Arusha. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amezikabidhi familia tatu za watoto walionusurika katika ajali ya Lucky Vincent Sh23.2 milioni zilizokusanywa kwa ajili ya rambirambi baada ya ajali hiyo iliyotokea Mei 6, mwaka huu wilayani Karatu kuua wanafunzi 32, walimu wawili na dereva.
Akizungumza ofisini kwake jana na familia hizo, Gambo alisema Serikali na wadau wamechangia fedha ambazo zilitumika katika shughuli nzima za mazishi ya marehemu hao na kiasi kilichobaki zinakabidhiwa kwa familia hizo ili kiwasaidie.
Hata hivyo, wakati Gambo akisema hayo baada ya kutoa fedha hizo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira ambaye alimwakilisha Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kuwapokea wanafunzi hao waliporejea kutoka kwenye matibabu huko Marekani Agosti 18, aliagiza Serikali ya Mkoa wa Arusha kutoa Sh20 milioni ambazo ni sehemu ya michango hiyo kuchangia mfuko wa elimu wa Stemm.
Lakini jana Gambo alisema, “Kimsingi napenda kumshukuru Mungu kwa kuwasaidia watoto wetu hawa na wadau wengine waliowezesha kupata matibabu nchini Marekani na wamerudi salama, katika fedha tulizokusanya tumeamua kila familia kati ya hizi tatu tuzikabidhi Sh7,750,000 kwa ajili ya matumizi yao.”
Alipoulizwa kuhusu kuwapa wahusika fedha hizo moja kwa moja ilhali maagizo ya Makamu wa Rais yalitaka zielekezwe kwenye mfuko wa elimu unaolenga kuwasaidia alisema Serikali huwa inafanya kazi kwa maandishi na ofisi yake haikuwa imepokea maagizo yoyote. Alisisitiza kuwa uamuzi wa kuwakabidhi umeridhiwa na uongozi wa mkoa huo.
Alisema yeye ndiye aliyemuomba Mghwira akawapokee watoto hao kwa kuwa alikuwa nje ya Arusha kwa majukumu mengine. Alipoulizwa kuhusu hotuba aliyoisoma kama ilikuwa ya Makamu wa Rais au mkuu wa mkoa mwenzake alisema mwenye majibu sahihi ni Mghwira.
Hata hivyo, Mghwira alipotafutwa jana kufafanua utata huo alijibu kuwa alikuwa kwenye kikao muhimu.
Baada ya kukabidhiwa fedha hizo, wazazi wa Doreen Mshana, Wilson Tarimo na Sadia Awadh walizishukuru serikali za Tanzania na Marekani taasisi za Stemm, Samaritan’s Purse na wadau wengine waliofanikisha matibabu ya watoto wao.
“Sisi wazazi tunawashukuru sana kwa msaada mkubwa mliotufanyia na kuwawezesha watoto wetu kupata matibabu. Mungu awabariki sana kwa sababu sisi wenyewe tusingeweza,” alisema mmoja wa wazazi hao, Neema Matemba.
Mitihani ya darasa la saba
Mzazi wa Doreen, Elibariki Mshana alimwomba Gambo aiingilie kati suala la watoto wao kufanya mitihani kwani dalili zinaonyesha kuwa uongozi wa shule hauko tayari kuwaruhusu kutahiniwa kutokana na kutokuwapo darasani kwa muda mrefu.
“Wazazi na wanafunzi wetu tupo tayari ili wafanye mitihani mwezi ujao lakini naona kama uongozi wa shule unasita kuwaruhusu, tusingependa warudie mwaka tunaamini watafanya vizuri mitihani yao tusiwekewe kikwazo,” alisema Mshana.
Gambo alisema iwapo wanafunzi hao wapo tayari kufanya mitihani yao na wazazi wameridhia haoni sababu ya kuzuiwa na kumwagiza ofisa elimu wa mkoa kufuatilia suala hilo na kulipatia majibu mapema.
No comments:
Post a Comment