakuwa na hamu ya kuzungumza na wanahabari kwani walipojaribu kumhoji aliwaambia kwa kifupi, “Mtanisaidia nini hata nikisema zaidi ni kama nachochea tu nyumba yangu kubomolewa naomba mniache.”
Ijumaa iliyopita, Leo alizirai baada ya kushuhudia nyumba ya jirani yake ikibomolewa. Inaelezwa kwamba alijaribu bila mafanikio kuwaomba maofisa wa Tanroads wasibomoe nyumba yake lakini ilishindikana ndipo alipoanguka. Kuona hivyo, maofisa hao waliahirisha kubomoa nyumba hiyo lakini wakiahidi kurejea jana.
Mwingine aliyebomolewa nyumba yake huku kukiwa na zuio la Mahakama ni Aisha Juma ambaye alisema walichokifanya ni kuokoa vitu vichache vya ndani.
Aisha alisema wanachosubiri sasa ni kusikia mahakama itasemaje tena baada ya tukio hilo.

No comments:

Post a Comment