Monday, August 21

Ukimgusa dada wa kazi umemruhusu amdharau aliyemfuata stendi




Mjini wanakwambia, ukiona swala anatamba porini ujue ana kauhusiano fulani hivi na simba mmoja. Yaani kwamba anaweza akakatiza mbele ya simba wengine, au hata akaamua kula nyasi za walipozoea kulala simba na asiguswe— anaguswaje sasa?
Iko hivyo hata kwa dada wa kazi wa nyumbani kwako— mtamtumia nauli ya kwenye ‘Nanii Pesa’, atapanda basi, atateremka stendi, mkeo atakuwa pale akimsubiri, atampokea, atamleta nyumbani, akikuona kwa mara ya kwanza atatambulishwa, atakusalimia kwa heshima, kwa kukunja goti, na wewe utamuitikia kwa hekima huku jicho lako likimfanisha na mwanao, na akili ikikuthibitishia kabisa kwamba kwa umri wake, kama Mungu angeamua kukafanya haka kasichana kuwa binti yako, wala isingekuwa miujiza.
Mkeo ataanza kumuelekeza kazi, jinsi ya kupika kwa kutumia jiko la gesi kama sio la umeme, jinsi ya kutumia ‘mop’ kupiga deki, jinsi ya kufungua jokofu na kumuelewesha nini hustahili kuhifadhiwa humo na visivyostahili hutunzwa wapi.
Na kuna siku wakati anaosha vyombo ataangusha sahani na itavunjika, mkeo atamsema kama ambavyo huwasema watoto wenu wanapokosea. Siku nyingine atapika nyama huku anatazama tamthilia kwenye runinga, nyama itaungua, mkeo atamkemea lakini kwa kiwango kile kile cha kufanana na wanavyokemewa watoto wako; hatakasirika, atajifungia chumbani, atalia kwa kuona labda ananyanyaswa, lakini mwisho wa yote atatii maagizo ya mkeo na kuendelea kumuheshimu kama bosi, kama dada, kama mama.
Lakini wewe ndiye utakayekuja kuharibu mambo; tamaa zako zisizokuwa na macho zitakutuma kuanza kukamezea mate haka katoto ulichojithibitishia kuwa hakana tofauti na wanao siku ya kwanza ulipomuona.
Utaziruhusu tamaa zikutawale na zenyewe zitakutuma kutimiza azimio lako— na kwa kuwa umempa shetani nguvu, kweli utafanikisha lengo; utatembea na dada wa kazi na usikute ni kwa kujirudiarudia.
Kifuatacho ni dada wa kazi kuanza kumdharau mkeo— akiambiwa apike chakula cha jioni, atakiivisha saa nne za usiku, akiagizwa kumuogesha mtoto atampakapaka maji na kumrudisha anateleza kama kambale. Na mkeo akithubutu kumsema atajibu, tena sio kujibu, ni kujibizana.
Mkeo ataanza kunung’unika kwamba Kidawa amekuwa jeuri siku hizi bila kujua chanzo ni nini. Kumbe chanzo ni simba wewe, ulishamtia kiburi na kumfanya ajione hana tofauti yoyote na mkeo, sasa ndio swala anatumia fursa hiyo kucheza na simba . Atafanya anavyotaka kana kwamba na yeye ni miongoni mwa wanyama wenye mamlaka mbugani; yaani kama vile na yeye ni mke ndani ya nyumba.
Tamati mkeo atajikuta kwenye vita kubwa na adui uliyemtengeneza wewe kwa tamaa za kijinga ambazo kama ungeamua ungeweza kujizuia kabisa. Hatukatai kuna nafasi ya kumsingizia shetani katika maisha yetu wanaume, lakini kuna ujinga tunafanya hata shetani anatushangaa huko alipo.

No comments:

Post a Comment