Monday, August 21

Dk Kalemani awaonya makandarasi, Tanesco




Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Merdad Kalemani amelitaka Shirika la Umeme (Tanesco) kuhakikika limeunganisha nishati hiyo katika vijiji 33 ifikapo Machoi mwakani.
Dk Kalemani pia ametaka makandarasi wanaotekeleza mradi wa kuunganisha umeme katika 242 vya Mkoa wa Arusha chini ya mpango wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), kuhakikisha wanatumia wananchi kutoka maeneo hayo ya mradi katika shughuli zao ili kuwapa ajira.
Mradi huo utakaogharimu Sh31 bilioni unafanywa na kampuni mbili za Nipo Group Limited ya Tanzania na Angelique International Limited ya India, ambao wamepewa miezi 18 kukamilisha usambazaji miundombinu ya umeme kwa awamu tatu.
Dk Kalemani alikuwa akizungumza katika uzinduzi wa mradi huo uliofanyika Kijiji cha Digodigo wilayani Ngorongoro mwishoni mwa wiki iliyopita.
Naibu waziri huyo pia aliionya Tanesco dhidi ya vitendo vya kuzidisha gharama za kuunganisha umeme katika kaya na kuunganisha nishati hiyo katika shule, zahanazi, makanisa na misikiti.
“Kazi ya kusambaza umeme hadi ngazi ya kaya si lelemama. Lazima kuhakikisha wananchi wanapata umeme,” alisema.
“Tena nataka hadi Machi mwakani vijiji 33 viwe vimepata huduma bila kuruka hata kimoja, kwa gharama ndogo ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (Vat) ambayo ni Sh27,000 kwa sababu Serikali imeshalipa gharama zote.”
Kuhusu makandarasi, Dk kalemani aliwataka kuwatumia wakazi wa eneo hilo ili kuwapa vibarua na ajira badala ya kutafuta wasaidizi nje ya eneo la mradi.
Naibu waziri huyo aliwataka makandarasi hao kuwalipa vibarua stahiki zao mapema kwa kulingana na kazi za ujuzi wao.
Dk Kalemani aliwaonya vishoka wanaokwenda kuwalaghai wananchi, wakidai fedha nyingi ya kuwaunganishia umeme, akisema hatawavumiliwa na kuwataka maofisa Tanesco kutembelea maeneo ya mradi.
Akitoa taarifa ya mradi, Mkurugenzi wa Rea, Gissima Nyamo-Hanga alisema kukamilika kwa mradi kutachochea maendeleo ya uchumi wa vijiji na kwamba, hadi Machi mwakani makandarasi wanatakiwa kukabidhi vijiji 121
“Wananchi sasa watumie nishati hii kama fursa ya kujiletea maendeleo, kama kubuni miradi ya kutumia umeme si kuendelea kukimbilia mijini,” alisema.
Naye Mbunge wa Ngorongoro, William Ole Nasha alishukuru kwa ujio wa mradi huo na kuahidi kuwahamasisha wananchi.     

No comments:

Post a Comment