Monday, August 21

Mstaafu aliyejitoa kuikabili saratani nchini




“Ujuzi hauzeeki” hii ni miongoni mwa methali yenye maneno ambayo yanaishi yakithibitishwa na Daktari Dominista Kombe ambaye ni bingwa wa magonjwa ya saratani .Licha ya kustaafu kwenye Hospitali ya Ocean Road ameamua kuendelea kutoa huduma hiyo kwa kuanzisha kituo cha Afyachek.
Dk Kombe anasema amefanya kazi katika Hospitali ya Oceam Road tangu mwaka 1995 na kustaafu mwaka jana, lakini alijisikia kuendelea kutoa huduma ya utatibu kwa magonjwa ya saratani.
“Nimestaafu kutumika kwenye hospitali ya Ocean Road, lakini nimeona bado nina nguvu ya kuendelea kutumia ujuzi wangu huu kutoa huduma hii, naamini kwamba kwa huduma yangu hii ninayoifanya kwa kumtegemea Mungu ananitumia kuokoa au kuongeza siku za maisha ya watu ninaowahudumia,” anasema.
Dk Kombe ambaye pia ni mjane anabainisha kuwa pamoja na kustaafu aliona haja ya kuendelea kuutumia ujuzi wake ili kuwaokoa wagonjwa wa saratani.
Saratani ipi?
“Kuna saratani ya matiti hii inawapata watu wa jinsi zote maana wapo ambao wanaamini kwamba hiyo ni kwa wanawake tu kumbe hata wanaume wanashambuliwa, ndiyo maana tunasisitiza kupimwa afya badala ya kusubiri kuugua,” anasema.
Anaisitiza: ” Hakuna sababu maalumu inayosababisha saratani ila kuna visababishi hatari ambavyo watafiti wamekuwa wakijaribu kuangalia uwezekano.
Anasema pia wapo vijana ambao wamepata saratani kutokana na mitindo yao ya maisha, ikiwamo kuwa na uhusiano wa ngono ikiwemo ya jinsia moja.
“Watu wanaofanya ngono kwa mdomo wapo kwenye hatari ya kupatwa na saratani kutokana na bakteria wanaotoka kwenye majimaji kutoka sehemu za siri, ambayo pia yanawezwa kupofusha macho.
“Ni kwa sababu kanuni zinazuia kuonyesha video za baadhi yao wanavyoteseka kwa maumivu na wanaeleza jinsi walivyoponwa kwa kuiga mambo yasiyofaa,”anasema.
Dk. Kombe anabainisha kuwa hata hivyo kuna sababu ambazo zinaweza kuzuilika ikiwamo kupata mtoto katika umri wa miaka 30, kutumia dawa za vichochezi vya kike (HRT) unene uliokithiri, kufanya mazoezi, kuepuka matumizi ya sigara, pombe kali, samli mgando wa wanyama.
Anawashauri wazazi kuwa makini na vyakula wanavyokula wanafamilia hasa kuku wa kisasa ambao kutokana na vyakula wanavyolishwa nyama yake ina vichocheo vinavyosababisha watoto kupevuka wakiwa na umri mdogo, hivyo kuwa kwenye hatari ya kupata saratani.
Anasema ni vyema wazazi wakahakikisha familia inakula mlo bora ulio na mboga za majani na matunda kwa wingi.
“Usilie makapi, wengi wanapenda kukoboa mahindi na kula ugali wa sembe lakini dona ndiyo unga mzuri wenye virutubisho, lakini ni vyema kuwa na utaratibu wa kupima afya kwa ujumla hasa kwa watu wenye umri wa miaka 45 na kuendelea saratani inashambulia zaidi,”anasema Dk Kombe
“Kupima kabla ya kuugua ni kuepuka gharama ambazo hutokea wakati wa kugharamia matibabu kwa kuwa ugonjwa huu ukifikia hatua ya kuanza kuugua inamaana tayari umekuwa kwa kiwango kikubwa,” anasema,” Dk Kombe.
Anasema hadi sasa anakadiria kuwa amehudumia wagonjwa 300 kwenye kituo chake hicho, ambapo wengi wao ni wanawake, ingawa pia anatambua kuwa kuna changamoto ya gharama za vipimo ambayo hata hivyo ni nafuu kuliko ile ya matibabu.

No comments:

Post a Comment