Monday, August 21

MEYA MANISPAA YA DODOMA ATOA RAI KUBORESHA MAONESHO YA WAKULIMA NA WAFUGAJI MAARUFU NANENANE


Meya wa Manispaa ya Dodoma Mstahiki Profesa Davis Mwamfupe (wa kwanza kulia) akishuhudia mmoja ya banda la maonesho alipotembelea Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kati katika Viwanja vya Nzuguni Manispaa ya Dodoma hivi karibuni.

Na Ramadhani Juma, Dodoma

HALMASHAURI za Manispaa na Wilaya katika mikoa ya Kanda ya Kati unayoundwa na mikoa ya Dodoma na Singida kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanaounga mkono shughuli za kilimo, mifugo na uvuvi wameshauriwa kubuni njia rahisi inayoweza kuwafikishia kwa wakulima na wafugaji elimu inayopatikana kwenye viwanja vya Maonesho ya Wakulima maarufu kama Nanenane.

Rai hiyo imetolewa na Meya wa Manispaa ya Dodoma Mstahiki Profesa Davis Mwamfupe kufuatia maenesho ya Nanenane yaliyomalizika hivi karibuni katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo amesema bado Maonesho hayo hususan Kanda ya Kati hayajafanikiwa kuwasaidia wakulima, wafugaji na wavuvi wetu kwa kiasi kinachoridhisha na kuwawezesha kubadili shughuli zao na kuzifanya kuwa na tija inayoridhisha.

Alisema Maonesho ya Nane Nane yamekuwepo kwa miaka mingi katika Kanda mbalimbali nchini na yamekuwa na mambo ya kuvutia sana hususani Teknolojia na mbinu bora za uzalishaji katika kilimo na mifugo ambazo zinauwezo wa kuleta tija kubwa lakini bado changamoto kubwa ni kwamba mambo yote bora na mazuri yanayopatikana kwenye Maonesho hayajaweza kumfikia mkulima kwenye ngazi za msingi kwa maana ya ngazi ya kaya na vijiji.

Alisema kuwa, unaweza kutoka umbali usiozidi kilomita mbili tu kutoka kituo (Uwanja) cha Maonesho kilipo utashangaa kukuta mkulima analima kilimo cha kienyeji ambacho hakina manufaa.

“Teknolojia inayooneshwa kwenye Maonesho haya bado haijaweza kuwafikia wakulima na wafugaji wetu kwenye vijiji vyao wanakoendesha shughuli zao za kilimo na mifugo” alisema Profesa Mwamfupe na kuongeza kuwa, bado teknolojia na ubunifu unaopatikana kwenye Maonesho haya unahitaji kuwafikia wakulima wa chini kabisa.

Alitoa wito kwa Mamlaka zinazohusika kuhakikisha Kiwanja cha Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Kati kilichopo katika Kata ya Nzuguni Manispaa ya Dodoma kinakuwa kituo cha Shamba Darasa la kilimo mifugo na uvuvi cha kudumu ili wataalamu wa kilimo na mifugo wawepo kituoni hapo kipindi chote cha mwaka wakisimamia shughuli za kilimo na mifugo kituoni hapo na Halmashauri zilete Wakulima na Wafugaji wao kujifunza na kupata suluhisho la changamoto zinazowakabili katika shughuli zao za uzalishaji.

No comments:

Post a Comment